Jumapili, 05 Oktoba, 2025
Leo ni Jumapili 12 Mfunguo Saba Rabiuthani 1447 Hijria ambayo inasadifiana na 5 Oktoba 2025 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1315 iliyopita, yaani tarehe 12 Mfunguo Saba Rabiuthani mwaka 132 Hijria, Abul Abbas Abdullah bin Muhammad maarufu kwa jina la 'Saffah' alikalia kiti cha uongozi akiwa khalifa wa kwanza wa kizazi cha Bani Abbasi. Utawala huo wa Kiabbasi kwa kushirikiana na Abu Muslim Khorasani na majeshi yake, ulimuuwa Marwan wa Pili, mtawala wa mwisho wa ukoo wa Bani Umayyah na kuondoa madarakani utawa wao. Bani Abbas nao kama walivyokuwa watawala wa Bani Umayyah, waliwakandamiza raia na Ahlubaiti wa Mtume Muhammad (saw) na kufanya dhulma kubwa, na utawala wao uliendelea kushika madaraka katika ulimwengu wa Kiislamu hadi mwaka 656 Hijria.

Katika siku kama ya leo miaka 161 iliyopita, alizaliwa Louis Jean Lumiere, mwanakemia mashuhuri wa Kifaransa. Mwaka 1895 akiwa pamoja na ndugu yake aliyejulikana kwa jina la Auguste Lumiere, walifanikiwa kutengeneza kifaa ambacho kiliwasaidia kuchukua picha mbalimbali na kusajili harakati. Mwaka huo huo Lumiere alifanikiwa kuonyesha filamu yake ya kwanza au Motion Picture katika majumba ya sinema. ***
Miaka 47 iliyopita katika siku kama ya leo Imam Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliondoka Iraq na kuhamia Paris, Ufaransa. Imam Khomeini aliamua kufanya hijra hiyo ya kihistoria wakati utawala wa zamani wa Iraq ulipoanza kumzuia kufanya harakati za mapambano dhidi ya utawala wa Shah. Serikali ya wakati huo ya Iraq ambayo ilikuwa ikilinda uhusiano wake na utawala wa Shah nchini Iran, ilimtaka Imam Khomeini ajiepushe na harakati zozote za kisiasa na za kimapinduzi dhidi ya utawala huo wa Shah. Hata hivyo Imam aliiambia serikali hiyo kuwa hilo lilikuwa jukumu lake la kisheria ambalo aliwajibika kulitekeleza na kusisitiza juu ya kuendelezwa mapambano kwa kutoa hotuba na kutuma kanda za kimapinduzi nchini Iran.

Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, Slobodan Milosevic dikteta wa zamani wa Yugoslavia na mhusika mkuu wa vita vya umwagaji damu huko Balkan, alijiuzulu baada ya miezi kadhaa ya malalamiko ya ndani na vikwazo vya kimataifa. Milosevic alikuwa rais wa Serbia tangu mwaka 1990 hadi 1997 na baadaye akawa Rais wa Jamhuri ya Yugoslavia. Katika vita vya Bosnia, na kwa uungaji mkono wa kila upande wa Waserbia, Slobodan Milosevic alishiriki pakubwa katika kutekeleza mauaji ya kizazi dhidi ya Waislamu wa Bosnia Herzegovina. Milosevic alikuwa kiongozi wa kwanza mtenda jinai za kivita kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa kwa ajili ya kuhukumiwa. Hata hivyo mhalifu huyo katili alifariki dunia akiwa katika korokoro za mahakama hiyo huko The Hague nchini Uholanzi kutokana na mwendo wa kinyonga wa kushughulikia kesi yake.
Tarehe 5 Oktoba ni Siku ya Kimataifa ya Mwalimu. Siku hii ilitangazwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Mwalimu katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika tarehe 3 hadi 8 mwezi Septemba mwaka 1994. Lengo la kutangazwa siku hii ni kwa ajili ya kuenzi mchango wa walimu na nafasi yao kubwa katika jamii ya mwanaadamu.
