Alkhamisi, tarehe 6 Machi, 2025
Leo ni Alkhamisi tarehe 5 Ramadhani 1446 Hijria sawa na tarehe 6 Machi mwaka 2025.
Katika siku kama ya leo miaka 550 iliyopita, alizaliwa Michelangelo, mchoraji na mhunzi wa masanamu wa Italia katika mjini Caprese.
Licha ya upinzani mkubwa wa baba yake dhidi ya sanaa hiyo ya uhunzi na uchoraji, Michelangelo alijiendeleza katika taaluma hiyo na kupata umahiri mkubwa. Uhodari wake ulionekana miaka michache baadaye ambapo alifanikiwa kuchonga masanamu mengi ya kuvutia. Michelangelo, alitokea kuwa mhunzi hodari wa karne ya 16 Miladia.
Mwaka 1505, wakazi wa mji wa Roma walimwalika Michelangelo, ili aende kuwachongea sanamu la papa kwenye kaburi lake. Baadaye papa wa wakati huo, alimtaka mtaalamu huyo kupamba paa la kanisa la Sistine, kazi iliyoanza hapo mwaka 1508 na kumalizika mwaka 1512. Mbali na hayo, Michelangelo alichonga sanamu kubwa la Nabii Issa (as), ambalo lipo mjini Roma hadi leo.

Miaka 125 iliyopita katika siku kama hii ya leo aliaga dunia mvumbuzi wa Kijerumani Gottlieb Daimler akiwa na umri wa miaka 64.
Daimler alizaliwa mwaka 1834 na kazi yake ya mwanzo ilikuwa utengenezaji bunduki. Tangu akiwa kijana mvumbuzi huyo alivutiwa sana na kazi za viwandani na alifanya utafiti mkubwa katika uwanja huo hadi alipofanikiwa kutengeneza pikipiki. Gottlieb Daimler pia alikuwa miongoni mwa watu walioweka misingi ya utengenezaji wa magari madogo na hata mabasi.

Siku kama ya leo, miaka 88 iliyopita, alizaliwa, Valentina Tereshkova, mwanamke wa kwanza mwanaanga wa dunia.
Akiwa kijana na baada ya kushiriki katika mashindano ya kuruka kwa mwavuli, Tereshkova aliibuka mshindi na hivyo kufikia daraja la ukapteni katika kikosi cha anga cha jeshi la Urusi ya zamani. Ni baada ya hapo ndipo akajifunza urubani wa ndege.
Hatimaye tarehe 16 mwezi Juni, mwaka 1963 na akiwa na umri wa miaka 22, aliweka rekodi ya dunia kwa kuwa mwanamke wa kwanza mwanaanga, baada ya kuanza safari ya mwezini na chombo cha Vostok 6.

Tarehe 6 Machi miaka 68 iliyopita, nchi ya Ghana ilifanikiwa kupata uhuru chini ya uongozi wa Dakta Kwame Nkurumah.
Ghana ilitumbukia katika makucha ya mkoloni wa Kireno kuanzia karne ya 15. Baada ya Wareno, Waingereza waliidhibiti na kuikoloni nchi hiyo iliyokuwa mashuhuri kwa jina la "Pwani ya Dhahabu" kutokana na utajiri wake mkubwa wa madini hayo.
