Apr 11, 2024 02:20 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 11 Aprili, 2024

Leo ni Alkhamisi tarehe Pili Shawwal 1445 Hijria sawa na tarehe 11 Aprili 2024.

Siku kama ya leo miaka 861 iliyopita, alifariki dunia Ibn Taawidhi, malenga na mtaalamu wa fasihi wa Baghdad. Ibn Taawidhi alizaliwa mwaka 519 Hijiria. Malenga huyo wa Kiislamu alitumia wakati wake mwingi kutunga na kusoma mashairi. Vilevile aliandika kasida nzuri na ndefu katika kuwasifu Ahlu Bayti wa Mtume Muhammad (swa). Baadaye Ibn Taawidhi alipoteza uwezo wa kuona na kuwa kipofu, lakini bado aliendelea kutunga na kusoma mashairi hadi mwisho wa uhai wake.  *

Tarehe 11 Aprili miaka 164 iliyopita chombo cha kuzalisha baridi kilibuniwa na mwanakemia wa Kifaransa kwa jina la Ferdinand Carre.

Kifaa hicho kilikuwa kikizalisha baridi kwa kutumia gesi ya ammonia. Ubunifu huo wa Carre ulikuwa hatua muhimu katika kuhifadhi vyakula ili visiharibike hususan katika maeneo yenye joto. Uvumbuzi wa msomi huyo hatimaye ulipelekea kutengenezwa kwa majokofu na vifaa vingine vikubwa vya kuzalisha baridi kwa ajili ya shughuli mbalimbali.  ***

Miaka 39 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo aliaga dunia Enver Hoxha Rais wa zamani wa Albania.

Hoxha alikuwa kiongozi wa wapiganaji wa mrengo wa kushoto baada ya Italia kuivamia na kuikalia kwa mabavu Albania mwaka 1939. Enver Hoxha alichukua madaraka ya nchi mwaka 1944 kwa kusaidiwa na jeshi la Urusi ya zamani baada ya kushindwa Italia katika Vita vya Pili vya Dunia.

Rais huyo wa zamani wa Albania miaka miwili baadaye aliitangaza nchi hiyo kuwa ni Jamhuri ya Kikomonisti.

Enver Hoxha

Na siku kama hii ya leo miaka 32 iliyopita, Muhsin Saba mwalimu na mwandishi wa zama hizi wa Kiirani alifariki dunia.

Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi katika shule ya Darul Funun alielekea nchini Ufaransa. Alirejea nchini Iran baada ya kupata shahada ya uzamivu (PhD) na kuanza kufundisha.

Dakta Muhsin Saba aliasisi Kundi la Taifa la Utambuzi wa Vitabu. Aidha hakuwa nyuma pia katika kutunga na kuandika vitabu.

Muhsin Saba

 

Tags