Nafasi ya msikiti wakati wa kutokea Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale yanapokufikieni matangazo haya ya Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan huko nyumbani AfrikaMashariki. Ninakukaribisheni mjiunge nami katika kipindi hiki maalumu nilichokuandalieni kwa mnasaba wa masiku haya adhimu ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran uliopatikana mwaka 1979 kwa uongozi wa hekima na busara wa Imam Ruhullah Musawi al-Khomeini (r.a).
Kipindi chetu cha leo kitazungumzia
nafasi muhimu iliyokuwa nayo misikiti wakati wa harakati za Mapinduzi ya
Kiislamu hapa nchini. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa name hadi mwisho
wa kipindi hiki.
Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalikuwa moja ya
harakati kubwa ya wananchi ambayo ilijumuisha humo matabaka mbalimbali
ya jamii ya Iran, matabaka ambayo yote yalikuwa na ushiriki amilifu.
Kama yalivyokuwa mapinduzi mengine makubwa duniani, Mapinduzi ya
Kiislamu ya Iran nayo yalikuwa na himaya kubwa mno ya wananchi. Kwa
maana kwamba, kama mapinduzi makubwa ya Ufaransa ambayo yalitokea mwaka
1789 yakianzia katika gereza la Bastille mjini Paris, na kama katika
mapinduzi ya Oktoba mwaka 1917 nchini Russia cheche za moto wake
zilianzia baina ya wafanyakazi wa viwanda na jamii ya wakulima, vivyo
hivyo wakati wa kujiri Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran misikiti ilikuwa
kituo na kambi ya kidini na kiutamaduni na hivyo kuwa na nafasi nyeti na
muhimu katika kupanda mbegu za awali za mapinduzi na kutoa mwelekeo kwa
harakati za wananchi.
Wakati wa kujiri Mapinduzi ya Kiislamu,
misikiti ilikuwa kiunganishi baina ya viongozi wa mapinduzi na wananchi
wanamapinduzi. Kwa hakika misikiti ilikuwa na jukumu la kuwashajiisha
wananchi. Katika kipindi chote cha kutokea mapinduzi kuanzia mwanzoni
mwa muongo wa 60 hadi wakati wa kupata ushindi mapinduzi hayo mwaka
1979, misikiti ya Iran iliweza kuwa na nafasi athirifu katika kuleta
umoja na uratibu wa wananchi katika kukabiliana utawala wa Shah. Uhakika
wa mambo ni kuwa, misikiti ilikuwa ikifanya kazi kama chombo cha habari
wakati wa kujiri Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Misikitini kulikuwa
kukitolewa mawaidha, hotuba, kuenezwa vitabu, vijarida, matangazo na
kanda na kaseti zilizokuwa na hotuba na jumbe za Imam Khomeini (r.a) na
kwa muktadha huo, misikiti ikaweza kuleta mawasiliano mazuri baina ya
wananchi na kiongozi wa mapinduzi.
Katika kipindi chote cha mapambano
dhidi ya utawala wa Kipahlavi, misikiti mingi kama Msikiti wa Jalili,
Msikiti wa Lor Zadeh, Msikiti wa Quba na Misikiti ya Bazar ya Tehran
ilikuwa na harakati za mapinduzi. Katika Msikiti wa Jalili, Ustadh
Murtadha Mutahhari alikuwa akitoa darsa mbalimbali msikitini hapo na
kupelekea vijana na wanachuo wengi kuvutiwa na darsa hizo. Shahidi
Bahonar Waziri Mkuu wa pili katika Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ambaye
aliuawa shahidi na mamluki wa makundi ya kigaidi, ni shakhsia mwingine
ambaye alikuwa akienda katika Msikiti wa Jalili na kutoa hotuba.
Ayatullah Mahdavi Kani alikuwa mmoja wa watoaji hotuba wakuu katika
msikiti huo. Baada ya kumalizika Swala, Ayatullah Mahdavi Kani alikuwa
akitoa hotuba na kuzungumzia masuala mbalimbali yakiwemo yale
yanayohusiana na utawala wa Kiislamu.
Masjid al-Jawad ni msikiti
mwingine unaohesabiwa kuwa, ulikuwa amilifu na wa kimapinduzi mjini
Tehran. Msikiti huo ukiwa msikiti wa kwanza wa kisasa nchini Iran, tangu
ulipojengwa na kuanza kutumika rasmi mwaka 1342 Hijria Shamsia hadi
sasa, umekuwa na nafasi muhimu sana. Ayatullah Mutahhari alikuwa Imam wa
msikiti huo wa al-Jawad kuanzia mwaka 1349 hadi 1351 Hijria Shamsia
yaani kabla ya kutiwa kwake mbaroni. Mbali na kuswalisha katika msikiti
huo, Ayatullah Shahidi Mutahhari alikuwa akitoa hotuba zilizokuwa
zikifichua njama za utawala wa Shah na kuwaamsha wananchi. Aidha alikuwa
akiwaalika msikiti hapo, shakhsia watajika wa Kimapinduzi kwa ajili ya
kuja kutoa hotuba na hivyo kuufanya msikiti wa al-Jawad kuwa na nafasi
muhimu na yenye taathira kubwa katika harakati za mapinduzi ya Kiislamu.
Akthari ya jumuiya kama Jumuiya ya Wahandisi, Jumuiya ya Wanachuo wa
Kiislamu, Jumuiya ya Wanachuo wa Chuo cha Ufundi, Jumuiya ya Madaktari
wa Kiislamu na kadhalika, walikuwa wakivutika katika mazingira ya
Msikiti wa al-Jawad kutokana na shakhsia ya kielimu kama ya Shahidi
Mutahhari na kufanya harakati katika msikiti huo. Mfano mwingine ni
msikiti wa Hidayat wa mjini Tehran. Umuhimu wa msikiti huo ulitokana na
jina la Imam aliyekuwa akiswalisha katika msikiti huo yaani Marhumu
Ayatullah Twaliqani. Ayatullah Twaliqani alikuwa mwanazuoni
mwanamapambano ambaye baada ya kumaliza kuswalisha katika msikiti wa
Hidayat alikuwa akitoa darsa ya Tafsiri ya Qur'ani. Darsa ya Tafsiri ya
Ayatullah Twaliqani ambayo ilikuwa na sura ya kisiasa na kijamii,
ilikuwa ikiwavutia wengi na kuwafanya wakusanyike katika msikiti huo.
Utawala wa Kipahlavi ukiwa na lengo la kukabiliana na Mapinduzi ya
Kiislamu ulikuwa ukichukua hatua kali za kudhibiti misikiti. Kuichunga
misikiti na kudhibiti ratiba zake zote za kiutamaduni na vievile darsa
za Qur'ani, Darsa za Fikihi, tamthiliya, visa na usimamizi wa maktaba
lilikuwa jukumu la Shirika la Intelijinsia na Usalama wa Taifa la Iran,
maarufu kwa jina la SAVAK ambalo lilikuwa moja ya mashirika ya ujasusi
yaliyokuwa yakitisha zaidi duniani. Udhibiti wa SAVAK kwa misikiti
ulikuwa mkubwa mno kiasi kwamba, hata shughuli kama za hitima, wahusika
walikuwa wakitakiwa kabla ya kufanyika shughuli kama hiyo, watoe orodha
ya majina ya masheikh au wanazuoni watakaohudhuria katika shughuli hiyo
na hata kufanya uratibu na shirika hilo kuhusiana na shughuli kama hizo.
Wakati mwingine Shirika la Intelijinsia na Usalama wa Taifa la Iran,
lilikuwa likilazimika kufunga baadhi ya misikiti kutokana na udhaifu au
kuzidiwa na harakati za wananchi misikitini.
Pamoja na ubinyaji
na hatua za udhibiti wa msikiti haukupoteza nafasi yake maalumu katika
mapambano na harakati za Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Katika fremu
ya kutoa mwogozo na muelekeo kwa wanamapinduzi, misikiti ilikuwa na
nafasi muhimu pia katika kutatua shida za kifedha. Kuasisiwa katika
misikiti mifuko ya utoaji mikopo ilikuwa moja ya njia za kuunga mkono
Mapinduzi ya Kiislamu. Akthari ya matajiri wa Kiislamu ambao walikuwa na
mfungamano wa karibu na misikiti walikuwa wakiona kuwa ni jukumu lao la
kidini kugharamia na kutoa fedha kwa ajili ya kuhudumia misikiti.
John
D. Stempel mwandishi wa kitabu cha "Inside the Iranian Revolution"
yaani "Ndani ya Mapinduzi ya Iran" anaandika kuhusiana na hilo kwamba,
Bazar na msikiti daima vilikuwa na ushirikiano, gharama za Vyuo Vikuu
vya Kidini na harija za karibu asilimia 80 za wanazuoni zilikuwa
zikigharamiwa na kudhaminiwa na wafanyabiashara hawa. Mwisho wa kunukuu.
Katika
upande wa tablighi na upashaji habari pia, misikiti ilikuwa na taathira
kubwa mno ikiwa kama kituo cha harakati za mapinduzi. Kwa hakika wakati
wa kujiri Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, misikiti ilikuwa ikienda na
wakati kikamilifu kuhusiana na matukio ya kisiasa na hali ya kijamii na
kama ikitokea tukio la kuvunjia heshima Uislamu au kuhujumiwa maslahi ya
nchi, basi cheche za malalamiko ya wananchi na maulama zilikuwa
zikianzia msikitini. Kwa mfano mwaka 1962, hotuba ya Imam Khomeini
katika Msikiti wa A'adham mjini Qum akilalamikia Mapinduzi Meupe,
ilikuwa cheche ya kwanza ya mapinduzi. Kwa mtazamo wa Imam Khomeini ni
kuwa, Mapinduzi Meupe ya Shah yalikuwa yakikinzana na misingi ya sheria
za Kiislamu.
Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran pia,
misikiti imeendelea kuwa ni ufunguo muhimu katika kuendelea kubakia
Mapinduzi ya Kiislamu. Hii leo baada ya kupita miaka 37 tangu kupatikana
ushindi wa Mapinduzi Kiislamu hapa nchini, misikiti imeendelea na
juhudi zake za kulinda utambulisho wa kidini wa wananchi wa Iran.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu maalumu kwa leo umefikia tamati tukutane tena wakati mwingine.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.