Jumamosi 09 Julai 2016
Leo ni Jumamosi tarehe 9 Julai mwaka 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 5 iliyopita, Sudan Kusini ilitangazwa rasmi kuwa nchi huru inayojitawala. Nchi mpya ya Sudan Kusini iliundwa baada ya kujitenga na Sudan. Miezi michache nyuma mwaka huo huo raia wa Sudan Kusini walishiriki kwenye kura ya maoni kwa ajili ya kuainisha mustakabali wa eneo la kusini mwa Sudan na lile la kaskazini, kura ambayo hatimaye ilipelekea eneo la kusini mwa Sudan kujitenga na lile la kaskazini na kuundwa nchi inayojitawala ya Sudan Kusini mji mkuu wake ukiwa Juba. ***
Miaka 14 iliyopita mwafaka na tarehe 9 Julai mwaka 2002 Umoja wa Afrika (AU) ulichukua nafasi ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) baada ya kuidhinishwa na wakuu wa nchi za Kiafrika. OAU iliundwa mwaka 1963 ili kusaidia juhudi za kupigania uhuru wa nchi za Kiafrika na kutatua hitilafu miongoni mwa nchi hizo. Hata hivyo siku baada ya siku kulijitokeza hisia kwamba katika mazingira ya ulimwengu wa leo kuna udharura wa kuundwa taasisi yenye nguvu za utendaji na yenye malengo mapya zaidi. Kwa msingi huo katika siku kama ya leo mwaka 2002 wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) waliunda Umoja wa Afrika (AU) katika mji wa Durban, Afrika Kusini. Taasisi kama vile bunge, kamisheni ya utendaji, benki kuu, mfuko wa fedha na mahakama zimezingatiwa katika umoja huo kwa ajili ya kuratibu mawasiliano na kusaidia ustawi wa kiuchumi wa nchi za Kiafrika. ***
Katika siku kama ya leo miaka 68 iliyopita na baada ya usitishaji vita wa mwezi mmoja, vita kati ya Waarabu na utawala haramu wa Israel vilianza tena. Vita hivyo vilianza baada ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu mwezi Mei 1948. Vita hivyo vilisimama mwezi Juni mwaka huo kufuatia ombi la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Vita kati ya utawala wa Kizayuni na Waarabu vilipelekea kukaliwa kwa mabavu asilimia 78 ya ardhi ya Palestina na Wapalestina 750,000 kuwa wakimbizi.***
Na miaka 200 iliyopita katika siku kama ya leo, ardhi ya Argentina ilijipatia uhuru. Nchi hiyo ilikuwa koloni la Muhispania kuanzia mwanzoni mwa karne ya 16 Miladia. Mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia na baada ya kudhoofika Uhispania kufuatia vita mtawalia na Uingereza, Waingereza waliukalia kwa mabavu mji mkuu wa Argentina Buenos Aires. Hata hivyo wananchi wa Argentina walisimama imara kukabiliana na jeshi la mkoloni Muingereza na kufanikiwa kulirejesha nyuma kutoka katika ardhi ya nchi hiyo na hivyo kujitangazia uhuru katika siku kama ya leo. ***