May 04, 2024 07:47 UTC
  • Jumamosi, 4 Mei 2024

Leo ni Jumamosi 25 Mfunguo Mosi Shawwal 1445 Hijria mwafaka na 4 Mei 2024 Miladia.

Leo tarehe 15 Ordebehesht Hijiria Shamsia ni siku ya kumuenzi Sheikh Swaduq, msomi mashuhuri wa Kiislamu. Abu Ja'far Muhammad Ibn Ali ibn Babawayh maarufu kwa jina la Sheikh Swaduq alizaliwa katika ene9o la Qum nchini Iraq yapata mwaka 306 Hijiria katika familia ya wasomi. Akiwa kijana mdogo alianza kujifunza elimu ya dini ya Kiislamu na kufanikiwa kukwea marhala za elimu kutoka kwa baba yake na maulama wengine wa zama zake. Baada ya hapo alifikia daraja za juu katika elimu, huku akifanya safari katika maeneo tofauti kwa ajili ya kusoma zaidi na kukusanya hadithi ambapo inaelezwa kuwa alipata kusoma kwa wasomi zaidi ya 200 wa zama zake. Baada ya kufanya safari mjini Baghdad, wasomi wa mji huo walivutiwa naye sana na wakapata kusoma kwake. Miongoni mwa wanafunzi wake ni pamoja na Sheikh Al-Mufid, Hassan Bin Muhammad Qumi, Alamul-Huda Sayyid Murtadha, na wengine wengi. Ameacha athari nyingi ambazo miongoni mwazo ni 'Man laa Yahdhuru al-Faqihi' chenye juzuu nne ambacho ni kati ya vitabu mashuhuri kwa Waislamu wa Shia na chenye hadithi 6000 na pia kitabu cha 'Madinatul-Ilm' chenye juzuu 10, 'Aamaal, Khiswaal', 'Uyuunu Akhbaar al-Ridha (as)' na 'Ilalu ash-Sharaaii'.  ***

Sheikh Saduq

 

Siku kama ya leo miaka 1297 iliyopita Imam Ja'far Sadiq mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu (saw), aliuawa shahidi kwa amri ya mtawala dhalimu wa Kiabbasi Mansur al Dawaniqi. Imam Sadiq alizaliwa mwaka 83 Hijria katika mji mtakatifu wa Madina. Alishika hatamu za kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 31 baada ya kuuawa shahidi baba yake Imam Muhammad Baqir. Imam Sadiq ambaye kipindi cha uongozi wake kilisadifiana na zama za mapigano makali kati ya watawala wa Kiumawi na Kiabbasi, alitumia fursa hiyo kueneza elimu na maarifa sahihi ya Kiislamu. Alifanikiwa kulea na kutayarisha wasomi hodari katika taaluma mbalimbali kama tiba, kemia, hesabati, nujumu hadithi na kadhalika. Jabiri bin Hayyan ambaye anatambuliwa hii leo kuwa ndiye baba wa elimu ya kemia alikuwa mwanafunzi wa Imam Ja'far Saqid (as). Ushawishi wa Imam ulienea kwa kasi katika ulimwengu wa Kiislamu, jambo ambalo halikuwafurahisha watawala wa Kiabbasi. Hatimaye mtawala Mansur al Dawaniqi aliamuru Imam apewe sumu. Mtukufu huyo aliuawa shahidi kwa sumu hiyo katika siku kama ya leo na akazikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, hayati Imam Ruhullah Khomeini akiwa na umri wa miaka 42, alitoa taarifa yake ya kwanza ya kisiasa akiwataka wananchi kusimama na kuanza harakati kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Katika taarifa hiyo Imam Khomeini alichunguza hali ya miaka ya nyuma, ya kipindi hicho na mustakbali wa wananchi wa Iran na Waislamu kwa ujumla na kusema: Kuanza harakati na mapambano kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ndiyo njia pekee ya kurekebisha hali ya dunia. Alisema suala hilo ndiyo falsafa ya kutumwa Manabii wote wa Mwenyezi Mungu. Imam pia alieleza sababu za hali mbaya ya Waislamu na wananchi wa Iran na kukumbusha majukumu mazito ya wanazuoni wa dini na athari mbaya za tabaka hilo kughafilika na masuala ya kisiasa. Katika taarifa hiyo Imam Khomeini alipiga kengele ya hatari na kuwaamsha Waislamu husuan wanafunzi wa vyuo vya kidini kuhusu umuhimu wa kusimama na kuanza mapambano ya kurekebisha umma. ***

 

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita chama cha National Socialism cha Ujerumani mashuhuri kwa jina la chama cha Nazi, kilivunjwa rasmi nchini humo. Kwa utaratibu huo kipindi cha utawala wa kidikteta, ukandamizaji na mabavu cha chama hicho ambacho kiliingia madarakani tangu mwaka 1932 nchini Ujerumani, kilifikia ukingoni. Si vibaya kuashiria hapa kuwa, chama cha Nazi kiliundwa mwezi Oktoba mwaka 1920 baada ya kuongezeka harakati ya kisiasa za Munich. Hadi mwaka 1929 chama hicho kilikuwa na wanachama laki moja na 76 elfu tu lakini mwaka 1933 idadi hiyo iliongezeka na kufikia milioni mbili na kuongezeka zaidi hadi kufikia milioni sita katika miaka iliyofuata. Inaelezwa kuwa, chama hicho kilikuwa na lengo la kuyaunganisha mataifa yanayozungumza Kijerumani na kuanzisha dola moja lenye nguvu ambalo lingeweza kupanua mipaka yake. Hata hivyo baada ya kushindwa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia chama hicho cha Nazi kilisambaratika na kutoweka. ***

 

Tarehe 4 Mei miaka 54 iliyopita wanafunzi wanne wa Chuo Kikuu cha serikali cha Kent katika jimbo la Uhio nchini Marekani waliuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Gadi ya Taifa na wengine kadha wakajeruhiwa katika maandamano ya Wamarekani ya kupinga vita vya Vietnam. Kuanza mwaka 1969 Wamarekani hususan vijana walizidusha upinzani na maandamano ya kupinga vita na uvamizi wa nchi hiyo dhidi ya Vietnam. Maandamano hayo yalishadidi baada ya kufichuliwa habari ya mauaji ya mamia ya Wavietnam katika kijiji cha My Lai (My Lai massacre) na vilevile mwaka 1970 baada ya kuchapishwa habari ya kupanuka zaidi vita vya Vietnam na kuingia Cambodia. ***

Mauaji dhiidi ya wanafunzi katika Chu Kikuu cha Kent

 

Katika siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, Josip Broz Tito, kiongozi wa Yugoslavia na mmoja wa waasisi wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM alifariki dunia. Wakati wa kujiri Vita vya Kwanza vya Dunia mwaka 1915, Tito aliyekuwa akipigana dhidi ya Russia alitiwa mbaroni na baada ya kuachiliwa huru akiwa na Wakomonisti alipigana vita dhidi ya utawala wa Tzar. Kwa muda fulani, Tito alikuwa na nafasi muhimu kkatika Chama cha Kikomonisti cha Yugoslavia na alifungwa jela miaka 6 kwa kosa hilo. Tito aliiongoza Yugoslavia kwa muda wa miaka 35. Josip Broz Tito aliaga dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 88 baada ya kuugua kwa muda mrefu. ***

Josip Broz Tito