Leo katika Historia, Jumatatu 24 Julai
Leo ni Jumatatu tarehe 6 Muharram 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 24 Julai 2023.
Tarehe sita Muharram mwaka 61 Hijria yaani miaka 1384 iliyopita katika siku kama hii ya leo mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) aliyekuwa Karbala alimwandikia barua fupi lakini muhimu sana ndugu yake, Muhammad bin Hanafiyya na wafuasi wake kadhaa waliokuwa Madina. "Barua hiyo ilisema: Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu. Hakika anayejiunga nami atapata daraja ya kuuawa shahidi, na ambaye hatajiunga nami hatapata ushindi." Barua hii ilikuwa na ujumbe kadhaa, miongoni mwa ujumbe hizo ni kwamba, Imam Hussein alikuwa akijua kuwa, atauawa shahidi yeye na masahaba wake katika mapambano yake na mtawala dhalimu, Yazid bin Muawiya. Pili ni kwamba aliweka wazi hatima ya wale wote watakaofuatana naye katika mapambano ya Karbala na kwamba wote watauawa, na hivyo mtu yeyote mwenye malengo tofauti bora arejee Madina.

Siku kama ya leo miaka 1384 iliyopita, Habib Bin Madhahir, mmoja wa masahaba wa Mtume Muhammad (saw) na mfuasi wa kweli wa Imam Hussein (as), aliwalingania watu wa kabila la Bani Asad kwa ajili ya kwenda kumsaidia mjukuu huyo wa Nabii wa Allah. Katika siku hiyo, sahaba huyo wa Mtume aliomba idhini kwa Imam Hussein (as) kwa kusema: “Ewe mjukuu wa Mtume, katika maeneo haya jirani wanaishi watu wa kabila la Bani Asad, ikiwa utaniruhusu nitaenda kwao nikawalinganie, huenda Mwenyezi Mungu akakuokoa kutokana na shari ya watu hawa makatili kupitia uwepo wa watu wa kabila la Bani Asad.” Imam Hussein alimruhusu Habib Bin Madhahir ambaye alitoka majira ya usiku kwenda kwa watu wa kabila hilo akiwataka wamsaidie mjukuu huyo wa Mtume. Akiwa katika linganio hilo, sahaba huyo wa Mtume alisema: “Kwa kuwa nyinyi ni watu wa ukoo na kabila langu, ninakulinganieni kufuata njia hii, leo ninakuombeni msikie usia wangu na mfanye haraka kwenda kumsaidia Imam Hussein (as) ili mpate utukufu wa dunia na Akhera.” Kutokana na wito huo, watu wachache kutoka kabila hilo wanaokadiriwa kufikia 90 walisimama na kwenda kumsaidia mjukuu huyo wa Nabii wa Allah. Hata hivyo baadaye walitoroka na kurejea makwao baada ya kufahamu kwamba jeshi la Omar Bin Sa’ad lilifahamu nia yao, hivyo walihofia kuuawa na jeshi hilo. Baada ya Imam Hussein kusikia habari hiyo, alisema: “Laa haula walaa quwwatan illa Billah.”

Siku kama ya leo miaka 1039 iliyopita inayosadifiana na tarehe 6 Muharram mwaka 406 Hijria, alifariki dunia Sayyid Muhammad Hussein Musawi Baghdadi, msomi mashuhuri, mwanafikra na mshairi wa Kiislamu. Aalim huyo pia alijulikana kwa jina la Sayyid Radhi. Alipata elimu za wakati huo katika kipindi cha ujana wake akiwa pamoja na ndugu yake, Sayyid Murtadha, ambaye pia alikuwa msomi mtajika. Sayyid Radhi aliinukia kuwa msomi mkubwa katika taaluma za fiqhi, tafsiri ya Qur'ani Tukufu na elimu nyingine za Kiislamu. Msomi huyo alikuwa wa kwanza kuasisi chuo kikuu kwa mtindo wa kisasa na ameandika zaidi ya vitabu 20 katika taaluma za fiqhi, tafsiri ya Qur'ani, historia na fasihi ya Kiarabu. Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni Nahjul Balagha ambacho kinakusanya semi, hotuba, amri, barua na mawaidha ya Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as).

Siku kama ya leo miaka 240 iliyopita Simón Bolívar mwanasiasa na mwanamapinduzi maarufu wa Amerika ya Kusini alizaliwa huko Caracas mji mkuu wa Venezuela. Simon Bolivar alikomboa ardhi kubwa ya Amerika ya Kusini kutoka katika makucha ya ukoloni wa Kihispania. Vilevile alikuwa na mchango mkubwa katika mapinduzi ya Caracas na kufanikiwa kuiteka Bogota huko katikati mwa Colombia. Simon Bolivar aliteuliwa kuwa Rais na Congress iliyokuwa imeundwa kwa shabaha ya kuasisi Colombia Kubwa na alifanikiwa kuzikomboa ardhi za Colombia, Venezuela na Panama. Mwaka 1822, mapambano ya ukombozi yaliyokuwa yakiongozwa na Bolivar yalienea pia hadi Ecuador na nchi hiyo ikajiunga na Colombia Kubwa, baada ya kupata uhuru.

Miaka 221 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, alizaliwa mwandishi maarufu wa Kifaransa Alexandre Dumas. Dumas aliandika riwaya nyingi kuhusiana na mapinduzi na historia ya Ufaransa kwa kustafidi na hadithi alizosimuliwa na baba yake ambaye alikuwa jenerali wa jeshi pamoja na kumbukumbu binafsi za wananchi kuhusu mapinduzi yalitokea nchini Ufaransa.

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita Jumuiya ya Mataifa iliipatia mamlaka rasmi serikali ya Uingereza ya kuzidhibiti Palestina, Iraq na eneo la mashariki mwa Jordan huku usimamizi wa Syria na Lebanon ukipewa serikali ya Ufaransa. Hata hivyo Paris na London ziliafikiana katika Vita vya Kwanza vya Dunia na baada ya hapo juu ya kugawana utawala wa kifalme wa Othmania na uamuzi huo wa Jumuiya ya Mataifa ulihalalisha suala hilo.

Miaka 79 iliyopita katika siku kama ya leo, kikosi cha anga cha jeshi la Uingereza kiliishambulia vikali bandari muhimu ya Hamburg huko kaskazini mwa Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Mashambulizi ya anga ya Ujerumani na Uingereza yalianza mwanzoni mwa Vita vya Pili vya Dunia na kushadidi zaidi baadaye. Kwa kadiri kwamba raia wengi wa nchi mbili hizo waliuawa katika mashambulizi hayo. Makumi ya maelfu ya raia wa kawaida waliuawa kwa umati katika mashambulizi ya kikosi cha anga cha Uingereza dhidi ya bandari ya Hamburg mbali na kuangamizwa taasisi kadhaa za kijeshi na kiuchumi.

Katika siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, baada ya kutiwa mbaroni Imam Khomeini na vyombo vya usalama vya utawala wa Shah, maulamaa kadhaa na marajii kutoka Qum na Mash'had na miji mingine ya Iran walifunga safari na kuelekea Tehran. Mbali na kuandika barua wakithibitisha daraja ya Umarjaa ya Imam Khomeini walitoa wito wa kuachiliwa huru mwanazuoni huyo. Hatua hiyo sambamba na kuendelea upinzani wa wananchi dhidi ya kutiwa mbaroni Imam Khomeini, kuliulazimisha utawala wa Shah kumhamisha kiongozi huyo kutoka jela na kumpeleka katika nyumba moja ili kuwatuliza maulama na wananchi hao. Siasa hizo za kutuliza mambo hazikuwa na taathira na kwa msingi huo utawala wa Shah ukiwa na lengo la kuweka pengo baina ya Imam Khomeini na wafuasi wake, uliamua kumbaidishia mwanazuoni huo nchini Uturuki na mwaka mmoja baadaye nchini Iraq.

Imam Khomeini akipelekwa uhamishoni nje ya nchi