Aug 01, 2016 06:08 UTC
  • Spoti, Agosti 1

Hujambo mpenzi msikilizaji na karibu katika dakika hizi chache za kukupasha matukio kemkem ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita hapa nchini na katika sehemu mbalimbali ya dunia. Nakusihi usibanduke kando ya radio yako hadi tamati ya kipindi, karibu…………………

Iran yatwaa Taji la Basketboli U18 la Asia

Timu ya taifa ya mpira wa kikapu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa Taji la Basketboli barani Asia kwa vijana wa kiume wenye chini ya umri wa miaka 18 mwaka huu 2016. Timu hiyo ilitwaa taji hilo linalofahamika kama FIBA baada ya kuibamiza Japan vikapu 71-65 katika mchuano wa fainali uliopigwa katika ukumbi wa michezo wa Azadi hapa Tehran.

Mabarobaro hao wa Iran walitinga fainali baada ya kuwachachawiza vijana wa Korea Kusini vikapu 85-65 siku ya Jumamosi. Hii ni mara ya tatu kwa timu hiyo ya taifa ya Iran kutwaa kombe hilo la FIBA katika mashindano ya Asia U18 Championship ikizingatiwa kuwa walitwaa taji hilo mwaka 2004 na 2008 mbali na kumaliza katika nafasi ya pili katika mashindano ya mwaka 2002 na 2014. Shangwe, nderemo vifijo vilihinikiza uwanja wa Azadi baada ya timu hiyo ya Iran kutawazwa mabingwa wa basketboli barani Asia.

Kwa ushindi huo, Timu ya taifa ya mpira wa kikapu ya vijana wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wenye chini ya miaka 18, Japan na Korea Kusini  zimejikatia tiketi ya kushiriki Mashindano ya Dunia ya Mpira wa Kikapu kwa vijana wenye chini ya miaka 19 nchini Misri mwaka ujao 2017.

Ligi Kuu ya Soka ya Iran yaanza

Ligi Kuu ya Soka ya Iran imeanza kwa kishindo ambapo mechi kadhaa za kusisimua zimeshuhudiwa katika viwanja na mikoa mbalimbali ya nchi. Klabu ya Persepolis iliitandika Saipa bao 1-0 katika mchuano wake wa ufunguzi uliopigwa katika uwanja wa Takhti hapa Tehran. Bao la Persepolis lilifungwa na Kamal Kamyabina kunako dakika ya 68 ya mchezo. Wakati huohuo, Esteghlal Khuzestan imeichabanga hasimu wake wa jadi Esteghlal Tehran mabao 2-1 katika mchuano wa kukata na shoka mwishoni mwa wiki.

Mchuano wa Sarkhobi (Wekundi dhidi ya Buluu) mjini Tehran

Kwengineko Sepahan ya Isfahan ililianza vibaya msimu kwa kulimwa bao 1-0 na Padideh wakati ambapo mchuano kati ya Gostareh Foolad na Paykan ulikuwa unaishia kwa sare tasa ya kutofungana sawa na mchezo wa Saba na Sanat Naft. Foolad ilikubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka timu iliyopandishwa daraja hivi karibuni ya Machine Sazi.

Matokeo mengine ya michuano ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Soka ya Iran ambayo pia inatambulika kama Ligi Kuu ya Wataalamu ni kama yafuatayo: Esteghlal 1-1 Naft Tehran, Teraktor Sazi dhidi ya mabingwa watetezi Esteghlal Khuzestan 2-2 huku Siahjamegan ikiinyuka Zobahan mabao 2-1.

Masumbwi: Tz vs Namibia

Wanamasumbwi wawili nyota wa Tanzania Fadhil Majia na Fabian Lyimo wanatazamiwa kusafiri kuelekea Namibia Agosti 6 kugombea mataji tofauti dhidi wa mabondia wa nchi hiyo.

Majia anatarajiwa kuzipiga na Emmanuel Naidjala kuwania ubingwa wa kimataifa wa mabara (WBO) uzani wa Bantam na Lyimo atapambana na Julius Indongo kugombea mkanda wa Afrika uzani mwepesi. Kwa mujibu wa Rais wa Kamisheni ya Ndondi za Kulipwa Tanzania (TPBC) Chaurembo Palasa, mabondia hao wamenolewa wakanoleka kwani wamepiga mazoezi ka majuma kadhaa. “Mabondia wako tayari kwa mapambano hayo, wataondoka Agosti 4 mwaka huu kuelekea Namibia, tuna imani watafanya vizuri kwani wana uzoefu wa kutosha na mapambano hayo.”

Beki wa DRC aburuzwa jela

Beki wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Fabrice Lokembo-Lokaso amehukumiwa kifungo cha miezi 10 jela baada ya kupatikana na hatia ya kushiriki utumwa mambo leo. Mchezaji huyo anadaiwa kujaribu kuwasafirisha kinyume cha sheria, raia 10 wa Afghanistan nchini Uingereza. Akijitetea mbele ya korti mjini Dunkirk, Lokembo-Lokaso, 33, ambaye alicheza soka yake ya malipo nchini Ubelgiji, Israel na Cyprus, alisema deni kubwa la mamilioni ya shuilingi lililomsukuma kuingilia kazi hiyo ya kusafirisha watu hao nyuma ya gari lililokuwa likibeba samani. Alinaswa mjini Calais nchini Ufaransa akijaribu kuabiri feri ya kuelekea Dover akiwa amebeba wanaume wanne, wanawake wawili mmoja wao akiwa na mimba na watoto wanne kwenye gari lake. Amenukuliwa na vyombo vya habari akidai kuwa: “Mwanamume mmoja kwa jina Malik alinialika kusafirisha samani hadi nchini Uingereza na sikujua kilichokuwa ndani ya gari hilo. Nilipofika Calais mwanamume mwingine kwa jina Al aliniambia kilichokuwa kikiendelea na kunipa kiasi Fulani cha fedha. Mambo yalifanyika haraka sana. Madeni yananiandama kwa hivyo nilikubali kuwasafirisha,” mwisho wa kunukuu. Mbali na kufingwa jela, mshahara wa kusafirisha watu hao pia ni kurudishwa nchini DRC baada ya kutumikia kifungo chake, kulingana na gazeti la Daily Star.  Lokembo-Lokaso alistaafu baada ya kuchezea klabu ya ligi ya daraja ya nne nchini Ubelgiji mwisho wa msimu 2010-2011.

Sudan Kusini Olimpiki ya Rio

Licha ya kuendelea kushuhudiwa mgogoro wa kisiasa, mapigano na mauaji ya hapa na pale, Sudan Kusini imeingia katika madaftari ya historia kwa kushiriki kwa mara ya kwanza katika michezo ya Olimpiki baada ya kupewa fursa ya kuonyesha umbuji wake katika Olimpiki ya Rio itakayokunjua jamvi lake Ijumaa ijayo nchini Brazil.

Mashindano ya Olimpiki ya Rio nchini Brazil yanaanza Agosti 5

Hatua hii inakuja baada ya nchi hiyo iliyopata uhuru wake mwaka 2011 kuwa mwanachama wa 206 wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki IOC mwezi Agosti mwaka uliopita. Katika Olimpiki ya mwaka huu, Sudan Kusini itawakilishwa na wanariadha wawili Santino Kenti atakayeshiriki katika mbio za Mita 1500 kwa upande wa wanaume na Margaret Rumat Hassan ambaye atashiriki katika mbio fupi za Mita 200 na 400 kwa upande wa wanawake. Kadhalika IOC imeiruhusu nchi hiyo kushiriki katika michezo ya riadha, kikapu, soka, mchezo wa mkono, judo, Tenis ya mezani na Taekwondo.

………………………….….TAMATI……………………………….