Jumatatu, tarehe Mosi Januari, 2024
Leo ni Jumatatu tarehe 18 Jamadithani 1445 Hijria sawa na tarehe Mosi Januari 2024.
Leo ni tarehe Mosi Januari inayosadifiana na kuanza mwaka mpya wa 2024 Miladia. Mpangilio wa miezi ya mwaka wa Kirumi unaoanza Januari hadi Disemba ulianza kutumiwa katika kipindi cha Mfalme Numa Pompilius wa Roma yapata miaka 700 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa Masih (as). Kwa msingi huo tarehe 31 Disemba huwa siku ya mwisho ya mwaka wa Miladia na usiku wa kuamkia tarehe Mosi Januari huanza sherehe za kupokea mwaka mpya katika jamii za Wakristo na nchi nyingi za Afrika, America, Ulaya, Australia na hata Asia. Tunawatakia heri ya mwaka mpya watu wote wanaoadhimisha mwaka huu.
Siku kama ya leo miaka 426 iliyopita aliuawa shahidi Kadhi Sayyid Nurullah Shushtari, faqihi, mwanatheolojia na alimu mkubwa. Alizaliwa mwaka 956 Hijiria katika familia bora na ya kielimu mjini Shushtar, kusini magharibi mwa Iran. Sayyid Nurullah Shushtari alijifunza masomo ya awali ya kidini kwa baba yake na kisha akaelekea mjini Mash’had, kaskazini mashariki mwa Iran na kuweza kustafidi na elimu kutoka kwa maulama wakubwa wa mji huo. Yapata mwaka 993, Kadhi Sayyid Nurullah Shushtari alielekea India kwa ajili ya kufanya tablighi ambapo wakati huo nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala wa Mfalme Akbar Shah katika silsila ya Mongolia. Hadhi yake, elimu na uadilifu wa Sayyid Shushtari vilimfanya ateuliwe kuwa kadhi wa mji wa Lahore nchini humo. Baada ya kufariki dunia Mfalme Akbar Shah, wapinzani wa alimu huyo walimwendea mfalme aliyechukua uongozi kwa jina la Jahangir Shah na kumwambia maneno ya uongo na ya uchonganishi ambapo kwa kutumia kisingizio cha madhehebu ya Shia ya alimu huyo mkubwa akauawa shahidi katika siku kama ya leo. Sayyid Nurullah Shushtari aliandika vitabu kadhaa miongoni mwavyo ni ‘Majaalisu-Mu’miniina’ ‘Ihqaaqul-Haqqi’ na ‘Tuhfatul-Uquul.’
Miaka 220 iliyopita sawa na tarehe Mosi Januari mwaka 1804 nchi ya Haiti ilijitangazia uhuru ikiwa nchi ya kwanza kufanya hivyo katika eneo la Amerika ya Latini. Uhuru wa Haiti ulipatikana kufuatia mapambano na harakati kubwa ya watumwa weusi wa nchi hiyo dhidi ya vitendo vya utumwa vya Ufaransa na kisha baadaye kuanzisha mapambano dhidi ya jeshi la Ufaransa. Ufaransa ilianza kuikoloni Haiti mwaka 1677. Baada ya kujipatia uhuru, Haiti ilikumbwa na machafuko ya ndani.
Tarehe 18 Jumadithani miaka 164 iliyopita aliaga dunia faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Murtadha Ansari katika mji mtakatifu wa Najaf huko Iraq. Alizaliwa mwaka 1214 Hijria Shamsia katika mji wa Dezful nchini Iran na baada ya kupata elimu ya msingi kwa baba yake alielekea katika miji mitakatifu ya Karbala na Najaf huko Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Miaka kadhaa baadaye Sheikh Ansari alitambuliwa kuwa miongoni mwa wanazuoni na walimu mashuhuri wa zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Rasail na Makasib ambavyo vingali vinatumiwa hadi sasa kufundishia katika vyuo vikuu vya kidini.
Siku kama ya leo miaka 130 iliyopita Heinrich Rudolf Hertz mwanafizikia na mwanahisabati wa Ujerumani aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 37. Alizaliwa mjini Hamburg Ujerumani mwaka 1857. Alikuwa na mapenzi makubwa na fizikia na umakenika tangu akiwa kijana mdogo. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana akajiendeleza kimasomo katika uwanja huo.
Miaka 68 iliyopita katika siku kama ya leo nchi ya Sudan ilipata uhuru kutoka kwa Misri na Uingereza. Mwaka 1899 Uingereza na Misri zilitiliana saini mkataba wa kuitawala kwa pamoja Sudan. Katikati mwa karne ya 20 lilianza vuguvugu la kutaka kujipatia uhuru nchini Sudan na mwaka 1956 Misri na Uingereza zikalazimika kuutambua uhuru wa nchi hiyo. Sudan inapakana na nchi za Sudan Kusini, Misri, Libya, Chad, Kenya, Uganda, Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Tarehe Mosi Januari mwaka 1959 miaka 65 iliyopita mapinduzi ya Cuba yalipata ushindi na dikteta Fulgencio Batista akaikimbia nchi hiyo. Ushindi wa mapinduzi hayo yaliyoongozwa na Fidel Castro uliiweka Marekani katika mazingira magumu baada ya kushindwa vibaraka wake nchini Cuba.
Miaka 64 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Kiafrika ya Cameroon ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Kwa miaka mingi nchi hiyo ilikuwa chini ya ukoloni wa nchi za Ulaya ikiwemo Ujerumani ambayo iliikalia kwa mabavu Cameroon kuanzia mwaka 1884. Baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia Ufaransa na Uingereza ziligawana baina yao ardhi ya Cameroon. Hata hivyo haukupita muda kabla ya kuanza mapambano ya kupigania uhuru nchini humo. Hatimaye mapambano ya kupigania uhuru nchini Cameroon yalizaa matunda katika siku kama ya leo baada ya nchi hiyo iliyoko magharibi mwa Afrika kujipatia uhuru.
Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita nchi ya Brunei ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Nchi hiyo ndogo na yenye wakazi wachache kijiografia iko kusini mashariki mwa Asia. Tangu kale mfumo wa utawala nchini Brunei ulikuwa wa Kifalme ambao ulikuwa ukisimamiwa na Uingereza. Brunei inahesabiwa kuwa miongoni mwa nchi tajiri duniani kutokana na kuwa na akiba kubwa ya mafuta na gesi.
Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, inayosadifiana na tarehe Mosi Januari 1993, yalianza kutekelezwa makubaliano ya Maastricht, eneo lililoko kusini mwa Uholanzi yaliyokuwa na lengo la kuondoa mipaka ya kiuchumi kati ya nchi 12 za Ulaya. Mkataba wa muungano wa Ulaya ulitiwa saini tarehe 10 Disemba mwaka 1991 na viongozi wa nchi 12 wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya katika mji mashuhuri wa Maastricht. Baadaye Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya ilibadilishwa na kuwa Umoja wa Ulaya. Utekelezwaji wa makubaliano ya Maastricht ulikuwa hatua kubwa katika mchakato wa kuungana zaidi wanachama wa Umoja wa Ulaya japo kuwa umoja huo ulikabiliwa na matatizo mengi katika miaka iliyofuatia.