May 24, 2024 02:30 UTC
  • Ijumaa, Mei 24, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 15 Dhilqaada 1445 Hijria sawa na 24 Mei 2024.

Siku kama ya leo miaka 945 iliyopita, alifariki dunia Ibn Fakhir, msomi na mtaalamu mkubwa wa lugha wa Kiislamu mjini Baghdad.

Akiwa kijana, Ibn Fakhir alifanya safari huko Makkah na Yemen na kukutana na maulama wakubwa wa zama hizo, ambapo alitokea kuwa alimu mkubwa wa lugha na Hadithi.

Miongoni mwa athari za Ibn Fakhir ni pamoja na kitabu kinachoitwa ‘Jawabul-Masaail.’   ***

Siku kama ya leo miaka 481 iliyopita, aliaga dunia mnajimu na mwanahesabati mashuhuri wa Poland, Nicolaus Copernicus akiwa na umri wa miaka 70.

Alizaliwa mwaka 1473 ambapo awali alijifunza elimu ya nujumu na baadaye tiba, na baada ya kukamilisha masomo alianza kufundisha hesabati huko Roma. Hata hivyo Copernicus aliendelea kudurusu na kufanya utafiti wa elimu ya nujumu na mwaka 1503 alivumbua nadharia ya harakati ya dunia kuzunguka jua na vilevile dunia kujizunguka yenyewe katika kila baada ya masaa 24.

Nicolaus Copernicus alifariki dunia tarehe 24 Mei 1543 siku chache tu baada ya kuchapisha kitabu cha On the Revolutions of the Celestial Spheres kinachofafanua nadharia zake.

Inafaa kuashirikia hapa kuwa, karne kadhaa kabla ya Corpenicus, mnajimu na msomi maarufu Muirani, Abu Raihan Biruni alikuwa tayari ameshavumbua ukweli kuwa sayari ya dunia huzunguka jua. Katika moja ya vitabu vyake, Corpenicus ameashiria ukweli huo.  ***

Siku kama ya leo miaka 202 iliyopita, nchi ya Ecuador ilipata uhuru wake kutoka kwa mkoloni Muhispania.

Ecuador ni moja ya nchi za Amerika ya Kusini ambayo kupitia uongozi wa Simón Bolívar mwanamapinduzi maarufu wa Venezuela, ilifanikiwa kuwa huru na kujiunga na umoja wa Colombia Kubwa. Hata hivyo umoja huo ulisambaratika haraka na kufanya nchi wanachama wa umoja huo ikiwemo Ecuador kuasisi mfumo wa jamhuri.  ***

Katika siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, nchi ya Eritrea iliyoko kaskazini mashariki mwa bara la Afrika ilijitenga na Ethiopia na kujitangazia uhuru.

Mwaka 1936 Miladia Italia iliikalia kwa mabavu Eritrea iliyokuwa ikihesabiwa katika zama hizo kuwa sehemu ya ardhi ya Ethiopia. Mwaka 1953, Italia iliirejeshea Ethiopia ardhi hiyo. Hata hivyo wananchi wengi wa nchi hiyo waliokuwa wakitaka uhuru walianzisha harakati za ukombozi dhidi ya serikali ya Ethiopia.

Mwaka 1991, Harakati ya Ukombozi wa Eritrea ikisaidiana na wanamapinduzi wa Ethiopia walihitimisha utawala wa kidikteta wa Mfalme Mengistu Haile Mariam, na wakakubaliana kuanishwa mustakbali wa Eritrea mwaka 1993 kupitia kura ya maoni. Washiriki wengi wa kura hiyo ya maoni walipiga kura ya kutaka kujitawala Eritrea. **

Miaka 24 iliyopita katika siku kama ya leo, vikosi vya utawala dhalimu wa Israel vililazimika kuondoka kwa madhila katika eneo la kusini mwa Lebanon baada ya kulikalia kwa mabavu eneo hilo kwa muda wa miaka 22.

Majeshi hayo yaliondoka baada ya kushindwa kukabiliana na mapambano ya wananchi wa kusini mwa Lebanon. Mwaka 1982, majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel yalishambulia Lebanon na kusonga mbele hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo Beirut. Hata hivyo kutokana na wananchi hao kuathirika na mafunzo ya kutokubali dhulma hasa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, nchini Lebanon kulianzishwa harakati za mapambano ya Kiislamu dhidi ya majeshi vamizi ya utawala haramu wa Israel.

Harakati ya Hizbullah ilikuwa na nafasi muhimu na ya kuzingatiwa mno katika kukombolewa eneo la kusini mwa Lebanon toka katika makucha ya utawala dhalimu wa Israel.  **

Tags