Feb 13, 2024 04:47 UTC
  • Tuujue Uislamu (5)

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu.

 

Katika sehemu ya 5 ya mfululizo huu juma hili, tutaendelea kueleza na kubainisha sifa maalumu za dini ya mwisho ya Mwenyezi Mungu yaani Uislamu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Kwa kufanya mlinganisho rahisi na mwepesi kati ya mahitaji mbalimbali ya mwanadamu, tunagundua kwamba mahitaji yake ya kimsingi hayapotei kamwe, lakini kulingana na mazingira na zama kuna wakati mahitaji haya hubadilika. Ustadh Shahidi Mutahhari, mwanafikra mahiri wa Kiislamu anasema kuhusiana na mahudhui ya mahitaji ya mwanadamu kulingana na zama na mazingira kwamba:

Mahitaji ya wakati yanamaanisha mahitaji kulingana na mazingira, jamii na maisha ya mwanadamu, kwa sababu mwanadamu huyu ana nguvu ya akili, ubunifu na busara na ana hamu ya kuishi maisha bora, anafikiria na kufikiria kila wakati na sababu na zana kukidhi mahitaji yake ya kiuchumi, kijamii na kiroho. Kujitokeza na kupatikana suhula na zana kamili na bora, hilo hupelekea vitu vipya kuchukua nafasi ya zana na suhula za zamani na hivyo kumfanya mwanadamu kuwa tegemezi kwa vitu na suhula hizo mpya.

Utegemezi wa mwanadamu kwenye msururu wa mahitaji ya kimwili na kiroho na matukio ya daima na sababu, kuondoa na kukidhi mahitaji haya, lenyewe hili humfanya mwanadamu huyu kuwa na msusuru wa mahitaji mengine mapya. Hii inasababisha mahitaji ya mazingira, jamii na maisha kubadilika katika kila zama na wakati, na mwanadamu analazimika kuwa katika hali ambayo ataendana na mahitaji mapya.”

Ukweli wa mambo ni kuwa, Mfumo wa kutunga sheria za Kiislamu una uwezo wa kuweka sheria mpya kulingana na mahitaji ya siku hizi, kwa mujibu wa hali mbalimbali za kimada na kimaeneo na mageuzi ya maisha ya mwanadamu.

Mfumo wa kutunga sheria za Kiislamu umetoa sheria zisizobadilika kwa mahitaji ya awali, ya kudumu na ya msingi ya mwanadamu na umeweka Ahkam Thanawi yaani sheria ambazo zinabadilika kulingana na mazingira na mahitaji yake.

Allama Tabatabai mfasiri mkubwa wa Qur'an anasema kuhusiana na hili:  Uislamu unajibu na kukidhi mahitaji yanayobadilika ya watu katika kila zama, wakati na mahali, bila ya kubadilisha au kubatilisha kanuni zilizowekwa za Uislamu ambazo ni thabiti kama ambavyo unakidhi pia mahitaji ya jamii ya wanadamu.

 

Kanuni zozote mpya zenye manufaa kwa maendeleo ya maisha ya kijamii na kwa manufaa ya Uislamu na Waislamu zinahusiana na mamlaka ya mtawala yaani (Mtawala wa Sharia) na hakuna katazo katika utekelezaji wake. Kipengele hiki kinaruhusu Uislamu kujibu mahitaji ya mwanadamu na jamii pamoja na mahitaji ya wakati na mabadiliko katika maisha. Kwa maneno mengine ni kuwa, Ahkam Thanawi yaani hukumu na sheria ziinazobadilika kulingana na mazingira au sheria ambazo hutekelezwa kutokana na kujitokeza mazingira maalumu na ya dharura kama vile kuruhusiwa Mwislamu kula mzoga au nyama ya nguruwe katika hali ya dharura ya kukabiliwa na hatari ya kufa kutokana na njaa ilhali katika hali ya kawaida ni haramu. Uislamu ukiwa na lengo la kuweka sheria hizi (Ahkam Thanawi), unatumia njia inayoitwa ijtihad. Ijtihad maana yake ni juhudi za kiakili na kielimu kwa ajili ya kunyambua na kupata sheria za kidini. Kila tatizo jipya linalowakabili wanadamu, Uislamu utalijibu kwa kutumia wenzo wa ijtihad, ambao uko mikononi mwa wataalamu na wanazuoni wa kidini waliobobea katiika elimu na ambao wamefikia daraja hii ya kielimu. Uislamu umetoa ruhusa kwa wanavyuoni na mafaqihi wa kidini kutunga sheria kwa kuzingatia kanuni na misingi thabiti na ya awali na kuzingatia mahitaji ya zama. Katika Uislamu, njia ya ijtihad na juhudi za kielimu kwa ajili ya kuelewa sheria za dini iko wazi kupitia akili na hoja. Huu ni uthibitisho mwingine wa umuhimu wa kutafakari na kutumia akili katika dini hii adhimu na inaashiria kwamba katika Uislamu vyanzo vya kidini havikomei kwenye Quran na Sunna pekee, bali akili pia ni miongoni mwa vyanzo vya kujua kanuni na sheria za dini ingawa hili nalo linapaswa kufanyika katika fremu ya mafundisho ya Qur'an na Sunna. Ili kuelewa vyema kiwango cha uwiano wa Uislamu na matakwa ya wakati na mahali, inafaa kusoma na kuchunguza zaidi vipengele vya dini, ambavyo ni: Imani, maadili na hukumu. Misingi ya kiitikadi au kiimani ni mambo thabiti na hayabadiliki si kutokana na zama wala mahali.

 

Kubadilika kwa jambo la imani kunamaanisha kubatilisha imani iliyotangulia, kwa hivyo mabadiliko hayo hayawezekani kuhusiana na misingi ya wazi ya kidini. Kwa mfano, imani juu ya Tawhidi yaani kumpwekesha Mwenyezi Mungu au Utume wa Mtume Muhammad (saw) ni miongoni mwa misingi thabiti ya dini ya Uislamu ambayo haiwezi kubadilishwa na mahali au zama. Isipokuwa kitu ambacho kinaweza kubadilika kuhusiana na itikadi hizi ni kutolewa hoja zaidi na makini kwa ajili ya kudiriki na kufahamu vyema zaidi misingii hii. Mabadiliko kama haya kimsingi ni mabadiliko katika ufahamu na maarifa ya kidini na sio Usul al-Din yaani Misingi ya Dini. Kuhusiana na thamani za kimaadili pia tunaweza kusema kuwa, misingi na kanuni jumla za kimaadili si yenye kubadilika. Uadilifu, uchajimungu, kuchukia dhulma, ukweli, kujitolea, kutenda wema, kusaidia na kadhalika daima ni mambo mazuri na yanayofaa na mkaba wake kuna mambo kama dhulma, ubaguzi, kukanyaga haki za wengine, kusema uwongo, kujiona na kadhalika, daima ni mambo mabaya na yasiyofaa. Hata katika jamii ambazo kimsinghi hazina dini hakuna mtu anayependa na kufurahia dhulma au kuona kuporwa haki za wengine kuwa ni jambo jema na linalopendeza.

Katika Uislamu hukumu au sheria zinagawanya katika makundi mawili sheria thabiti na zisizobadilika na sheria zinazobadilika. Katika sheria thabiti za dini katu hakuna mabadiliko kama vile wajibu wa Saumu, Sala, Hija na kadhalika. Lakini katika sheria zinazobadilika kama vile namna ya kuhami na kutetea ardhi za Kiislamu, yumkini katika hili kukafanyika mabadiliko kulingana na mazingira ya zama na mahali. Mwenye jukumu la kuainiisha sheria hizi zinazobadilika ni Mujtahidi na mtu aliyebobea katika misingi ya Uislamu. Ayatullah Makarem Shirazi, mmoja wa wanazuoni na wanafikra wa Kiirani, anaandika kuhusu sheria zisizobadilika na zisizobadilika katika Uislamu zinazojibu mahitaji mbalimbali ya mwanadamu: Mwanadamu wa zama za sasa, kwa mujibu wa maumbile yake, silika yake, na mielekeo ya asili isiyobadilika, ni sawa na mtu wa karne ya 10. Ubinadamu wake na sifa zake hazijabadilika. Kwa maana hii, vikwazo na marufuku yao inapaswa pia kuwa ya kudumu. baya.

 

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa juma hili umemalizika hivyo sina budi kukomea hapa kwa leo nikitaraji kuwa mtakuwa pamoja namI wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu. Kwaherini.