Jun 18, 2024 10:34 UTC
  • Jumapili, 16 Juni, 2024

Leo ni Jumapili 9 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1445 Hijria mwafaka na 16 Juni 2024 Miladia.

Leo ni siku ya Arafa tarehe 9 Dhilhaji. Arafa ni jina la jangwa kubwa linalopakana na mlima Jabalur Rahma ulioko kusini mashariki mwa Makka. Tangu adhuhuri ya siku hii mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba, husimama katika uwanja wa Arafa, na Hadithi nyingine za Mtume (saw) na Ahlibaiti zake watoharifu zimetaja fadhila na utukufu mkubwa wa kisimamo hicho. Hadithi zinasema kuwa, Mwenyezi Mungu SW ameifanya ardhi ya Arafa ambayo ilikuwa medani ya matukio mengi muhimu ya kihistoria, kuwa mahali pa kuwapokea wageni wake wanaokwenda Hija na ameweka meza na karamu yake pembeni ya mlima Jabalur Rahma. Ni vyema kukumbusha kuwa magharibi ya siku hii ya leo mahujaji wanaondoka uwanja wa Arafa na kuelekea Mash'arul Haram na kujitayarisha kwa ajili na amali nyingine za Hija. ***

 

Siku kama ya leo miaka 1385 iliyopita, Muslim bin Aqil binamu wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib AS aliuawa shahidi huko Kufa nchini Iraq. Alikuwa mmoja wa shakhsia wakubwa na wacha Mungu katika zama zake. Alielekea al-Kufa, Iraq akiwa na lengo la kwenda kutathmini ni kwa kiwango gani watu wa eneo hilo walikuwa wakimtii Imam Hussen, baada ya watu wa mji huo kumwandikia maelfu ya barua mjukuu huyo wa Mtume wakimtaka aende Kufa na kwamba wako tayari kumuunga mkono katika harakati yake dhidi utawala dhalimu wa Yazid bin Muawiya. Watu wa Kufa walimsaliti Muslim bin Aqil baada ya kuhadaika kwa hila na uongo wa Ubeidullah bin Ziyad, mtawala wa wakati huo wa Kufa, na wakamuacha Muslim bin Aqil peke yake. ***

Mahali alipozikwa Muslim bin Aqil

 

Miaka 897 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Kkiislamu, aliaga dunia Fadhl bin Hassan Tabarsi anayejulikana kwa lakabu la Aminul Islam, alimu, mpokeaji wa hadithi na mfasiri mkubwa wa Qur'ani. Fadhl bin Hassan Tabarsi alikuwa mwanazuoni mkubwa na alikuwa akiheshimiwa na makundi mengi ya Kiislamu. Sheikh Tabarsi pia alikuwa miongoni mwa makadhi waadilifu katika zama zake. Kitabu muhimu zaidi cha msomi huyo wa Kiislamu ni tafsiri ya Qur'ani ya Majmaul Bayan yenye juzuu kumi. Vilevile ameandika tafsiri nyingine ya Qur'ani aliyoipa jina la Jawamiul Jamii. ***

Mahali linapopatikana kaburi la Sheikh Tabarsi

 

Katika siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, yaani sawa na tarehe 16 Juni mwaka 1944, wanajeshi wa majini wa Marekani waliaza kushambulia kwa mabomu miji ya Japan sambamba na kuulenga mji wa Fokula ulioko kusini mwa nchi hiyo. Hayo yalijiri wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Aidha mashambulizi hayo yalifanyika kwa lengo la kuilazimisha Tokyo isalimu amri. Katika mashambulizi hayo makumi ya maelfu ya raia wa Japan waliuawa na kujeruhiwa, sambamba na kuangamizwa viwanda na mashamba ya nchi hiyo. Vita hivyo vilipelekea Marekani kushambulia kwa mabomu ya nyuklia miji miwili ya Japan ya Hiroshima na Nagasaki mwezi Oktoba mwaka 1945. ***

 

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita sawa na tarehe 16 Juni 1963, Valentina Tereshkova mwanamke wa kwanza duniani mwanaanga kutoka Russia, alianza safari yake ya angani kwa kutumia safina ya anga iliyoitwa Vostok-6. Mwanake huyo alitua katika orbiti ya ardhi wakati ambao Valery Bykovsky mwanaanga mwingine wa Russia alipokuwa akijishughulisha pia kuzunguka dunia. Safari ya Tereshkova katika anga za juu ilifanyika miaka miwili baada ya safari ya Yuri Gagarin ambayo ilikuwa ya kwanza kufanywa na mwanadamu katika anga hizo. Katika muda wa masaa 70 na dakika 50 aliyokuwa katika anga za juu, Tereshkova alizunguka dunia mara 48. ***

 

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita wananchi wa Soweto huko Afrika Kusini walianza harakati za mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi wa makuburu. Katika kipindi hicho Afrika Kusini ilikuwa ikitawaliwa na wazungu wachache waliodhibiti kila kitu na sheria zilizokuwa dhidi ya binadamu. Juni 16 mwaka 1976 maelfu ya wanafunzi wazalendo walifanya maandamano makubwa kupinga sera za kibaguzi katika sekta ya elimu ambayo yalikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa utawala wa kibaguzi. Mamia ya raia waliuawa na wengine kujeruhiwa. ***

 

Siku kama ya leo miaka 45  iliyopita, yaani tarehe 27 Khordad kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani ya Hijria Shamsia, Imam Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa amri ya kuasisiwa taasisi ya Jihadi ya Ujenzi kwa ajili ya kulinda uhuru wa Iran, kujitegemea na kumaliza umaskini hususan katika maeneo ya vijijini. Kufuatia kutolewa amri hiyo, wananchi wa matabaka mbalimbali hasa wanafunzi na wanachuo, vijana wenye ghera na imani na wasomi walijitolea kwenda kufanya kazi za ujenzi za kuwasaidia watu maskini katika pembe mbalimbali za Iran. Taasisi ya Jihadi ya Ujenzi imezaliwa kutoka ndani ya Mapinduzi ya Kiislamu na hadi sasa inafanya kazi kubwa za ujenzi na kusaidia watu maskini na wenye haja. Taasisi hiyo inajihusisha na mambo mengi yakiwemo masuala ya viwanda, kazi za vijijini, kilimo, ufugaji, ujenzi wa mabwawa, kulinda mazingira na makumi ya kazi nyingine za kujenga taifa. Mwaka 1362 Hijria Shamsia Taasisi ya Jihadi ya Ujenzi ya Iran ilibadilishwa na kuwa Wizara, na mwaka 1379 Hijria Shamsia iliingizwa kwenye Wizara ya Kilimo ya Iran. ***

Tags