Oct 12, 2025 02:19 UTC
  • Jumapili, 12 Oktoba, 2025

Leo ni Jumapili 19 Mfunguo Saba Rabiuthani 1447 Hijria mwafaka na 12 Oktoba 2025 Miladia.

Leo tarehe 20 mwezi wa Mehr kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, inasadifiana na maadhimisho ya kumuenzi Khaja Shamsuddin Muhammad Hafiz Shirazi, mshairi na malenga mkubwa wa Kiirani. Hafiz alizaliwa mwaka 727 Hijiria Shamsia huko Shiraz moja kati ya miji ya kusini mwa Iran. Alikuwa mtaalamu wa tafsiri ya Qur'ani, falsafa na fasihi ya Kiarabu na alipata umashuhuri kwa jina la Hafiz kutokana na kuhifadhi kwake Qur'ani Tukufu kwa visomo tofauti. Mbali na elimu hizo, Khaja Shamsuddin Muhammad Hafiz Shirazi, alikuwa mtaalamu mkubwa wa elimu ya Irfan. 

Kaburi la Hafiz Shirazi

 

Miaka 267 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Ayatullah al-Haj  Muhammad Ibrahim Khorasani, anayejulikana kama "Karbasi", mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Isfahan moja ya miji ya katikati mwa Iran. Alianza kusoma katika mji wa Isfahan na akiwa na lengo la kujiendeleza kielimu alielekea katika Chuo Kikuu (Hawza) cha Najaf Najaf, Iraq. Baada ya kurejea katika mji aliozaliwa alianza kujishughulisha na ufundishaji sambamba na kuandika vitabu. Ayatullah al-Haj  Muhammad Ibrahim Khorasani, alikuwa mashuhuri kwa taqwa, uchajimungu na kuipa mgongo dunia. Alimu huyu ameacha athari nyingi za vitabu vyenye thamani kubwa na miongoni mwavyo ni Isharaat al-Usul na Manasik al-Haj.

 

Katika siku kama ya leo miaka 212 iliyopita, kulitiwa saini mkataba wa aibu wa "Golestan" kati ya Iran na Russia. Mkataba huo ulitiwa saini kufuatia kushindwa Iran na Russia. Mkataba huu ulitiwa saini baada ya kumalizika kwa duru ya kwanza ya vita vya Iran na Russia, ambavyo vilidumu kwa miaka kumi na ulitiwa saini kwa uingiliaji kati wa serikali ya Uingereza. Kulingana na makubaliano haya, miji yote ambayo ilikuwa imechukuliwa na Russia hadi wakati huo ilibaki kuwa sehemu ya Russia, na umiliki wa Russia kwa miji ya Karabakh, Baku, Darband, Lankaran, na sehemu ya Talesh pia ulikubaliwa.

 

Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita aliaga dunia Anatole France, mwandishi wa riwaya, mwanafasihi na mwanafalsafa wa Ufaransa. Anatole France, alizaliwa katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris. Baba yyake alikuwa muuza vitabu na sehemu kubwa ya maisha ya Anatole France ilitawaliwa na vitabu. Mwaka 1921 mwandishi huyo mahiri wa Kifaransa alitunukiwa tuzo ya Nobel katika uga wa fasihi.

Anatole France

 

Tarehe 12 Oktoba miaka 26 iliyopita, Jenerali Parviz Musharraf, aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Pakistan alifanya mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu na kumuondoa madarakani Waziri Mkuu wa wakati huo wa nchi hiyo Muhammad Nawaz Sharrif. Baada ya mapinduzi hayo Musharraf ambaye alichukua madaraka ya rais wa nchi, alivifanyia mabadiliko baadhi ya vipengee vya katiba ya nchi hiyo na kuzidisha nguvu na uwezo wa rais. Hata hivyo kutokana na kuongezeka mashinikizo ya ndani na nje, Musharraf alisalimu amri mwezi Novemba 2007 na kuachia cheo cha Mkuu wa majeshi ya Pakistan. Musharraf aliondoka kikamilifu madarakani mwezi Julai 2008, baada ya kushika kasi vyama vya upinzani ambavyo vilishinda uchaguzi wa rais.  ***

Parviz Musharraf