Mar 26, 2024 02:08 UTC
  • Jumanne, Machi 26, 2024

Leo ni Jumanne tarehe 15 Ramadhani 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 26 Machi 2024 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1442 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Imam Hassan al-Mujtaba (as), mjukuu wa Mtume Muhammad (saw).

Imam Hassan (as) alikulia katika malezi na usimamizi wa Mtume, Bibi Fatmatu al Zahra, binti wa Mtume, na Imam Ali bin Abi Twalib (as).

Baada ya kuuawa shahidi baba yake, yaani Imam Ali hapo mwaka wa 40 Hijria, mtukufu huyo alifanya kazi kubwa ya kusimamia na kuwaongoza Waislamu. Mwanzoni, Waislamu wengi walimbai na kumpa mkono wa utiifu Imam Hassan, lakini utawala wa Bani Umayyah uliokuwa ukiongozwa na Muawiya mwana wa Abu Sufiyan ambao wakati huo ulikuwa na nguvu kubwa, ulianzisha uadui na chuki dhidi ya mjukuu huyo a Mtume.

Hatimaye Imam Hassan (as) alijiandaa kukabiliana na utawala dhalimu wa Bani Umayyah, lakini viongozi wengi wa jeshi lake walidanganyika na ahadi za uongo za Muawiya na kumuacha peke yake, hali iliyomlazimu mtukufu huyo kufanya suluhu na mtawala huyo wa Bani Umayyah kwa lengo la kuhifadhi dini tukufu ya Uislamu. 

Katika siku kama hii ya leo miaka 113 iliyopita alizaliwa mwandishi mashuhuri wa michezo ya kuigiza wa Marekani, Tennessee Williams.

Alivutiwa sana na fasihi na mvuto huo uliimarika zaidi wakati alipokuwa masomoni katika chuo kikuu na hatimaye alifanikiwa kuwa mwandishi mkubwa. Tennessee Williams alitumia umahiri wake kueleza fikra zake kwa lugha ya michezo ya kuigiza. Kazi zake nyingi zilieleza hali ya watu wa tabaka la chini na wanaosumbuliwa na ukata katika jamii ya Marekani.

Miongoni mwa kazi za mwandishi huyo mashuhuri ni Cat on a Hot Tin Roof, Sweet Bird of Youth na The Glass Menagerie.

Tennessee Williams

Miaka 72 iliyopita katika siku kama ya leo, yalianza mapambano ya Mau-Mau yakiongozwa na Mzee Jomo Kenyatta, mwasisi wa nchi huru ya Kenya, dhidi ya wakoloni wa Kiingereza.

Katika kipindi cha vita viwili vikubwa vya dunia, Kenya ilikumbwa na machafuko na vurugu nyingi. Hata hivyo baada ya Vita vya Pili vya Dunia, wananchi wa nchi hiyo waliamua kupambana kufa na kupona ili kuikomboa nchi yao kutoka mikononi mwa wakoloni wa Ulaya.

Wakoloni wa Kiingereza waliweka sheria kali katika maeneo tofauti ya Kenya hasa katika maeneo ya Wakikuyu lakini hilo halikuzuia kuasisiwa harakati ya Mau-Mau. Kaulimbiu kuu ya wapiganaji wa Mau-Mau ilikuwa kuweko usawa na uadilifu katika masuala ya kijamii na kisiasa baina ya wenyeji wa Kenya na Wazungu.

Hatimaye harakati hiyo ya Mau-Mau, kwa uongozi wa Mzee Jomo Kenyatta, ilifanikiwa kuikomboa Kenya kutoka mikononi mwa wakoloni wa Kiingereza mwanzoni mwa muongo wa 60.

Mzee Jomo Kenyatta

Tarehe 26 Machi mwaka 1971 katika siku kama hii ya leo, Pakistan Mashariki ambayo hivi sasa inajulikana kwa jina la Bangladesh iliamua kujitenga na Pakistan baada ya kuzuka mivutano mikubwa ya kisiasa na uasi nchini humo.

Pakistan Mashariki na ile ya Magharibi ilikuwa nchi moja, iliyoamua kujitenga na India mwaka 1947. Wabangladeshi waliokuwa wakiishi Pakistan Mashariki na kuunda jumla ya asilimia 98 ya watu wa eneo hilo, hawakuridhishwa na vitendo vya kibaguzi vilivyokuwa vikifanywa na serikali kuu huko Pakistan Magharibi na kwa msingi huo, awali walitaka kupewa mamlaka ya kujiendeshea mambo yao wenyewe. Baadaye walianzisha mapambano ya silaha na kufanikiwa kulifukuza jeshi la Pakistan Magharibi wakisaidiwa na jeshi la India. Pakistani Mashariki ilipewa jina la Bangladesh.

Bendera ya Bangladesh

Miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Ahmad Sekou Toure kiongozi mkubwa wa nchi ya Kiafrika ya Guinea.

Sekou Toure alizaliwa Januari 9 mwaka 1922 katika moja ya miji ya katikati mwa Guinea. Aliingia katika harakati za kisiasa akiwa katika rika la ujana na alikuwa akitaka uhuru wa  chi yake kutoka kwa wakoloni wa Kifaransa.

Hatimaye mwaka 1958 nchi hiyo ilipata uhuru na mwaka mmoja baadaye Touré akateuliwa kuwa rais na kusalia madarakani hadi mwaka 1984 alipofariki dunia.

Ahmad Sekou Toure

Siku kama hii ya leo miaka 36 iliyopita Katibu Mkuu wa wakati huo wa Umoja wa Mataifa alitoa taarifa akilaani kitendo cha utawala wa Iraq cha kutumia silaha za kemikali katika vita vyake dhidi ya Iran.

Baada ya kupita muda serikali ya Iraq ikitumia silaha za kemikali na kutochukuliwa hatua ya maana katika Baraza la Usalama ya kukabiliana na suala hilo, Katibu mkuu wa wakati huo wa Umoja wa Mataifa, Javier Pérez de Cuéllar alichukua hatua ya kutoa taarifa yake mwenyewe akiilaani Iraq kwa kutumia silaha za kemikali licha ya kimya cha Baraza la Usalama.

Javier Pérez de Cuéllar alisema katika taarifa yake iliyotolewa tarehe 28 Machi 1988 kwamba: "Kuna ushahidi mwingi unaothibitisha kwamba jeshi la Iraq linatumia silaha za kemikali ambazo zimesababisha madhara makubwa kwa raia wa Iran na Iraq." Katika sehemu nyingine ya taarifa hiyo katibu mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa alisema: utumiaji wa silaha za kemikali umapaswa kulaani. 

Javier Pérez de Cuéllar

 

Tags