Apr 17, 2025 04:08 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 17 Aprili, 2025

Leo ni Alkhamisi tarehe 18 Shawwal 1446 Hijria sawa na Aprili 17 mwaka 2025.

Katika siku kama ya leo miaka 192 iliyopita Mirza Hussein Nuri, alimu na faqihi mashuhuri wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Nur kaskazini mwa Iran.

Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali, Mirza Hussein Nuri alielekeza juhudi na jitihada zake katika masuala ya kujifunza na kukusanya Hadithi. Msomi huyo wa Kiislamu alitokea kuwa mmoja wa wanazuoni wakubwa wa masuala ya Hadithi na baadaye akaanza kuandika vitabu vya thamani katika uwanja huo.

Miongoni wma vitabu hivyo ni Akhbaru Hifdhil Qur'an, Risala ya Tuba na Muhtasari wa Historia ya Viongozi wa Uislamu.     

Mirza Hussein Nuri

Siku kama ya leo miaka 110 iliyopita, sawa na tarehe 17 Aprili 1915, kwa mara ya kwanza kabisa duniani ilitumiwa gesi ya kubana pumzi ya wanadamu vitani.

Hatua hiyo ya kinyama ilichukuliwa katika Vita vya Kwanza vya Dunia.

Ujerumani ilitumia gesi hiyo ya kubana pumzi dhidi ya askari wa Uingereza na Ufaransa na kuua askari wengi wa vikosi vya Waitifaki. Wajerumani walipata ushindi katika vita hivyo vilivyokuwa mashuhuri kwa jina la Vita vya Gesi.   

Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita, raia wa Scotland kwa jina la John Logie Baird, alifanikiwa kuvumbua televisheni ambayo hii leo imekuwa na umuhimu mkubwa katika upashaji habari duniani.

Baird alikuwa mmoja wa wavumbuzi wakubwa wa enzi zake. Baada ya hapo mtu wa kwanza kutengeneza televisheni iliyoimarika zaidi alikuwa Giovanni Caselli, raia wa Italia ambaye mnamo mwaka 1862 alifanikiwa kutengeza chombo ambacho kwa kutumia mfumo wa telegrafi, kiliweza kutoa ramani na picha.

Televisheni ya kwanza ambayo ilionyesha vizuri picha, ilianza kutumika tarehe 17 mwezi Aprili mwaka 1926 kwa ajili ya klabu ya kifalme nchini Uingereza. 

John Logie Baird

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita inayosadifiana na tarehe 17 Aprili 1946, Syria ilipatia uhuru kutoka kwa askari wa kigeni waliokuwa wakiitawala nchi hiyo.

Syria na baadhi ya ardhi zinazoizunguka awali ilikuwa ikijulikana kwa jina la Sham, na kabla ya kudhihiri dini tukufu ya Kiislamu ilikuwa chini ya udhibiti wa Iran, Ugiriki, Misri na Rome. Ardhi hiyo ilikuwa makao ya utawala wa Ugiriki na baada ya kukaliwa kwa mabavu na Misri, baadaye ilichukuliwa na utawala wa Othmaniya.

Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na baada ya kuporomoka utawala wa Othmaniya, Syria ilikoloniwa na Ufaransa. Kufikia Juni 1941, wakati wa vita vya pili vya dunia, askari wa Uingereza na Ufaransa waliikalia kwa mabavu nchi hiyo, hadi kufikia mwaka 1946 wakati ilipojipatia uhuru wake. 

Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita, mwafaka na tarehe 17 Aprili 2004, vifaru vya utawala wa Kizayuni wa Israel vilishambulia gari lililokuwa limembeba Dakta Abdulaziz Rantisi, mwanaharakati wa Palestina na kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, na kumuuwa shahidi.

Dakta Rantisi alichaguliwa kuiongoza harakati ya Hamas baada ya kuuawa shahidi Sheikh Ahmad Yassin mwasisi na kiongozi wa harakati hiyo.

Rantisi alizaliwa mwaka 1964 katika mji wa Yafa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na alihitimu elimu ya tiba kama daktari katika chuo kikuu cha Alexandria nchini Misri.   

Dakta Abdulaziz Rantisi