Jumatano, Februari 19, 2025
(last modified Wed, 19 Feb 2025 02:59:02 GMT )
Feb 19, 2025 02:59 UTC
  • Jumatano, Februari 19, 2025

Leo ni Jumatano tarehe 20 Sha'ban 1446 Hijria sawa na tarehe 19 Februari mwaka 2025.

Katika siku kama ya leo miaka 1061 iliyopita alifariki dunia mwanahistoria na mtaalamu maarufu wa vitabu wa Kiislamu Ibnu Nadeem.

Ibnu Nadeem alipata umaarufu kutokana na kitabu cha "al Fihrist". Katika kitabu hicho Ibn Nadeem aliarifisha taaluma na elimu zote zilizokuwepo katika zama hizo na kutoa maelezo na wasifa wa wasomi mashuhuri wa elimu hizo.

Kitabu hicho kinakusanya maelezo kamili kuhusu maulamaa na wasomi wa Kiislamu wa zamani hadi kufikia zama za Ibn Nadeem. 

Katika siku kama ya leo miaka 552 iliyopita alizaliwa mnajimu na mwanahesabati mashuhuri wa Poland, Nicolaus Copernicus.

Awali alijifunza elimu ya nujumu na baadaye tiba, na baada ya kukamilisha masomo alianza kufundisha hesabati huko Roma. Hata hivyo Copernicus aliendelea kudurusu na kufanya utafiti wa elimu ya nujumu na mwaka 1503 alivumbua nadharia ya harakati ya dunia kuzunguka jua na vilevile dunia kujizunguka yenyewe katika kila baada ya masaa 24.

Nicolaus Copernicus alifariki dunia tarehe 24 Mei 1543 siku chache tu baada ya kuchapisha kitabu cha On the Revolutions of the Celestial Spheres kinachofafanua nadharia zake. 

Nicolaus Copernicus

Miaka 74 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 19 Februari mwaka 1951 alifariki dunia mwandishi na mkosoaji mashuhuri wa Ufaransa, Andre Gide, akiwa na umri wa miaka 82.

Alizaliwa mwaka 1869 Miladia mjini Paris lakini alitumia umri wake mwingi Afrika kaskazini na hasa nchini Algeria. Visa vingi alivyoandika viliathiriwa na maisha pamoja na utamaduni wa watu bara hilo. Miongozi mwa visa vya kuvutia vilivyoandikwa na mwandishi huyo ni pamoja na "Wimbo wa kijijini" na "Meza ya Ardhi." Mwaka 1947 Gide alitunukiwa zawadi ya Nobel.   

Andre Gide

Miaka 73 iliyopita katika siku kama ya leo mwaka 1952 alifariki dunia mwandishi wa Norway, Knut Hamsun. Alizaliwa mwaka 1859 katika familia masikini kaskazini mwa nchi hiyo, na alipotimiza miaka 24 aliingia katika uwanja wa uandishi.

Hamsun alisafiri mara mbili kwenda Marekani na akaandika makosa aliyoyaona nchini humo ndani ya kitabu alichokipa anwani ya "Maisha ya Kimaanawi katika Zama Mpya Nchini Marekani" pia aliandika kitabu kilichopewa jina la "Njaa" ambacho kilibeba tamaduni mbali mbali za dunia.

Uandishi wake wa kitabu cha "Matunda ya Ardhini" ulikuwa na nafasi muhimu katika kutunukiwa zawazi ya Nobel mwaka 1920. 

Knut Hamsun

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, inayosadifiana na tarehe Mosi Esfand 1366 Hijria Shamsia, ndege ya abiria ya Iran ilishambuliwa na kutunguliwa kwa kombora la majeshi ya utawala wa kidikteta wa Saddam Hussein wa Iraq na kuangushwa, wakati wa vita vya Iran na Iraq.

Katika tukio hilo, Hujjatul Islam Fadhlullah Mahallati, mwakilishi wa Imam Khomeini kwenye Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) aliuawa shahidi akiwa pamoja na maafisa wa serikali na wabunge 39 wa Iran. 

Hujjatul Islam Fadhlullah Mahallati

Tarehe 19 Februari miaka 28 iliyopita alifariki dunia Deng Xiaoping, kiongozi wa zamani wa China na mhandisi wa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa ya nchi hiyo.

Katika kipindi cha uongozi wa Xiaoping China ilifanya mageuzi makubwa katika nyanja mbalimbali na alifanya marekebisho makubwa katika uchumi wa kisoshalisti wa wakati huo wa China na kuuelekeza kwenye uchumi wa soko. Wakati huo China ilifanikiwa kuingia katika nyanja mbalimbali za kimataifa na kutatua migogoro iliyokuwepo katika uhusiano wake na nchi kadhaa.

Deng Xiaoping alijiuzulu mwaka 1990 kutokana na maradhi na umri wake mkubwa na hadi anafariki dunia alikuwa akihesabiwa kuwa shakhsia mkubwa zaidi wa China.

Deng Xiaoping