Jul 02, 2024 04:08 UTC
  • Jumanne, tarehe Pili Julai, 2024

Leo ni Jumanne tarehe 25 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1445 Hijria sawa na tarehe Pili Julai 2024.

Tarehe 25 Dhulhija inasadifiana na siku ya kuteremshwa Suratu Dahr ambayo inawahusu Imam Ali bin Abi Twalib, mkewe Bibi Fatimatu Zahra na watoto wao Hassan na Hussein (as).

Baada ya watukufu hao kuweka nadhiri ya kufunga swaumu siku tatu kwa ajili ya kukidhiwa haja zao na kuanza kutekeleza nadhiri hiyo, katika siku zote tatu za swaumu masikini, yatima na fakiri walikwenda nyumbani kwa Imam Ali (as) na kuomba chakula. Watukufu hao walitoa chakula chao kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili ya futari na kuwapa wahitaji hao kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu.

Hali hiyo iliendelea kwa siku tatu za kutimiza nadhiri ya swaumu na wakati huo ndipo iliporetemshwa Suratu Dahr ikipongeza na kubakisha hai tukio hilo.

Siku kama ya leo miaka 135 iliyopita mfumo wa kisultani ulifutwa huko Brazil katika mapinduzi ambayo hayakuwa na umwagaji wa damu na badala yake ukaasisiwa mfumo wa jamhuri.

Mfalme wa mwisho wa Brazil alikuwa Pedro II ambaye alifanya jitihada za kufanya mabadiliko nchini humo. Hatua za mfalme huyo hususan ile ya kuondoa biashara ya utumwa mwaka 1888, iliwakasirisha wamiliki wa ardhi waliokuwa wakiunga mkono mfumo wake wa kisultani.

Pedro II alienguliwa madarakani bila ya mapambano yoyote na mfumo wa jamhuri ukaasisiwa nchini Brazil.

Miaka 99 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Patrice Lumumba mhandisi wa uhuru wa Kongo.

Lumumba alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kukombolewa Kongo wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kiafrika. Lumumba aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi baada ya kuundwa Jamhuri ya Kongo mwaka 1960. Patrice Lumumba aliuawa mwaka 1961 na vibaraka wa Marekani na Ubelgiji baada ya kuvumilia mateso na unyama mkubwa.

Lumumba aliandika vitabu kadhaa wakati wa uhai wake na mashuhuri zaidi ni kile alichokita "Kongo, Nchi Yangu."

Patrice Lumumba

Tarehe 12 Tir 1349 Hijria Shamsia, yaani miaka 54 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia Allamah Abdul Hussein Amini, faqihi mkubwa na mwandishi hodari na mashuhuri wa Kiislamu.

Kitabu cha kwanza cha mwanazuoni huo alikipa jina la Shuhadaul Fadhila. Hata hivyo kitabu mashuhuri na kikubwa zaidi cha Allamah Amini ni kile cha "al Ghadiir Fil Kitabi Wassunnah". Ndani ya kitabu hicho Allamah Amini amekosoa na kuchunguza vitabu vikubwa na marejeo vya Kiislamu 150 akithibitisha wilaya na haki ya Imam Ali bin Abi Twalib ya kuwa Khalifa na Imam wa Waislamu baada tu ya Mtume Muhammad (saw) kufariki dunia.

Mwanazuoni huyo alisafiri kwa taabu katika nchi nyingi kama India, Uturuki, Syria, Misri na Iraq kwa ajili ya kukusanya ushahidi wa kihistoria alioutumia katika kitabu hicho.

mah Abdul Hussein Amini

Tarehe Pili Julai miaka 63 iliyopita aliaga dunia mwandishi mtajika wa Kimarekani kwa jina la Ernest Hemingway.

Alizaliwa mwaka 1899 na kwa muda fulani alijishughulisha na uandishi huko Uingereza na Ufaransa. Hemingway alianzisha mbinu ya kuandika riwaya na tungo fupi fupi na alikuwa akitumia lugha nyepesi na inayoeleweka. Mwaka 1954 mwandishi Ernest Hemingway alitunukukiwa tuzo ya Nobel katika medani ya fasihi.

Miongoni mwa vitabu maarufu vya Hemingway ni "The Old Man and The Sea", "A Farewell to Arms" na For Whom The Bell Tolls".

Ernest Hemingway

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita ndege ya abiria aina ya Airbus ya shirika la ndege la Iran iliyokuwa ikitoka Bandar Abbas, kusini mwa Iran na kuelekea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, ilishambuliwa kwa makombora mawili ya jeshi la Marekani kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi.

Manowari ya kijeshi ya Marekani USS Vincennes ilifyatua makombora hayo na kuua shahidi abiria wote 298 waliokuwa katika ndege hiyo. Shambulio hilo lilidhihirisha zaidi unyama wa serikali ya Marekani.

Viongozi wa Marekani walizidisha ukatili wao pale walipomzawadia medali ya ushujaa nahodha wa meli hiyo kutokana na kitendo hicho kilichoonekana na serikali ya Washington kuwa eti ni cha kishujaa.   

 

Tags