Jumatatu, Februari 19, 2024
Leo ni Jumatatu tarehe 9 Sha'ban 1445 Hijria sawa na tarehe 19 Februari mwaka 2024.
Siku kama ya leo miaka 964 iliyopita sawa na tarehe 9 Sha'ban mwaka 481 Hijria, aliaga dunia Ibn Barraj mmoja wa mafaqihi na maulamaa mashuhuri wa Misri. Ibn Barraj alifahamika sana kwa jina la Trablosi kutokana na kuwa, kwa muda fulani alikuwa na cheo cha kadhi katika mji wa Trablos yaani Tripoli huko kaskazini mwa Lebanon ya sasa. Msomi huyo wa Kiislamu alifunzwa na maulamaa kama vile Sayyid Murtadha na Sheikh Tusi. Ibn Barraj ni msomi mtajika wa Kiislamu ambaye fikra na mitazamo yake ilikuwa ikiheshimiwa na mafaqihi wakubwa wa zama hizo.
Katika siku kama ya leo miaka 868 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria aliaga dunia Abul Barakaat Abdul Rahman bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Anbari fakihi na mtaalamu mashuhuri wa lugha wa mjini Baghdad. Alihitimu masomo yake katika Chuo cha Nidhamiyyah mjini Baghdad na kutokana na kupata alama za juu mno katika masomo alianza kufundisha katika chuo hicho. Ibn Anbari hakuwa nyuma pia katika uwanja wa uandishi wa vitabu na amevirithisha vizazi vilivyokuja baada yake vitabu vyenye thamani kubwa.
Katika siku kama ya leo miaka 551 iliyopita alizaliwa mnajimu na mwanahesabati mashuhuri wa Poland, Nicolaus Copernicus. Awali alijifunza elimu ya nujumu na baadaye tiba, na baada ya kukamilisha masomo alianza kufundisha hesabati huko Roma. Hata hivyo Copernicus aliendelea kudurusu na kufanya utafiti wa elimu ya nujumu na mwaka 1503 alivumbua nadharia ya harakati ya dunia kuzunguka jua na vilevile dunia kujizunguka yenyewe katika kila baada ya masaa 24. Nicolaus Copernicus alifariki dunia tarehe 24 Mei 1543 siku chache tu baada ya kuchapisha kitabu cha On the Revolutions of the Celestial Spheres kinachofafanua nadharia zake. *
Miaka 73 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 19 Februari mwaka 1951 alifariki dunia mwandishi na mkosoaji mashuhuri wa Ufaransa Andre Gide akiwa na umri wa miaka 82. Alizaliwa mwaka 1869 Miladia mjini Paris lakini alitumia umri wake mwingi Afrika kaskazini na hasa nchini Algeria. Visa vingi alivyoandika viliathiriwa na maisha pamoja na utamaduni wa watu bara hilo. Miongozi mwa visa vya kuvutia vilivyoandikwa na mwandishi huyo ni pamoja na "Wimbo wa kijijini" na "Meza ya Ardhi." Mwaka 1947 Gide alitunukiwa zawadi ya Nobel.
Miaka 72 iliyopita katika siku kama ya leo mwaka 1952 alifariki dunia mwandishi wa Norway, Knut Hamsun. Alizaliwa mwaka 1859 katika familia masikini kaskazini mwa nchi hiyo, na alipotimiza miaka 24 aliingia katika uwanja wa uandishi. Hamsun alisafiri mara mbili kwenda Marekani na akaandika makosa aliyoyaona nchini humo ndani ya kitabu alichokipa anwani ya "Maisha ya Kimaanawi katika Zama Mpya Nchini Marekani" pia aliandika kitabu kilichopewa jina la "Njaa" ambacho kilibeba tamaduni mbali mbali za dunia. Uandishi wake wa kitabu cha "Matunda ya Ardhini" ulikuwa na nafasi muhimu katika kutunukiwa zawazi ya Nobel mwaka 1920.
Tarehe 19 Februari miaka 27 iliyopita alifariki dunia Deng Xiaoping, kiongozi wa zamani wa China na mhandisi wa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa ya nchi hiyo. Katika kipindi cha uongozi wa Xiaoping China ilifanya mageuzi makubwa katika nyanja mbalimbali na alifanya marekebisho makubwa katika uchumi wa kisoshalisti wa wakati huo wa China na kuuelekeza kwenye uchumi wa soko. Wakati huo China ilifanikiwa kuingia katika nyanja mbalimbali za kimataifa na kutatua migogoro iliyokuwepo katika uhusiano wake na nchi kadhaa. Deng Xiaoping alijiuzulu mwaka 1990 kutokana na maradhi na umri wake mkubwa na hadi anafariki dunia alikuwa akihesabiwa kuwa shakhsia mkubwa zaidi wa China.
Miaka 14 iliopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 30 Bahman 1388 Hijiria Shamsia, manowari ya kwanza ya kivita ya Iran inayojulikana kwa jina la Jamaran ilianza kufanya kazi. Jamaran ni manowari ya kijeshi yenye uwezo wa kubeba aina kadhaa za makombora ya kuhujumu meli na kutungua makombora na ndege za adui. Pia ina rada za kisasa na uwezo wa kushiriki katika vita vya kielektroniki. Meli hiyo inayoenda kwa kasi kubwa pia ina eneo la kutua helikopta. Baadhi ya teknolojia iliyotumia kutengeneza manuwari hiyo inamilikiwa na nchi kadhaa tu dunia na wataalamu wa Jamhuri ya Kiislamu wamefanikia kuvunja mzingiro huo na kuiwezesha Iran kuwa miongoni mwa nchi zenye utaalamu wa kubuni na kuzalisha teknolojia hiyo. *