Jul 08, 2016 06:09 UTC
  • Ijumaa, 08 Julai 2016

Miaka 22 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, Kim Il Sung kiongozi wa zamani wa Korea ya kaskazini na Katibu Mkuu wa chama cha Kikomonisti cha nchi hiyo alifariki dunia. Kim Il Sung alizaliwa mwaka 1912. Mwaka 1945, Sung alirejea na jeshi la nchi hiyo upande wa kaskazini mwa nchi akiwa kama kamanda.

Kim Il Sung alichukua haraka uongozi wa Korea na mwaka 1948 na alikuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo wakati wa kuasisiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Korea. Aliongoza majeshi ya nchi hiyo katika vita vilivyojiri nchini humo na mwaka 1972 akawa Rais wa Korea ya Kaskazini.

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita njama ya mapinduzi ya Nojeh iliyokuwa ikisimamiwa na Marekani nchini Iran iligunduliwa na kuzimwa. Njama hiyo ya mapinduzi iliratibiwa na Shirika la ujasusi la Marekani (CIA) likishirikiana na baadhi ya vibaraka wa jeshi la anga la utawala wa Shah kwa shabaha ya kumuua Imam Khomeini, kuangamiza utawala wa Kiislamu hapa nchini na kumrejesha madarakani  Shapur Bakhitiyar. Waratibu wa njama hiyo ya mapinduzi walikusudia kufanya mashambulizi dhidi ya makazi ya Imam Khomeini mjini Tehran na kumuua na kisha kushambulia kituo cha kuongozea ndege cha uwanja wa Mehrabad. Hata hivyo njama hiyo iligunduliwa na kusambaratishwa na waratibu wa njama hiyo walitiwa mbaroni na kuhukumiwa.

Na miaka 60 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia mtaalamu, mwanafikra na mwandishi wa Kitaliano Giovanni Papini. Alizaliwa mwaka 1881 katika mji wa Florence nchini Italia. Giovanni alipitia kipindi kigumu cha utoto na ujana wake. Hata hivyo hamu yake kubwa ya masomo ilimpelekea kwenda katika maktaba za kijamii na kuzidisha elimu na taratibu alidhihirisha uwezo wake mkubwa katika taaluma ya fasihi. Msomi huyu ameandika vitabu vingi kama "A man--finished," "The Failure," na “Life of Christ,"

 

Tags