Jumanne 8 Oktoba, 2024
https://parstoday.ir/sw/radio/event-i117242-jumanne_8_oktoba_2024
Leo ni Jumanne tarehe 4 Mfunguo Saba Rabiuthani 1446 Hijria inayosadifiana na Oktoba 8 mwaka 2024
(last modified 2025-10-20T07:03:11+00:00 )
Oct 08, 2024 02:18 UTC
  • Jumanne 8 Oktoba, 2024

Leo ni Jumanne tarehe 4 Mfunguo Saba Rabiuthani 1446 Hijria inayosadifiana na Oktoba 8 mwaka 2024

Siku kama ya leo miaka 1,273 iliyopita, alizaliwa Sayyid Abdul Adhim al Hassani aliyekuwa mmoja wa wajukuu wa Imam Hassan al Mujtaba (a.s) huko katika mji wa Madina.

Sayyid Abdul Adhim alikuwa mmoja kati ya shakhsiya walioaminiwa na Imam al Hadi (as) na alinukuu Hadithi moja kwa moja kutoka kwa maimamu watukufu kama vile al Ridha, al Jawad na al Hadi (as).

Sayyid Abdul Adhim alihamia Iran kutokana na pendekezo la Imam al Hadi (as) kwa ajili ya kuwaongoza Waislamu na akaishi katika mji wa Rei karibu na Tehran ya sasa. Aliuawa shahidi mwezi Shawwal mwaka 250 Hijria.

Kaburi la mtukufu huyo liko katika eneo la Rei na ni miongoni mwa maeneo yanayotembelewa na Waislamu kutoka maeneo mbalimbali duniani.   

Haram ya Sayyid Abdul Adhim al Hassani

Siku kama ya leo, miaka 933 iliyopita alizaliwa mjini Baghdad Abubakr Muhammad al Anbari, faqihi, mtaalamu wa hadithi na lugha.

Anbari alipata kusoma elimu ya dini, nahwu na lugha akiwa kijana mdogo kutoka kwa baba yake. Baada ya kuhitimu masomo yake katika nyanja tofauti, alianza kufundisha na kulea wanafunzi wengi. Alitokea kuwa faqihi mkubwa na kutabahari katika elimu ya lugha ya Kiarabu.

Msomi huyo ameandika vitabu vingi, maarufu zaidi kikiwa ni kitabu cha ‘Manshurul-Fawaaid.’   

Miaka 143 iliyopita katika siku kama ya leo, kimbunga kikubwa kilitokea nchini Vietnam. 

Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na tufani hiyo kubwa yalikuwa ya kusini mwa nchi hiyo. Kimbunga hicho kiliharibu mashamba na kubomoa kikamilifu nyumba za maeneo ya kusini mwa Vietnam. Aidha kufuatia janga hilo la kimaumbile, zaidi ya watu 300,000 waliaga dunia. ***

Katika siku kama ya leo miaka 113 iliyopita, vita vya Balkan vilianza kwa ushiriki wa Bulgaria, Serbia na Ugiriki dhidi ya Utawala wa Othmania.

Ufalme wa Othmania kwa miaka kadhaa mtawalia ulikuwa umefanikiwa kuyafanya maeneo mengi ya magharibi mwa Asia, kaskazini mwa Afrika na mashariki mwa Ulaya kuwa chini ya udhibiti wake na hivyo ukawa umetanua utawala wake.

Vuguvugu la kulitaka kujitenga nchi zilizokuwa chini ya utawala huo lilikuwa likipelekea kutokea vurugu mara kwa mara na vita vya Balkan ni moja ya harakati hizo.

Miaka 19 iliyopita katika siku kama ya leo, mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na ukubwa wa 7.8 kwa kipimo cha Rishta uliyakumba maeneo ya kaskazini mashariki mwa Pakistan.

Kitovu cha mtetemeko huo kilikuwa katika mji wa Muzaffarabad. Watu wapatao 90 elfu walipoteza maisha yao na wengine milioni 3 na laki 6 kubaki bila makazi kufuatia mtetemeko huo.