Aug 06, 2023 11:29 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (73)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji wa Radio Tehran Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran popote pale yanapokufikieni matangazo haya. Karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili kwa pamoja tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu.

 

Kipindi chetu kilichopita kilimzungumzia Hassan Ali Nokhodaki Isfahani ambaye alizaliwa 4 Mei 1863 katika mji wa Isfahan Iran. Tulieleza kwamba, tangu utotoni Hassan-Ali alikuwa pamoja na baba yake kila usiku ambao alikuwa akikesha na kufanya ibada. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 73 ya mfululizo huu, kitamzungumzia Sayyid Hassan Modarres, msomi na alimu mwingine wa Kishia aliyekuwa na mchango mkubwa sana katika harakati za kielimu na kisiasa. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuuwa pamoja name hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Mwaka 1278 Hijria, katika nyumba ya Sayyid Ismail Tabatabai, mmoja wa masayyid na masharifu ambao nasaba yao inaishia kwa Imam Hassan (as) alizaliwa mtoto aliyepewa jina la Hassan. Familia ya mtoto huyu ilikuwa mashuhuri kwa elimu, maarifa na kulikuweko na wanazuoni na Maulamaa mahiri waliotokea katika familia hiyo. Familia yake ilikuwa ikijidhamiania maisha kupitia kilimo. Sayyid Hassan alipokuwa na umri wa miaka 6 alipelekwa kwa babu yake Mir Abdul-Baqi aliyekuuwa akijishughulisha na mahubiri na uenezaji wa mafundisho ya dini katika eneo la Qamsheh katika mji wa Isfahan Iran ili amfundishe dini. Mir Abdul-Baqi alifanya kila awezalo ili kumfundisha elimu na masomo ya dini Sayyid Hassan na kumjenga ili aje kuwa alimu mtegemewa. Kipaji alichokuwa nayo pamoja na bidii ya kusoma vilimfanya akwee haraka haraka daraja za kielimu. Akiwa na lengo la kujiendeleza zaidi kielimu aliondoka kwa babu yake na kujiunga na chuo cha mji huo katika zama hizo na kubakia katika chuo hicho kwa muda wa miaka 13. Alisoma falsafa na Irfan kwa Ustadh Mirza Jahangir Khan Qashqaei. Baada ya hapo, kutokana na kiu ya masomo aliyokuwa nayo, alifunga safari na kuelekea katika mji wa Najaf Iraq na akiwa huko alihudhuria darsa na masomo ya walimu watajika katika zama hizo kama Mirza Shirazi wa kwanza. Alibakia katika Hawza na chuo cha kidini cha Najaf kwa muda wa miaka 7. Alirejea Isfahan baada ya kupata daraja ya Ijtihadi na kuanza kufundisha katika chuo cha dini cha mji huo. Ni katika miaka hiyo ambapo kutokana na kutabahari kusiko na mithili katika kufundisha aliondokea kuwa mashuhuri kwa lakabu ya Modarres (mwalimu mfundishaji) na baada ya hapo, watu wote walimtambua kwa jina la Sayyid Hassan Modarres.

Maisha ya Sayyid Hassan Modarress yalisadifiana na matukio ya harakati za mapinduzi makubwa Iran na duniani, kama vile katika maeneo yote ya dunia  yalitaka kupinduliwa juu chini. Mapinduzi ya katiba nchini Iran, Vita vya Kwanza vya Dunia na Mapinduzi makubwa ya Russia, yote yalikuwa katika hali ya kutokea. Katika ulimwengu huu uliokuwa unafukuta joto na vuguvugu la mapinduzi, Sayyid Hassan Modarres daima alikuwa akifuatilia na kupigania uadilifu na tangu mwanzo alipoanza tu kufundisha katika chuo cha kidini cha Isfahan ambapo alikuwa akipinga vikali miamala na vitendo vya watawala na alikuwa akifanya jitihada kuzuia dhulma na ukandamizaji dhidi ya watu kwa kutumia mantiki na hoja madhubuti.

 

Sambamba na kufundisha, Hassan Modarres alikuwa akifuatilia na kushughulikia hali ya matalaba (wanafunzi wa masomo ya dini), vyuo vya kidini pamoja na wakfu zake na alikuwa akiwashinikiza wasimamizi wake watumie vipato vinavyopatikana kwa ajili ya kushughulikia matatizo ya wanafunzi wa dini. Katu Hassan Modarres hakuwa akisalimuu amri mbele ya mambo ya uhalifu na mambo yasiyo ya kimantiki na hakuwa akisita hata kidogo kutekeleza uadilifu. Moyo wake wa kutosalimu amri ulilikwamisha kundi la kutanguliza mbele maslahi yake na ni kutokana na sababu hiyo kwa mara ya kwanza likachukua uamuzi wa kutaka kumuua. Hata hivyo, kwa bahati nzuri alinusurika katika jaribio la kutaka kumuua na watu waliokuwa na nia mbaya na yeye wakashindwa kufikia malengo yao.

Sayyid Hassan Modarress

 

Miaka minne baada ya Modarres kuwa katika mji wa Isfahan, Mapinduzi ya Katiba nchini Iran yakapata ushindi. Tangu awali Modarres alikuwa akiafikiana na mapinduzi hayo kwani alikuwa akiamini kwamba, hiyo ni njia ya kukata mikono ya madhalimu. Baada ya ushindi wa awali wa wapigania katiba, uongozi na usimamizi wa miji ulikabidhiwa kwa jumuiya za mikoa na Modarres akawa mmoja wa wajumbe wa jumuiya ya mkoa wa Isfahan. Ni katika kipindi hiki ambapo Samsam al-Saltane, kamanda wa vikosi vya wapigania mapinduzi wa Kibakhtiyar, alichukua jukumu la kuongoza mji wa Isafahan na alikusudia kufidia hasara zilizotokana na vita na utawala wa Qajar kupitia ukusanyaji kodi kutoka kwa wananchi wa Isafahan. Akiwa na nia ya kutekeleza mpango huo aliwashinikiza wananchi na hata kufikia kutumia mabavu. Modarres ambaye alikuwa na taarifa ya hilo alijitokeza na kuwauunga mkono wananchi. Samsam al-Saltaneh alitoa amri ya kupelekwa uhamishoni Hassan Modarres. Wananchi wa Isfahan nao wakiwa na lengo la kumuunga mkono Modarres walifunga masoko yote na wakawa wakimfuata Modarres na wao wakiwa na nia ya kuondoka katika mji huo.

Msimamo na hatua hii ya wananchi ilimlazimisha Samsam al-Saltaneh aache kutumia mabavu na Modarres akarejea Isfahan katika anga ya saut na nara kubwa za wananchi zilizokuwa zikimuombea dua na kumtakia umri umre. Mwaka 1909 Modarres alitangazwa na Maulamaa wa Najaf kama mmoja wa Maulamaa msomi zaidi. Hii ilikuwa ni baada ya Bunge la pili la Kitaifa kutangaza uwepo wake. Ilikuwa kwamba, kwa mujibu wa sheria kamilisho ya katiba, Maulamaa wawe wasimamizi wa maazimio ya Bunge. Sayyid Modarres aliingia Bungeni katika hali ambayo, hakuna mtu aliyekuwa akitaraji hilo kwamba, mwanazuoni huyu mwembamba mwenye mkongojo mkonini ataweza kushika hatamu za uongozi wa masuala ya Bunge. Baada ya hapo, Modarres alichaguliwa katika duru nne zilizofuata za Bunge kama mwakilishi wa wananchi wa Tehran. Kuna duru moja alikuwa Spika wa Bunge na kiongozi wa chama cha waliowengi Bungeni.

Samsam al-Saltane,

 

 

Sambamba na kuchaguliwa Bunge la pili la taifa nchini Iran, Russia na Uingereza zilitumia udhaifu wa serikali kuu kadiri walivyoweza na kutiliana saini mkataba wa kifidhuli wa kuigawa ardhi ya Iran. Maeneo mbalimbali ya Iran wakati huo yalikuwa yakishuhuudia vuguvugu na harakati za upinzani za wananchi dhidi ya uwepo wa maajinabi katika ardhi ya nchi yao. Hali ya mambo ya kifedha na kijeshi ilikuwa mbaya ambapo hakuna serikali ambayo ilikuwa na uwezo wa kudhibiti na kusimamia vyema mambo. Bunge likiwa na nia ya kulipatia ufumbuzi tatizo hilo lilipasisha uamuzi wa kumleta hapa nchini Mmarekani William Morgan Shuster ili aje kuwa mweka hazina mkuu. Hata hivyo baada ya muda, mfupi Russia ikagundua kwamba, uwepo wa William Morgan Shuster si kwa maslahi yake na katika hali ya ujeuri kabisa, ikaitaka Iran imtimue Mmarekani huyo. Si hayo tu,Russia ilitishia kwamba, kama matakwa yake hayatatekelezwa basi itavamia Iran.

Ijapokuwa bunge lilisimama kupinga dhulma, utumiaji mabavu na upendaji makuu wa Russia, lakini serikali ya Wathouq al-Daulah, Waziri Mkuu ilikuwa ikiona kwamba, haina ubavu wa kukabiliana na majeshi ya Urusi, ilivunja bunge na kukubali pendekezo la Russia. Matokeo yake, Mmarekani Morgan Shuster hakuweza kuendelea na shughuli zake zaidi ya mwaka mmoja nchini Iran na hivyo akarejea Marekani.

William Morgan Shuster

 

Miaka miwili baada ya kutimuliwa kwa Morgan Schuster kutoka Iran, bunge la tatu lilifunguliwa huku ulimwengu ukikaribia kuingia katika vita vya dunia. Iran ilitangaza kutoegemea upande wowote katika vita hivi, lakini majeshi ya washirika, yaani serikali ya Urusi na Uingereza, yalikalia kwa mabavu maeneo ya kaskazini na kusini mwa Iran. Kutokana na uwepo wa jeshi la Urusi na Uingereza nchini Iran, njaa kubwa ilitokea, na karibu nusu ya watu wa Iran walikufa kwa njaa au kwa magonjwa.

Katika mazingira haya, wanazuoni wa Kiislamu walitangaza Jihad dhidi ya majeshi washirika na katika kutetea dola ya Uthmaniyya, na wanazuoni wa Iran wakiwafuata wanazuoni wa Najaf waliwaita watu kukabiliana na wavamizi.

Maisha ya heka heka ya Sayyid Hassan Modares yanaendelea na katika kipindi chetu kijacho tukusimulieni yale aliyokumbana nayo mwanazuoni na mwanamapambano huyu katika kipindi fulani cha historia pamoja na yale aliyokumbana nayo.

Wathouq al-Daulah,

 

Basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo, nikakuageni nikikutakieni kila la kheri.