Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (78)
Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili tuweze kwa pamoja kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu.
Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 78 ya mfululizo huu kitatupia jicho kwa muktasari historia, maisha na harakati za Sayyid Hussein Tabatabai Qummi. Nataraji mtakuwa pamoja nami hadi tamati ya dakika hizi chache kutegea sikio yale niliyokuandalieni juma hili. Karibuni.
Sayyid Hussein Tabatabai alizaliwa tarehe 28 Rajab mwaka 1282 Hijria mwafaka na 1865 Miladia katika mji mtakatifu wa Qom, kusini mwa mji mkuu wa Iran, Tehran. Nasaba yake inaishia kwa Imam Hassan Mujtaba (a.s.). Seyyid Hussein alisoma masomo ya awali na ya msingi huko Qom na akaenda Tehran kumaliza elimu yake mwanzoni mwa miaka yake ya ujana. Akiwa na umri wa miaka 22, aliondoka kwenda Hijja na aliporudi kutoka katika safari hii ya kiroho, aliamua kuishi Samarra Iraq kwa muda wa miaka miwili na kushiriki katika masomo ya Mirza Shirazi wa Kwanza.
Seyyid Hossein Tabatabai, baada ya kupitia hatua mbalimbali za kielimu huko Tehran, Samarra, Karbala na Najaf, mwaka 1321 Hijria mwafaka na 1903 Miladia akaondokea kuwa miongoni mwa wanafunzi mahiri na wakubwa wa Marjaa mkubwa Mirza Shirazi wa Pili. Mwalimu wake alikuwa akimzingatia kwa namna maalumu.
Ilikuwa imepita miaka kumi tangu Seyyid Hassan Tabatabai aanze kukaa na kuishi katika mji wa Samarra wakati watu wa Mashhad walipomwomba Ayatullah Muhammad Taqi Shirazi, au Mirza Shirazi wa Pili kama anavyojulikana pia amtume mjuzi na mwenye uwezo na uchamungu na mujtahid katika mji huo ili watu wamrejee na kupata muongozo katika masuala mbalimbali ya kidini na kijamii.
Alipendekeza jambo hili muhimu kwa Seyyid Hussein Tabatabai ambaye naye alikubali kuchukua jukumu hii kwa heshima ya mwalimu wake. Hatimaye baada ya miaka arobaini ya hima mtawalia katika njia ya kutafuta elimu aliondoka na kuelekea Mash'had Iran kwa minajili ya kuchukua jukumu la kuwa kiongozi wa watu katika masuala ya dini jirani na Haram ya Mtukufu Imam Ridha (a.s.).
Sayyid Hussein Tabatabai, ambaye sasa alikuwa akijulikana kwa jina la Haj Agha Hussein Qommi, aliingia Mashhad mwaka 1322 Hiijria sawa na 1904 Miladia na kuanzia siku za mwanzo kabisa, kwa kuongoza Sala za jamaa, alianzisha uhusiano wake na watu na akijikita pia katika kueneza hukumu na sheria za dini sambamba na kujibu maswali mbalimbali ya watu.
Aliweka katika ajenda zake suala la kuwahudumia wastadhaafu na wasio na uwezo huku akichukua pia jukumu la uongozi na usimamizi wa Hawza (Chuo cha kidinii) ya Mash'had. Katika kipindi hiki, Iran ilikuwa na misukosuko mingi ya kisiasa na aliwasaidia watu walioshikamana na dini wa Mashhad na alikuwa pamoja nao katika dhiki na faraja.
Moja ya matukio muhimu zaidi liliotokea wakati askari ambaye kila mtu alimfahamu kama "Reza Khan Mirpanj" akipata himaya na msaada wa Waingereza kwanza alipofanikiwa kuwa waziri wa vita na kisha akawa mfalme. Mwanzoni, alikuwa akijitambulisha kuwa ni Mwislamu mwenye ghera na taasubi na dini yake, kwa sababu alikuwa akifahamu vyema kwamba nchini Iran kuna mizizi mirefu na mikongwe ya dini na kwamba, hatua yoyote inayokwenda kinyume na matakwa ya kidini ya watu haitafanikiwa.
Baada ya Reza Khan kushika hatamu za ufalme, taratibu aliiweka kando sera yake ya zamani ya kidini na ili kuiondoa dini tukufu ya Kiislamu katika jamii ya Kiirani, aliwakandamiza na kuwadhoofisha wanazuoni na wahubiri wa Kiislamu na akatangaza wazi na bayana kwamba, dini ni kinyume na ustaarabu na mambo ya kisasa na yanayokwenda na wakati.
Moja ya hatua za Reza Shah dhidi ya dini na mwelekeo wa Magharibi, ambayo ilisababisha uasi wa watu, ilikuwa ni kupiga marufuku vazi la staha ya Kiislamu yaani hijabu kwa wanawake. Hili lilitokea mwaka 1934 na kwa hakika liliwanyima wanawake wengi waumini wa Iran maisha ya kijamii.
Mahudhurio na uwepo katika mikusanyiko kuliwalazimu kuvua hijabu, na wanawake hawakuwa tayari kuweka kando vazi lao tukufu la staha ya Kiislamu, hivyo walipendelea kukaa nyumbani.
Katika kutekeleza njama hii, Reza Khan alionyesha unyeti zaidi kwa miji kadhaa mikubwa na ya kidini, ikiwa ni pamoja na miji mitakatifu ya Mash'had na Qom, kwa sababu kama wanawake wa miji hii miwili wangekubali kuvua na kutupa hijabu, basi jambo hili lingewezekana kutekelezwa kwa urahisi na bila wasiwasi katika miji mingine. Kwa muktadha huo, Reza Khan aliweka mashinikizo zaidi kwa miji ya kidini.
Wanazuoni na Mujtahidina wa Mashhad walifanya vikao kadhaa vya kupinga sera hii, na katika moja ya mikutano hiyo ambao ulifanyika kwenye nyumba ya Hussein Qommi", mwanazuoni huyo alionyesha kuguswa sana na jambo hili na alilia kwa uchungu kuhusiana hali iliyokuwa ikitawala nchini na mashinikizo yaliyokuwa yakifanywa dhidi ya Uislamu kisha akasema: "Leo Uislamu unataka kujitolea." Ni juu ya watu kuanzisha harakati."
Hatimaye wanazuoni wakafikia uamuzi kwamba Haj Agha Hossein Qummi aende Tehran kuzungumza na Reza Khan kupinga vitendo vyake. Hussein Qummi akakubali kuchukua jukumu hilo na akatangaza kwamba, ikiwa Reza Khan hataacha vitendo vyake haramu, atasimama na kuendesha mapambano hadi tone lake la mwisho la damu.
Kabla ya kuondoka kuelekea Tehran, Hussein Qummi alituma telegrafu kwa Reza Khan na kumfahimisha mfalme Shah na baraza lake la mawaziri sababu ya kuelekea huko. Baada ya kuwasili Tehran, kundi la watu lilimtembelea kila siku na kutangaza kuwa tayari kwa ajili ya kujitolea kwake kufa kwa namna yoyote.
Uwepo mkubwa wa watu ulimfanya Reza Khan aingiwe na hofu na wahaka. Ni kwa sababu hiyo, makazi ya Ayatullah Qummi yalizingirwa na ikapigwa marufuku kumtembelea. Habari za kukamatwa kwa Ayatullah Qummi zilifika Mashhad na kubadilisha hali ya mji huo.
Watu wengi walifanya mgomo wa kuketi katika Msikiti wa Gohar Shad karibu na haram tukufu ya Imam Ridha (AS), makundi mbalimbali ya watu kutoka Mashhad na vijiji vya jirani yalisonga mbele kuelekea Msikiti wa Gohar Shad na kujumuika na umati wa watu na Maulamaa waliokuweko katika msikiti huo. Yakatokea mapigano baina ya maaskari na wananchi. Hata hivyo matukio makubwa zaidi yalikuwa yanakuja. Katikati ya usiku, askari wa Reza Khan walitumwa katika maeneo nyeti ya Msikiti wa Goharshad na maeneo ya kando kando yake.
Bunduki nzito za rashasha ziliwekwa kwenye paa la msikiti zikiwa zimeelekezwa katika ua wa msikiti huo na kuanza mashambulizi. Kulipopambazuka, takriban watu elfu tano walikuwa wameuawa shahidii na kujeruhiwa. Miili ya watu ilikuwa imelala kwenye damu katika Msikiti wa Goharshad.
Baada ya tukio hili la umwagaji damu, Reza Khan alimpeleka uhamishoni Hussein Qummi huko Iraq.
Kuaga dunia Ayatullah Mirzai Shirazi wa Pili, kulipelekea kudhoofika Hawza ya Karbala. Hata hivyo kwa kuwasili Haj Agha Hussein Qomi huko Karbala, chuo kikuu hiki cha kidini kikapata uhai. Hatua na harakati zake zilibadilisha hali jumla ya Hawza ambapo kwa mara nyingine tena kukaanza kushuhudiwa vikao vya kielimu na darsa mbalimbali tena kwa kiwango cha ustawi. Mnamo 1941 wakati wa kuendelea Vita vya Pili vya dunia na vikosi vya Uingereza na Urusi viliingia nchini Iran na Waingereza walimwondoa Reza Khan kutoka nafasi yake na badala yake kumtambua rasmi mwanawe yaani Muhammad Reza kuwa Shah na mfalme wa Iran. Ayatullah Qummi alitumia fursa hiyo na akahitimisha maisha yake ya uhamishoni kwa kuelekea Mash'had.
Hatua yake ya kwanza aliyoichukua baada ya kufika Mash'had ilikuwa ni kutuma telegrafu kwa serikali na kutaka utekelezaji sahihi wa sheria za Kiislamu. Muda fulani ulipita, lakini serikali haikukusudia kuyakubali mapendekezo ya wanazuoni kama ilivyokuwa huko nyuma, hivyo Ayatullah Qomi akatangaza hadharani vita na serikali. Hatua hii ilikaribishwa na wasomi na watu. Vuguvugu hili la umma hatimaye lilimlazimiisha mfalme na watumishi kukubali matakwa ya raia na wanazuoni.
Baada ya ushindi huu, Ayatullah Qummi alirejea Karbala na kuendelea kusoma na kufundisha masomo ya dini hadi mwisho wa maisha yake. Hatimaye, mwanachuoni huyu mwanamapambano aliaga dunia mnamo 14 Rabiu al-Awwal 1366 Hijria mwafaka na 1947 Miladia akiwa na umri wa miaka 84 na kuzikwa katika haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) katika mji wa Najaf, Iraq.
Wapenzi wasikilizaji muda uliotengwa kwa ajilii ya kipindi hiki umefikia tamati kwa juma hili, msisite kujiunga nami tena wiki ijayo, katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.
Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh