Jul 07, 2024 02:20 UTC
  • Jumapili, 7 Julai, 2024

Leo ni Jumapili tarehe Mosi Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria mwafaka na tarehe 7 Julai 2024.

Tarehe Mosi Muharram inasadifiana na kuanza mwaka mpya wa Hijria Qamaria. Mwaka wa Hijria Qamaria unahesabiwa kwa mujibu wa mzunguko wa mwezi na katika nchi nyingi za Kiislamu unatumiwa kwa ajili ya masuala ya kidini au hata kijamii. Mwaka wa Hijria Qamaria pia unatumika katika masuala mengi ya kiibada kama vile kuainisha mwanzo wa funga ya mwezi wa Ramadhani, Hija, kuainisha miezi mitakatifu na kwa ajili ya historia ya matukio mbalimbali. Mwaka wa Hijria ulianzishwa katika zama za utawala wa Khalifa Umar bin Khattab kutokana na ushauri uliotolewa na Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as) ambaye aliagiza mwanzo wa hijra ya Mtume kutoka Makka na kwenda Madina uwe mwanzo wa mwaka wa Kiislamu. Kabla ya kalenda ya Miladia kutumika kote duniani, nchi nyingi za Kiislamu zilikuwa zikitumia kalenda ya Hijria Qamaria. ***

 

Miaka 217 iliyopita mwafaka na siku kama hii ya leo, ulitiwa saini mkataba wa kihistoria wa Tilsit katika mji wenye jina hilo huko Russia kati ya Alexander wa Kwanza, mfalme wa Russia na Napoleon Bonaparte wa Ufaransa. Kwa mujibu wa mkataba huo Urusi na Ufaransa zilikubaliana kuwa, ikiwa nchi yoyote ingeishambulia nchi moja wapo kati ya hizo, zingesaidiana kumpiga adui. Mkataba huo wa urafiki, uliendelea hadi mwaka 1810. ***

Napoleon Bonaparte

 

Katika siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, visiwa vya Solomon vilivyoko kaskazini mashariki mwa Australia katika bahari ya Pacific vilipata uhuru. Visiwa hivyo viligunduliwa na watu kutoka Ulaya mwaka 1567. Mwaka 1885 Ujerumani ilidai umiliki wa visiwa vya kaskazini mwa Solomon na ndiyo maana ikachukua hatua ya kuvishambulia na kisha kuvikalia kwa mabavu. Muongo mmoja baadaye, Uingereza ilivishambulia visiwa hivyo na kuvidhibiti. Harakati ya kupigania uhuru ilianzishwa katika visiwa hivyo baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kuzaa matunda katika tarehe kama ya leo ambapo visiwa hivyo vilipata uhuru.   ***

Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Muhammad Mahdi Rabbani Amlashi aalimu na mujahidi wa Kiirani. Ayatullah Amlashi alizaliwa mwaka 1313 Hijria Shamsia katika familia ya kidini katika mji mtukufu wa Qum na kuanza masomo ya kidini katika mji huo. Mwanazuoni huyo alipambana vilivyo kwa miaka mingi katika njia ya kuutetea Uislamu na kulinda thamani zake. Kama walivyokuwa viongozi na wafuasi wengine wa Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Rabbani Amlashi katika uhai wake hakuacha kufanya juhudi za kupambana dhidi ya utawala wa Shah licha ya kufungwa na kubaidishwa. ***

Ayatullah Muhammad Mahdi Rabbani Amlashi

Miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Muhammad Nasih mwanafasihi na mshairi wa Kiirani. Muhammad Ali Nasih alizaliwa mjini Tehran ambapo mbali na kujifunza elimu mpya alijihusisha pia na kusoma elimu za kale. Nasih alikuwa mwanachama wa Jumuiya ya Kifasihi ya Iran ambapo baadaye alikuwa kiongozi wa jumuiya hiyo hadi anaaga dunia. ***

Muhammad Ali Nasih

 

Tarehe 7 Julai mwaka 2005 kulitokea mlipuko katika basi na milipuko mingine katika vituo vitatu vya treni ya chini ya ardhi katikati mwa mji mkuu wa Uingereza, London na kusababisha vifo vya watu 50 na wengine wapatao 700 kujeruhiwa. Mashambulio hayo yalifanywa sambamba na kikao cha Viongozi wa Nchi Tajiri Kiviwanda Duniani G8 huko nchini Scotland kaskazini kwa Uingereza. Mashambulio hayo ya mabomu yalitekelezwa ili kupinga ushirikiano wa London na Washington katika kuikalia kwa mabavu Afghanistran na Iraq na kuuawa kiholela wananchi wa nchi hizo. Serikali ya Uingereza ilidai kwamba, Waislamu walihusika na tukio hilo, na kwa muktadha huo mashinikizo dhidi ya Waislamu wa Uingereza yaliyoanza baada ya mashambulio ya Septemba 11, 2001 yakashadidi zaidi. ***

 

Tags