May 03, 2024 02:40 UTC
  • Ijumaa, tarehe 3 Mei, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 24 Mfunguo Mosi Shawwal 1445 Hijria sawa na Mei 3 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 595 iliyopita, Jeanne d'Arc alianzisha harakati ya kihistoria ya kuzikomboa baadhi ya ardhi za Ufaransa zilizokuwa zikikaliwa kwa mabavu na Uingereza. Jeanne d'Arc alikuwa kamanda wa jeshi ambaye alipewa jukumu na Mfalme wa Ufaransa la kuongoza mapambano dhidi ya majeshi ya Uingereza yaliyolikalia kwa mabavu eneo la kaskazini mwa Ufaransa. Hatimaye Kamanda huyo alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kimaonyesho nchini Uingereza kwa tuhuma za kuritadi na kuacha dini na mwaka 1431, aliuawa kwa kuchomwa moto akiwa hai. 

Siku kama ya leo miaka 555 iliyopita alizaliwa Niccolò di Bernardo dei Machiavelli, mwanahistoria na mwanasiasa wa Italia katika mji wa Florence. Sambamba na shughuli zake za kisiasa, Machiavelli aliandika pia historia ya Florence. Katika mtazamo wa kisiasa, Machiavelli alikuwa akiamini kwamba yawezekana kutumia wenzo wowote ule kwa ajili ya kupata madaraka na kwa ajili ya kuyalinda, na kwamba hakuna udharura wowote wa kuheshimu misingi ya maadili katika masuala kama hayo. Miongoni mwa kazi za mwanahistoria na mwanasiasa huyo wa Italia ni "The Art of War" na "The Prince."   

Niccolò di Bernardo dei Machiavelli

Katika siku kama ya leo miaka 530 iliyopita, sawa na tarehe 3 Mei 1494 Miladia, Christopher Columbus, baharia wa Uhispania aligundua nchi ya Jamaica, huko Amerika ya Kati katika safari yake ya pili ya uvumbuzi ndani ya bara la Amerika. Licha ya tabia ya upendo na maridhiano ya wakazi asilia wa Jamaica na nchi nyingine zilizogunduliwa, lakini Christopher Columbus na watu wengine waliotumwa na Uhispania, waliwafanyia ukatili wenyeji hao wakazi. Kwa utaratibu huo Jamaica ambayo kutokana na nafasi yake muhimu ya kijografia na kwa kuwa na dhahabu nyingi zilizokuwa zikikodolewa macho na Uhispania, ilikoloniwa kuanzia mwaka 1509 Miladia hadi muda unaokaribia karne mbili. Baada ya Uhispiania nchi hiyo pia ilikoloniwa na Uingereza ambapo katika kipindi hicho akthari ya wakazi wake asilia walifukuzwa au kuuawa. Hatimaye nchi hiyo iliweza kujipatia uhuru wake mwaka 1962. 

Siku kama ya leo miaka 509 iliyopita yaani tarehe 3 Mei 1515 manowari za Ureno zilianza kushambulia kisiwa cha Hormuz cha Iran na hivyo kuanzisha wimbi la uingiliaji na ukoloni wa nchi za Magharibi katika eneo la Mashariki ya Kati. Kisiwa hicho kiko katika eneo la kiistratijia la lango la Hormuz lililoko katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman, kusini mwa Iran. Kutokana na kuwa Iran ilikuwa dhaifu katika upande wa jeshi la majini, wakoloni wa Kireno walivikalia kwa mabavu visiwa kadhaa vya Iran vilivyoko katika Ghuba ya Uajemi, ikiwemo Bahrain ambayo wakati huo ilikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Hatua kwa hatua, Iran iliimarisha jeshi lake la majini, na mwaka 1652, iliweza kuvikomboa visiwa vyote vilivyokuwa vikikaliwa kwa mabavu na Wareno.

ramani ya kisiwa cha Hormuz

Siku kama ya leo miaka 217 iliyopita ulitiwa saini Mkataba wa Finckenstein (Treaty of Finckenstein) kati ya Iran na Ufaransa wakati mfalme Napoleon wa Ufaransa alipokuwa katika vita na nchi nyingine za Ulaya. Kwa mujibu wa mkataba huo uliokuwa na vipengee 16, ilipangwa kuwa Iran ingepata silaha za aina mbalimbali kutoka Ufaransa kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi ya Warusi. Ufaransa pia iliahidi kutuma wataalamu wa mizinga na wahandisi wa masuala ya kijeshi nchini Iran kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa jeshi la nchi hiyo. Kwa upande wake, Iran iliahidi kukata uhusiano wake na Uingereza na kuisaidia Ufaransa katika kupeleka majeshi yake huko India.

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari. Maadhimisho haya yanalenga kulinda na kutetea uhuru wa vyombo vya habari na kuwaenzi wadau wa sekta hiyo ambao wakati mwingine wanahatarisha maisha yao wakitekeleza wajibu na majukumu yao.

Siku hiyo iliainishwa kutokana na pendekezo lililotolewa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO). Hii leo uhuru wa vyombo vya habari unabinywa na kukandamizwa na baadhi ya tawala za kidikteta na kimabavu zisizopenda kuona ukweli ukiwafikia watu. Katika upande mwingine uhuru wa vyombo vya habari unatumiwa vibaya na baadhi ya nchi hususan za Magharibi kutangaza kila kitu, makala, picha na filamu chafu na zinazokiuka maadili ya kibinadamu. Mwenendo huo umekwenda mbali zaidi kiasi cha kutumiwa uhuru wa vyombo vya habari kwa ajili ya kuvunjia heshima matukufu ya kidini ya mabilioni ya watu kote duniani. 

Na katika Siku kama hii ya leo miaka 42 iliyopita ndege iliyokuwa imembeba Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Muhammad Siddiq Bin Yahya, ilidunguliwa na ndege za kivita za Iraqi baada ya kufanya ziara nchini Iran.

Baada ya tukio hili, mwakilishi maalumu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wajumbe kadhaa walitumwa kwenye eneo la tukio kwa ajili ya uchunguzi. Maafisa wa Iran walitangaza kuwa kwa mujibu wa nyaraka zilizopatikana, ndege za kivita za Iraq zilikuwa zikiikimbiza ndege ya Algeria.

Shambulio la ndege za kivita za Iraq dhidi ya ndege iliyokuwa imembeba Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria liliitia doa serikali ya Iraq mbele ya macho ya walimwengu hususan nchi za Kiarabu za eneo Mashariki ya Kati.

Muhammad Siddiq Bin Yahya