Jul 15, 2023 02:46 UTC
  • Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lapitishia azimio la kulaani uchomaji wa Qur'ani

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano liliidhinisha azimio lililopendekezwa na nchi za Kiislamu la kulaani kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na kutaka uchunguzi ufanyike kuhusu jambo hilo pamoja na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu kutakiwa kutoa ripoti kuhusu suala hilo.

Azimio hilo pia linaitaka Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu na mifumo mingine ya Baraza la Haki za Binadamu kutoa mapendekezo yanayohitajika kwa nchi zote ili kuziwezesha kurekebisha mapungufu ya kisheria yanayochochea kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini. Azimio hilo lililowasilishwa na Pakistan kwa niaba ya nchi 57 za Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, limemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuchapisha ripoti kuhusu chuki za kidini na kuzitaka serikali ziangalie upya sheria zao na kurekebisha mapungufu yanayoweza kuzuia wahalifu kufunguliwa mashtaka na wakati huo huo kuchochea chuki za kidini.

Wawakilishi wa nchi za Kiislamu wamesema Uislamu ni dini ya amani na udugu, na kwamba kudhalilishwa Qur'ani Tukufu na vitabu vya dini nyingine za mbinguni kunasababisha chuki, ubaguzi na uadui, na kuwa ni katika nembo za kuchochea chuki dhidi ya Uislamu, ambazo zinapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria na kukomeshwa mara moja. Azimio hilo lilipingwa vikali na Marekani na Umoja wa Ulaya kwa madai kuwa linakinzana na maoni yao kuhusu haki za binadamu na uhuru wa kujieleza. Wamagharibi wanadai kuwa azimio hilo linakwenda kinyume na kile kinachodaiwa kuwa hatua za muda mrefu za kutetea haki za binadamu na uhuru wa kujieleza.

Waislamu wakiandamana dhidi ya kuvunjiwa heshima Kitabu chao Kitakatifu

Hii ni katika hali ambayo katika nchi za Magharibi, masuala kama vile madai ya mauaji ya Holocaust yanachukuliwa kuwa matakatifu, na kushuku au kuhoji suala hilo huambatana na adhabu kali na kifungo cha muda mrefu jela. Ni wazi kuwa Wamagharibi wanapuuza kwa makusudi tofauti iliyopo kati ya uhuru wa kusema na uhuru wa kuvunjia heshima matukufu ya dini.

Undumakuwili wa nchi za Magharibi, ikiwemo Sweden, kuhusu uhuru wa kujieleza unaonyesha kuwa suala hili huzingatiwa tu linapohoji na kuyatukana mambo yanayolengwa na nchi za Magharibi, ikiwa ni pamoja na kueneza chuki dhidi ya Uislamu na matukufu ya Waislamu, lakini linapogusa masuala kama Holocaust au hata kuchukua msimamo unaopendelea Russia katika vita vya sasa nchini Ukraine, serikali za Magharibi huchukua msimamo mkali na wa kiuhasama dhidi ya watu na serikali zinazochukua misimamo huru kama hiyo na kuzifuatilia kisheria. Mkimbizi mmoja wa Kikristo mzaliwa wa Iraq ambaye amepata uraia wa Uswidi kwa jina Salwan Momika mwenye umri wa miaka 37, siku ya Jumatano, Juni 28, alichoma moto Qur'ani Tukufu nje ya msikiti mkuu wa Stockholm, mbele ya takriban Waislamu 200 sambamba na maadhimisho ya Eid al-Adha, huku akiungwa mkono na maafisa pamoja na polisi wa Uswidi.

Kitendo hicho cha kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu kimekabiliwa kimataifa na wimbi kubwa la malalamiko na hasira ya Waislamu. Katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya nchi za Ulaya hususan eneo la Scandinavia, zimekuwa uwanja wa matusi na kuvunjiwa heshima matukufu ya Waislamu. Chini ya uungaji mkono wa polisi wa Uswidi, watu wenye itikadi kali za mrengo wa kulia wamekuwa wakipewa ruhusa ya kuchoma moto Qur'ani Tukufu, na maandamano ya Waislamu ya kulalamikia suala hilo kuzimwa kwa mabavu.

Hossein Amirabdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na kuenezwa chuki dhidi ya matukufu ya Kiislamu nchini Sweden na kuandika katika ujumbe wake wa Twitter kwamba: "Kuumiza hisia za Waislamu duniani na kueneza chuki dhidi ya Uislamu kwa kisingizio cha kutetea uhuru wa kusema halipasi kubadilishwa kuwa jambo la kawaida katika baadhi ya nchi za Ulaya zinazodai kutetea haki za binadamu."

Hossein Amirabdollahian

 

Wamagharibi wanaunga mkono kitendo cha kuchukiza cha kuchoma moto Qur'ani Tukufu katika hali ambayo Umoja wa Mataifa unapinga kitendo hicho cha aibu.

Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa anasema: Miguel Moratinos, Mwakilishi Mkuu wa Muungano wa Ustaarabu wa Umoja wa Mataifa UNAOC amelaani vikali kuchomwa moto kurasa za Qur'ani Tukufu mbele ya msikiti mmoja katikati ya mji wa Stockholm, nchini Uswidi. Farhan Haq amefafanua kuwa: Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema kitendo hicho kiovu na cha kuchukiza ni kuvunjiwa heshima Waislamu waliokuwa wanasherehekea Eid al-Adha.

Ameongeza kuwa: Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasisitiza umuhimu wa kudumishwa uhuru wa kujieleza kama haki ya kimsingi ya binadamu, lakini wakati huo huo anasisitiza kuwa kuvunjiwa heshima vitabu vitakatifu na maeneo ya ibada pamoja na nembo za kidini ni jambo lisilokubalika na linaloweza kusababisha vurugu.

Tags