Taathira za Mapinduzi ya Kiislamu katika Harakati ya Kuhuisha Fikra za Kidini
Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya vipindi maalumu vinavyokujieni katika kipindi hiki cha maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuwa nasi hadi mwisho.
Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalikuwa mapinduzi ya aina yake ambayo hayawezi kulinganishwa wala kufananishwa na mapinduzi yaliyotokea katika maeneo mengine ya dunia. Uwezo mkubwa wa Imam Ruhullah Khomeini kama kiongozi wa juu wa kidini, uungaji mkono mkubwa wa wananchi kwa kiongozi wao, umoja na mshikamano usio na kifani wa wananchi vyote kwa pamoja vilikuwa sababu ya kuondolewa madarakani haraka na kwa hasara ndogo utawala uliokuwa na nguvu kubwa zaidi na tegemezi kwa madola makubwa ya kibeberu duniani katika eneo la Mashariki ya Kati. Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran hapo mwaka 1979 ambao kwa hakika ulikuwa ushindi wa utamaduni na ustaarabu mkubwa wa Uislamu, uliathiri na kuvuruga mlingano wa dunia. Matukio yaliyoambatana na mapinduzi hayo yamewashangaza na kuwaacha bumbuazi wanafikra, wasomi na wachanganuzi wengi wa masuala ya siasa. Hii ni kwa sababu katika mapinduzi haya wananchi wote na kwa wakati mmoja walisimama kwa pamoja wakitaka mageuzi na mabadiliko ya kimsingi, yaani kuondolewa madarakani utawala wa kifalme wa Pahlavi na kuanzishwa serikali ya Kiislamu. Mwangwi wa harakati hiyo ulienda mbali sana kiasi kwamba mwanafalsafa, mwanahistoria na mwanafikra wa zama hizi, Michel Foucault anasema: Umoja na mshikamano wa wananchi wa Iran huenda visionekane kamwe kwa jicho kama ilivyo roho.. lakini irada na azma hiyo kubwa ilidhihirika wazi mjini Tehran na katika maeneo mengine ya Iran na kubakia hai.." Michel Foucault anasema Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalikuwa roho ya dunia iliyokuwa imekufa na mwanzo wa kurejea dini na masuala ya kiroho katika medani ya masuala ya kijamii na kisiasa duniani.
Miongoni mwa sifa makhsusi za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kwamba mapinduzi hayo yalitokea katika kipindi ambacho misingi na nguzo za dini zilikuwa zimepoteza rangi yake na kunyauka katika maeneo mengi ya dunia na watu wengi walikuwa ama wametupilia mbali imani zao au walikuwa wakificha itikadi na imani zao wakichelea kuchezewa shere na wafuasi wa fikra za kilaiki na wapinzani wa mafundisho ya dini. Katika mazingira hayo mapinduzi ya kidini yaliyokuwa na lengo la kuhuisha utambulisho wa Kiislamu na kuasisi serikali ya kidini yalileta mabadiliko makubwa si ndani ya Iran pekee bali pia katika upeo wa kimataifa. Kuhusu mabadiliko hayo makubwa gazeti la Times limeandika kuwa: "Wimbi la harakati ya dini na mapinduzi limeikumba dunia nzima na kuufanya ulimwengu wa Magharibi uvumbue upya Uislamu kutokana na Mapinduzi ya Iran." Hii ni kutokana na ukweli kwamba, watu katika maeneo mbalimbali ya dunia walielewa kwamba, Mapinduzi ya Iran sambamba na maajabu yake mengi na ushindi wake mtawalia na wa haraka ni matokeo ya kitu ambacho hakikushuhudiwa katika mapinduzi ya kabla yake nacho ni mafundisho sahihi ya dini ya Uislamu na kuhuishwa fikra na utambulisho wa Kiislamu. Mambo haya yaliwakusanya pamoja watu wa Iran na kuwapa nguvu ya kuuondoa madarakani utawala uliokuwa na nguvu zaidi wa kisiasa wakati huo katika eneo la Mashariki ya Kati.
Mtaalamu maarufu wa masuala ya jamii wa Marekani, Theda Skocpol anasema kuhusu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwamba: Kuondolewa madarakani utawala wa Shah na kuanza harakati ya mapinduzi hapo mwaka 1977 hadi 1979 kuliwashangaza wengi duniani kuanzia marafiki na waitifaki wa Shah mwenyewe, waandishi habari, na hata wasomi wa masuala ya siasa na jamii na kadhalika. Sote tulikuwa tukiyatazama matukio ya mapinduzi ya Iran kwa jicho la mshangao. Theda Skocpol anaendelea kusema kwamba: Zaidi ya yote ni kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni tukio lililokwenda kinyume na kaida na mkondo uliozoeleka.
Msomi wa Uingereza, Michael Fisher pia anaashiria nafasi na mchango wa kiongozi wa kidini wa mapinduzi ya Iran na kuandika: Mapinduzi ya Imam Khomeini yalibadili hata mwenendo wa kawaida wa ustawi wa mwanadamu, na walimwengu wote waliathiriwa na mapinduzi yake ya kiroho."
Kwa msingi huo miongoni mwa matunda makubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kuhuisha tena fikra za Kiislamu na mtazamo wa kidini duniani ambao ulikuwa umesahaulika kutokana na harakati za wasomi wa kisekulari na kilaiki. Anthony Giddens ambaye ni mtaalamu mashuhuri wa masuala ya kijamii wa Uingereza anasema: Magwiji wa elimu jamii kama Marx, Durkheim na Max Weber, kwa hitilafu ndogo, walikuwa wakiona harakati jumla ya dunia kuwa ni kuelekea kwenye usekulari na kuwekwa kando dini. Lakini mwanzoni mwa muongo wa 1980 na sambamba na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran tulishuhudia haarakati iliyokwenda kinyume na mkondo huo. Kwa maana kwamba, harakati jumla ya dunia iliekelea upande wa dini na masuala ya kiroho."
Ni ukweli usiopingika kwamba baada ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwenendo wa harakati ya dunia uliekelea kwenye masuala ya kiroho hususan katika upande wa dini ya Uislamu katika nchi mbalimbali. Mapinduzi hayo yalionesha taswira safi na halisi ya dini kama suala la kiroho na kuwadhihirishia wanadamu nafasi ya mafundisho na itikadi za kidini na mwongozo wa mwanadamu katika masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa na maisha ya mtu binafsi. Kanali ya televisheni ya BBC ya Uingereza ilikiri katika filamu yake ya matukuio ya kweli (documentary) iliyotayarishwa kwa mnasaba wa kukaribia karne ya 21 kwamba: Kilichotokea Iran mwaka 1979 ni jambo muhimu si kwa Wairani pekee bali kwa dini zote duniani... Katika maeneo mbalimbali ya dunia wafuasi wa dini nyingine kama Wakristo, Wayahudi, Wahindu na kadhalika walianza kurejea katika misingi ya dini zao. BBC iliendelea kusema: Hata nchini Uturuku ambako serikali iliingia vitani dhidi ya dini miaka 70 iliyopita, mwenendo wa watu kurejea katika mafundisho ya dini ya Uislamu ulishika kasi zaidi", mwisho wa kunukuu.
Baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran harakati ya kuelekea kwenye masuala ya kiroho na kimaanawi ilishika kasi pia katika uwanja wa sanaa kwa kadiri kwamba, hivi sasa baada ya kupita zaidi ya miongo mitatu baada ya mapinduzi hayo filamu zenye ujumbe wa kiroho na kidini zimepata mashabiki na wafuatiliaji wengi katika nchi mbalimbali. La kuvutia zaidi ni kuwa, hata studio za Hollywood ambazo awali zilikuwa zikipuuza bali hata kupiga vita masuala ya kidini, sasa zinatengeneza filamu zenye vielelezo vya kiroho na kidini.
Wakati huo huo makampuni makubwa ya kibiashara duniani pia na taasisi za utafiti na uchunguzi zimekuwa zikiwausia washirika wao kujali na kutilia maanani mwelekeo wa watu kwenye masuala ya kiroho na kidini wakati wa kutengeneza bidhaa mbalimbali. Kwa mfano tu hii leo tunaona kuwa, utengenezaji wa bidhaa za vyakula halali unashamiri pia si katika nchi za Kiislamu tu bali hata katika masoko ya Magharibi ambako jamii ya Waislamu inaongezeka kwa kasi.
Harakati ya kurejea kwenye masuala ya dini na ya kiroho baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran haikuishia hapo bali ilitinga pia katika nyanja za michezo na wanamichezo. Harakati za wachezaji kusujudu au kuinua mikono juu kuomba dua au kumshukuru Mwenyezi Mungu baada ya kufunga goli au kupata ushindi, kuongezeka idadi ya wasichana na wanawake wanaovaa vazi la staha la hijabu katika mashindano ya kimataifa ya michezo na kadhalika baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ni baadhi ya vielelezo vya taathira za mapinduzi hayo katika masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa na katika kuhuisha utambulisho wa Kiislamu.
Wapenzi wasikilizaji kuna mifano mingi sana ya taathira za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika kuhuisha masuala ya kiroho na utambulisho wa Kiislamu duniani lakini kutokana na kumalizika wakati uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki hatuna budi kuishia hapa kwa leo. Tunakutakieni kila la kheri na kwaherini.