Mar 22, 2024 02:53 UTC
  • Ijumaa, tarehe 22 Machi, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 11 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1445 Hijria, mwafaka na tarehe 22 Machi 2024.

Siku kama ya leo miaka 592 iliyopita, alifariki dunia mjini Cairo Ibrahim Karaki, mwanahistoria, mtaalamu wa fasihi na Hadithi wa Kiislamu.

Baada ya kusoma Qur'ani na masomo ya awali ya kidini, Ibrahim Karaki alianza kufanya safari katika maeneo mbalimbali katika vituo vya elimu ya kidini kwa lengo la kukamilisha masomo yake ya juu kama vile fiqihi na fasihi ya lugha ambapo alifanikiwa kufikia daraja ya juu katika uwanja huo.

Kitabu cha I'rabul-Mafsal ni miongoni mwa athari zilizoachwa na msomi huyo.

Siku kama ya leo miaka 143 iliyopita lilianzishwa Muungano wa Soka wa Kimataifa kwa shabaha ya kusimamia mashindano ya mpira wa miguu kote duniani.

Kabla ya kuundwa muungano huo, mashindano ya soka yalikuwa yakifanyika katika nchi mbalimbali kwa muundo usiokuwa rasmi. Muungano huo ulibadilisha muundo wake na kujulikana baadaye kwa jina la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na liliandaa pambano rasmi la kwanza la kimataifa mwaka 1901, kati ya timu za Uingereza na Ujerumani.   

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita yaani tarehe 3 Farvardin 1301 Hijria Shamsia, Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha Qum, Iran kilianzishwa na Ayatullah Sayyid Abdul Karim Hairi Yazdi.

Mji wa Qum ulikuwa kitovu cha kueneza elimu, maarifa ya dini na kulea maulama mashuhuri tangu mwanzoni mwa karne za awali za kudhihiri dini Tukufu ya Kiislamu.

Kuweko Haram ya Bibi Fatma Maasuma (as) dada wa Imam Ridha (as) katika mji wa Qum, kumezidisha umuhimu wa mji huo. Baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Hawza ya Qum iligeuka na kuwa kituo muhimu cha mafunzo na uenezaji wa elimu na maarifa ya Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Abdul Karim Hairi Yazdi

Katika siku kama hii ya leo miaka 79 iliyopita, yaani tarehe 22 Machi 1945, iliundwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kutokana na mapendekezo ya Farouk, aliyekuwa mfalme wa wakati huo wa Misri. Hati ya kuanzisha jumuiya hiyo ilitiwa saini na serikali za Syria, Iraq, Saudi Arabia, Misri na Yemen mjini Cairo.

Lengo la kuanzishwa jumuiya hiyo lilikuwa ni kulinda ardhi na kujitawala kwa nchi wanachama na kuwepo ushirikiano wa karibu wa kisiasa kiuchumi na kiutamaduni kati ya nchi hizo. 

Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita aliuawa shahidi Sheikh Ahmad Yassin mwanachuoni na mwasisi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) pamoja na watu wengine 10.

Sheikh Ahmad Yassin aliuawa shahidi baada ya kumaliza swala ya Alfajiri katika msikiti mmoja ulioko eneo la Ukanda wa Gaza, wakati aliposhambuliwa na helikopta za utawala wa Kizayuni wa Israel. Sheikh Ahmad Yasin aliasisi harakati ya Hamas mwaka 1987 akishirikiana na wanamapambano wengine kadhaa wa Kipalestina na miaka miwili baadaye alifungwa jela na utawala ghasibu wa Israel.

Mauaji ya mpigania uhuru huyo ambaye alikuwa kiwete na kipofu wakati wa kuuawa kwake, yalidhihirisha tena ugaidi wa kiserikali wa utawala haramu wa Israel. 

 

Tags