Jumanne, 08 Julai, 2025
Leo ni Jumanne tarehe 12 Mfunguo Nne Muharram 1447 Hijria, mwafaka na tarehe 8 Julai 2025.
Siku kama ya leo miaka 1386 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Muharram mwaka 61 Hijria msafara wa mateka wa Karbala uliokuwa na wanawake na watoto wa mashahidi wa Karbala, uliwasili katika mji wa Kufa, nchini Iraq.
Kiongozi wa msafara huo alikuwa Bibi Zainab (as) dada wa Imam Hussein bin Ali (as) pamoja na Imam Ali bin Hussein Sajjad (as), mtoto wa Imam Hussein (as). Imam Sajjad na Bibi Zaynab (as) walitekeleza majukumu yao kwa kufikisha ujumbe wa Imam Hussein kwa jamii ya Waislamu.
Siku kama ya leo miaka 1352 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, Imam Ali Zainul Abidin maarufu kwa lakabu ya Sajjad mwana wa Imam Hussein (as) na mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu S.A.W, aliuawa shahidi.
Imam Zainul Abidin alizaliwa mwaka 38 Hijria huko katika mji wa Madina. Mtukufu huyo aliishi katika zama ambapo watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu walikuwa wakikabiliwa na masaibu mengi. Imam Sajjad A.S ambaye alikuwa mgonjwa wakati wa tukio la Karbala, baada ya harakati adhimu ya Imam Hussein, alibeba jukumu kubwa la kueneza ujumbe wa mapambano hayo na kuendeleza njia ya baba yake.

Siku kama ya leo miaka 145 iliyopita aliaga dunia Pierre Paul Broca, msomi wa Kifaransa na mwanzilishi wa elimu ya kraniolojia (elimu ya fuu la kichwa).
Broca alizaliwa Juni 28 mwaka 1824 huko Ufaransa na baada ya kukamilisha masomo ya msingi na sekondari alijiunga na Chuo Kikuu kwa ajili ya kusoma taaluma ya tiba na kuhitimi vyema katika fani hiyo. Baada ya kuhitimu masomo Broca alijishughulisha na kazi ya upasuaji akiwa daktai mahiri.
Sambamba na kazi yake hiiyo aliendelea na utafiiti na uhakiki. Utafiti wake huo ulimfanya afikie ugunduzi muhimu.

Katika siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, alifariki dunia Kim Il-sung aliyekuwa Kiongozi na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti wa Korea Kaskazini.
Kim Il-sung alizaliwa mwaka 1912. Akiwa na cheo cha ukapteni jeshini alirejea kaskazini mwa nchi hiyo mwaka 1945 akiandamana na jeshi. Alipanda ngazi ya uongozi haraka na akachaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha wakomunisti wa nchi hiyo. Mwaka 1948 wakati nchi hiyo ilipoasisiwa na kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, Kim Il-sung alifikia cheo cha uwaziri mkuu.
Katika vita vya Korea, Kim Il-sung aliteuliwa kuwa kamanda mkuu wa majeshi ya nchi hiyo na mwaka 1972 akawa rais wa taifa hilo.

Tarehe 8 Julai miaka mitatu iliyopita, waziri mkuu wa zamani wa Japan, Shinzo Abe aliuawa kwa kupigwa risasi.
Shinzo Abe (安倍 晋三, Abe Shinzō) alizaliwa mnamo Septemba 21, 1954 na aliwahi kuwa Waziri Mkuu na Mwenyekiti wa Chama cha Kidemokrasia cha Liberal cha Japan kutoka 2006 hadi 2007 na kwa mara ya pili kutoka 2012 hadi 2020. Abe ndiye mwanasiasa aliyekalia kiti cha waziri mkuu wa Japan kwa muda mrefu zaidi katika historia ya nchi hiyo.
Shinzo Abe alijulikana kimataifa kwa sera za kiuchumi za serikali yake, iliyopewa jina la utani la Abenomics.
Abe aliuawa Julai 8, 2022 karibu 11:30 asubuhi wakati alipokuwa akihutubia kampeni za uchaguzi huko Nara. Abe ni waziri mkuu wa sita wa Japani kuuawa.
