Jul 10, 2016 06:29 UTC

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya Makala hii inayozungumzia hatima ya mwanadamu na safari yake ya kurejea kwa Mola Muumba. Katika Makala ya wiki iliyopita tulisema kuwa, dunia ni shamba la Akhera na kwamba matunda ya dunia yanachumwa huko katika ulimwengu mwingine.

Kwa maneno mengine ni kuwa, dunia si lengo bali na wenzo na chombo tu kama anavyosema Imam Ali bin Abi Twalib kwamba: Dunia ni njia ya kupita na si mahala pa kukaa". (Mahjul Balagha, Hekima:133) Kwa msingi huo ni lazima tuitumie dunia kama wenzo na wasila wa kukusanya mtaji wa amali njema na kupata maarifa aali na kuvitumia huko katika ulimwengu wa Akhera. Leo tutazungumzia dunia na umuhimu wake kwa ajili ya kufikia ukamilifu wa Akhera.      <<<<<      >>>

Inapozungumziwa dunia, watu huwa na ufahamu tofauti kuhusu kinachozungumziwa na maana halisi ya dunia. Katika Qur'ani tukufu pia baadhi ya aya za kitabu hicho zimekemea na kutahadharisha watu kuhusu dunia na nyingine zimeisema na kuizungumzia vizuri. Baadhi ya aya za kitabu hicho zinaitaja dunia kuwa ni mchezo, bidhaa isiyo na thamani, mali isiyo ya kudumu na kadhalika. Hata hivyo kuna aya nyingine za kitabu hicho ambazo zinaitaja dunia na vilivyomo kwa sifa nzuri kama kheri, rehma na wema. Miongoni mwa sifa kubwa na kuu za dunia hii ni mali na utajiri ambao Qur'ani tukufu inautaja kuwa ni nguzo ya kusimama na kuimarika kwa jamii na inawatahadharisha wanadamu wasije wakatoa mali na utajiri huo kwa watu masafihi na fidhuli. (al Nisaa:5) Hapa linajitokeza swali kwamba, je, kuna hitilafu na mgongano kati ya aya za Qur'ani tukufu ambayo ni muujiza hususan katika upande wa lafdhi na maana ya aya za kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu? Inawezekana kwa kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu kikaitaja dunia na vielelezo vyake kuwa ni mchezo, bidhaa isiyo na thamani na kadhalika na katika sehemu nyingine kikaitaja kuwa ni kheri, baraka na rehma?

Tunapofanya uchunguzi wa kina katika aya za Qur'ani tunakutana na kundi jingine la tatu la aya za kitabu hicho linaloweka wazi na kufafanua aya za makundi mawili yaliyotangulia. Kwa hakika aya hizo za kundi la tatu zinatueleza kwa muhtasari kuwa, dunia kama dunia na kwa dhati yake si kitu kisicho na thamani, bali kinachokemewa na ambacho wanadamu wanatahadharishwa ni kuikumbatia na kuiganda dunia.

Neno "dunia" lina mana mbalimbali lakini maana mbili kati yazo ndizo zinazotumika kwa wingi zaidi: Dunia kwa maana ya "karibu zaidi" na dunia kwa maana ya "duni, ya chini na ya daraja la chini'. Dunia kwa maana ya karibu zaidi ni kutokana na kwamba maisha ya dunia yako karibu zaidi kwetu sisi kuliko maisha ya Akhera, na dunia kwa maana ya chini na duni ni kwamba, maisha ya dunia ni ya daraja ya chini yakilinganishwa na yale ya Akhera. Hata hivyo hii haina maana kwamba, madamu dunia iko daraja ya chini ikilinganishwa na Akhera basi ni mbaya ya isiyo na thamani. Mwenyezi Mungu SW anasema katika aya ya 7 ya Suratu Sajda kwamba: (Mwenyezi Mungu) Ambaye ametengeneza vizuri umbo la kila kitu… Kwa mujibu wa aya hii, dunia kama moja ya viumbe vikubwa vya Mwenyezi Mungu SW ni haki na kiumbe kizuri. Vilevile kuna hadithi nyingi za Mtume (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu zinazoitaja dunia kuwa ni shamba la Akhera, eneo la kuteremkia wahyi na ufunuo wa Allah na nyumba ya biashara ya mawalii wa Mwenyezi Mungu. Kwa mujibu wa hadithi hizo, kama dunia haitakuwepo basi mwanadamu hatapata masurufu ya kumfikisha Akhera. Hivyo dunia ni neema kubwa kwa waumini kwa sababu ndiyo msingi na mtaji wa saada na ufanisi wa milele katika ulimwengu mwingine wa kudumu.

Imepokewa kwamba siku moja Imam Ali bin Abi Twalib alimsikia mtu mmoja akiitusi na kuisema vibaya dunia. Imam alimkemea na kusema: Dunia ni nyumba ya ukweli kwa anayeamiliana nayo kwa ukweli, na makazi ya afya kwa anayeitambua, nyumba ya utajiri kwa anayechukua masurufu humo, nyumba ya mawaidha kwa mwenye kuwaidhika. Ni masjidi ya vipenzi vya Mwenyezi Mungu, mswala wa Malaika Wake, mahala pa kuteremka wahyi wa Mwenyezi Mungu na nyumba ya biashara ya mawalii wa Allah. Walichuma rehma humo na wakapata faida ya pepo". (Nahjul Balagha, hekima: 126)         <<<<<     >>>>>

Imam Sajjad, Ali bin Hussein bin Ali bi Abi Twalib (as) amenukuu kwamba Nabii Issa Masih (as) alisema kuwaambia Hawariyyun waliokuwa wanafunzi wake wa karibu kwamba: "Dunia ni daraja, hivyo basi itumieni kama kivuko na wala musiijenge".  Kwa msingi huo dunia kama kivuko, ina umuhimu kwa mwanadamu anayevuka kuelekea upande mwingine. Hata hivyo ni makosa kwa mtu kutaka kujenga nyumba ya kudumu juu ya daraja na mahala watu wanapotumia kuvuka. Watu wa aina hii ni wale walioifanya dunia kuwa lengo lao kuu na asili. Hawa, dunia imeteka na kutawala fikra na nyoyo zao kiasi kwamba wako tayari kufanya lolote kwa ajili ya kupata muradi wao. Mkabala wake wapo watu ambao hawayaoni maisha ya dunia kuwa ni mwisho wa kila kitu bali hutumia dunia kama merikebu na chombo cha kuwafikisha katika lengo na muradi wao katika ulimwengu mwingine. Watu hawa hupanga matendo, mienendo na amali zao zote kwa mujibu wa lengo lao huko Akhera.

Katika aya za 200 hadi 202 za Suratul Baqara, Qur'ani tukufu inachora hatima ya wapenzi wa dunia na wale wanaoitafuta Akhera kwa kusema: Na wapo baadhi ya watu wanaosema: Mola wetu Mlezi, tupe duniani! Naye katika Akhera hana sehemu yoyote. Na katika watu wapo wanaosema: Mola wetu Mlezi, tupe mema duniani, na mema huko Akhera, na utulinde na adhabu ya Moto! Hao ndio watakaopata sehemu yao kwa sababu ya yale waliyoyachuma. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu".

Imenukuliwa kwamba, mmoja wa wanafunzi wa mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw) Imam J'afar Swadiq (as) aliyejulikana kwa jina la Abu Yaafur alimwambia mtukufu huyo kwamba: Mimi Ninaipenda dunia. Imam alisema: Unaipenda dunia ili uifanyie kitu gani? Nilisema: Ili niowe, niende Hija, nipate matumizi ya kukimu familia yangu, niwashughulikie ndugu zangu na nitoe sadaka. Imam Swadiq (as) alisema: Huko si kuipenda dunia bali hiyo ndiyo Akhera." (Biharul Anwar:J-37)

Wapenzi wasikilizaji dunia ni utangulizi wa safari ya kuelekea Akhera isiyo na mwisho na ya kudumu. Hata hivyo inatupasa kuithamini dunia kwa sababu ni kwa kuitumia dunia na maisha yake mafupi ndiyo tunaweza kupata maisha na saada ya milele. Makosa makubwa ya mwanadamu ni kuikumbatia na kuiashiki dunia, suala ambalo huwa kizuiazi cha kukusanya masurufu kwa ajili ya safari ya Akhera.

Swahaba mmoja alikwenda kwa Mtume Muhammad (saw) na kumkuta akiwa ameketi juu ya mkeka ambao kindo zake zilikuwa zimekwaruza mwili mtoharifu wa mtukufu huyo. Sahaba huyo alisema: Yaa Rasullah! Lau ungekusanya mkeka huu na badala yake ukakalia zulia, miguu yako isingeumia kiasi hiki. Mtume wa Mwenyezi Mungu alimwambia: Mimi na dunia wapi na wapi! Mfano wangu na dunia ni mithili ya mpanda farasi anayefanya harakati mchana kutwa wakati wa jua kali akiwa safarini, kisha anaona mti na kuketi chini yake kwa muda. Baada ya kupumzika kidogo na kuondokewa na uchovu, anaondoka mahala hapo na kuendelea na safari." (Biharul Anwar:J-70)

Imam Ali bin Abi Twalib (asa) pia anasema: "Watu wa dunia ni mithili ya msafara unaopelekwa huku watu wake wakiwa amelala".

Haya yote wapenzi wasikilizaji yanatutanabahisha kwamba, maisha mafupi ya dunia hayapaswi kupita hivi hivi bali tunapaswa kuyatumia vyema bila ya kuikumbatia dunia na kuitumia kwa ajili ya kufika kwenye ulimwengu wa milele na maisha ya kudumu huko Akhera.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. 

Tags