Iran yaanza sherehe za Alfajiri Kumi za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu
Raia wa Iran leo wameanza sherehe za Alfajiri Kumi ili kuadhimisha mwaka wa 46 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaliyouangusha utawala wa kifalme wa Pahlavi uliokuwa ukiungwa mkono na kusaidiwa na Marekani.
Sherehe za kitaifa zimeanza leo Ijumaa, ambayo inasadifiana na siku ya 12 ya mwezi Bahman kwa kalenda ya mwaka wa jua.
Siku hii inaadhimisha kurudi nyumbani kwa marehemu muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, Imam Ruhullah Khomeini, baada ya miaka kadhaa ya kuishi uhamishoni.
Katika sehemu moja ya maadhimisho ya siku hii, gwaride la pikipiki lilifanyika katika mji mkuu, Tehran, na miji mingine kote nchini.
Ikiwa ni moja ya programu za maadhimisho ya leo, eneo alikoketi Imam Khomeini huko Behesht Zahra, makaburi makubwa zaidi ya Tehran kusini mwa mji huo, punde tu baada ya kurejea nchini, limepambwa kwa maua leo Ijumaa katika hafla iliyohudhuriwa na maelfu ya watu pamoja na viongozi kadhaa wa ngazi ya juu.
"Baada ya miaka 46, tumeweza kuanzisha Muqawama duniani na kuuelekeza ulimwengu kwenye dunia ya kambi kadhaa," amesema Hamidreza Hajibabaei, Naibu Spika wa Bunge la Iran, wakati wa hafla hiyo.
Ameongeza kuwa: "Katika kipindi cha miaka 46 iliyopita, watu wa Iran wamekuwa katika hali ya kujilinda katika vita vilivyoanzishwa na Marekani dhidi yetu, na mshindi wa vita hivyo daima amekuwa taifa la Iran."
Zaidi ya programu 46,000 zimetayarishwa na kuratibiwa na Baraza la Uratibu wa Uenezi wa Kiislamu katika ngazi ya kitaifa kwa ajili ya kuadhimisha sherehe za mwaka huu za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Kila mwaka, Wairani huadhimisha kumbukumbu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuanzia tarehe 1 hadi 11 Februari, ambazo hujulikana kama sherehe za Alfajiri Kumi.
Alfajiri Kumi inawakilisha siku kumi za baina ya siku Imam Khomeini aliporejea nchini baada ya kuwa uhamisho kwa karibu miaka 15 na siku Mapinduzi ya Kiislamu yalipopata ushindi kamili chini ya uongozi wa Imam Ruhullah Khomeini, tarehe 22 Bahman.

Kwa kuuangusha utawala wa Pahlavi miaka 46 iliyopita, taifa la Iran lilihitimisha miaka 2,500 ya utawala wa kifalme na kuanzisha mfumo mpya wa kisiasa wa jamhuri yenye msingi wa maadili ya Kiislamu na demokrasia.