Hikma za Nahjul Balagha (50)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 50 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 50 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 43.
وَ قَالَ (علیه السلام) فِی ذِکْرِ خَبَّابِ بْنِ الْأَرَتِّ: [رَحِمَ] یَرْحَمُ اللَّهُ خَبَّابَ بْنَ الْأَرَتِّ، فَلَقَدْ أَسْلَمَ رَاغِباً، وَ هَاجَرَ طَائِعاً، وَ قَنِعَ بِالْکَفَافِ، وَ رَضِیَ عَنِ اللَّهِ، وَ عَاشَ مُجَاهِداً
Katika hikma hii ya 43, Imam Ali AS anasema kuhusu Khabbab ibn al Aratt kwamba: Mwenyezi Mungu amrehemu Khabbab ibn al Aratt, alisilimu kwa khiyari, akafanya Hijra kwa utiifu, na akatosheka na alichoruzukiwa na Allah na aliishi akiwa mujahid.
Kwenye sehemu hii ya 50 ya mfululizo wa vipindi hivi vya Hikma za Nahjul Balagha Imam AS anamsifu mmoja wa Mujahidina wa Uislamu ambaye ni katika watu wa awali kabisa kuingia kwenye Uislamu na akashikamana vilivyo na dini hiyo tukufu hadi mwisho wa umri wake. Akiitwa Khabbab ibn al Aratt. Anataja sifa ya kwanza ya Sahaba huyo mtukufu akisema ilikuwa ni mapenzi yake makubwa kupindukia kwa Uislamu. Hakuukubali Uislamu kwa woga na kutenzwa nguvu, bali aliupenda kwa moyo safina kwa dhati ya moyo na kwa kutambua uhakika wake. Wala hakuingia kwenye Uislamu kwa tamaa na kufuata mambo kibubusa, bali kwa weledi kamili. Wakati Waislamu walipokuwa wachache huku kila aina ya mateso yakiwaangukia wao, Khabab alisimama kidume na kishujaa na alibaki imara na hakutetereka kwenye imani na itikadi yake. Imeandikwa katika historia kwamba washirikina wa Makka walimchukua Khabbab na kumvisha nguvu za chuma kama walivyowafanyia Waislamu wengine wanyonge na kumuweka kwenye jua kali na kwenye mchanga wa Makka unaounguza sana ili ateseke kwa joto lisilovumilika na mwishowe aachane na Uislamu, lakini walishindwa. Walipoona ukatili wao huo mkubwa hauna athari zozote kwenye imani ya chuma na madhubuti ya Khabab, washirikina wa Makkah waliwasha moto wa kuni na hata ulipokoka kisawasawa walimvua nguo Khabab na kumbanika kwenye moto huo mbele na nyuma kama anavyobanikwa samaki. Khabbab mwenyewe anahadithia mateso hayo akisema: Wakati huo akiwa amelazwa juu ya moto uliokokwa mpaka ukapiga wekundu, mtu kutoka kabila la Kikuraishi alikwenda akadidimiza mguu wake kwenye kifua changu na akaushikilia mpaka moto ukazimwa na nyama na ngozi ya mwili wangu. Makovu ya moto huo yaliendelea kuwa mwilini mwa Sahaba Khabab hadi mwisho wa maisha yake. Wakati Umar alipochukua ukhalifa alikutana na Khabab siku moja na akamuuliza kuhusu mateso aliyoyapata kutoka kwa washirikina wa Kikuraish mwanzoni mwa Uislamu, Khabab alisema: Tazama mgongo wangu, na Umar alipouona mgongo wake, alisema. : Sijawahi kuona kitu kama hiki umri wangu wote.
Kufanya Hijrah kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ni sifa ya pili ya "Khabbab". Pengine baadhi ya watu walihama Makka na kuhamia Madina kutokana na woga na kukimbia mateso ya washirikina wa Makka au tamaa ya kufaidika na kipato au kupata mke na vitu kama hivyo. Lakini Sahaba Khabbab yeye alifanya Hijra kwa ajili tu ya kutii amri za Mwenyezi Mungu. Kama tunavyojua, Hijra ya Bwana Mtume Muhammad SAW ya kuhamia Madina ilifungua ukurasa mpya katika historia ya Uislamu. Waislamu mjini Madina walishirikiana, walipendana sana na waliunda Serikali ya Kiislamu chini ya uongozi wa Bwana Mtume Muhammad SAW.
Sahaba Khabbab alikuwa mtu wa kuridhika na kukinai. Aliishi maisha mepesi na ya kujinyima raha, na tunajua kwamba watu walioridhika ni watu wa heshima na wenye imani thabiti na imara ambao kamwe hawasalimu amri mbele ya mataghuti na madhalimu bali wanatii na kusujudu mbele ya Allah tu.
Sifa nyingine bora kabisa ya Sahaba Khabbab ambayo Imam Ali AS anaitaja kwenye hikma hii, ni kuridhika kwa yanayomridhisha Allah na kuridhia maamuzi ya Muumba.
Jihadi na kujitolea mhahnga Sahaba Khabbab katika medani za vita wakati wa Bwana Mtume na baadaye wakati wa Imam Ali AS ni sifa nyingine ya aina yake aliyokuwa nayo Sahaba Khabbab RA. Ni kwa sababu hiyo ndi maana Imam Ali Ali akasema mwishoni mwa hikma hii kwamba Khabbab aliishi akiwa mujahid. Sahaba huyo mtukufu alizikwa kwenye makaburi ya nyuma ya mji wa Kufa wa Iraq ya Leo baada ya kupitisha umri uliojaa baraka, jihadi, kukinai na kuitaliki dunia. Wakati Imam Ali AS alipokuwa pembeni mwa kaburi la Sahaba huyo mtukufu alisema: Hongera kwa mtu ambaye anaangalia mbali na anatekeleza vizuri majukumu yake ya kujiandaa kwa ajili ya Siku ya Malipo, anayeishi kwa kukinai na kuwa radhi na Mwenyezi Mungu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.