Spoti, Agosti 14
Hujambo mpenzi msikilizaji na haswa shabiki wa masuala ya spoti na karibu nikupashe kuhusu viwanja na wachezaji ndani ya siku saba zilizopita na haswa habari kutoka Brazil kunakoendelea Olimpiki ya Rio….….karibu……..
Iran yaendelea kuzoa medali kochokocho Rio
Bingwa wa mchezo wa kunyanyua uzani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelishindia taifa hili medali ya kwanza ya dhahabu sambamba na kuvunja rekodi ya dunia katika mashindano ya Olimpiki ya Rio yanayoendelea nchini Brazil. Kianoush Rostami aliyeshiriki katika kitengo cha wenye uzito wa kilo 85, alishinda medali ya dhahabu katika mchezo wa kunyayua vyuma vizito baada ya kunyanyua uzani wa kilo 396. Medali ya fedha ilimuendea Mchina Tian Tao aliyenyanyua uzani wa kilo 395 huku raia wa Romania Gabriel Sincraian akifunga orodha ya tatu bora kwa kushinda medali ya shaba. Ushindi huo wa Rostami ulifanya bendera ya Iran ipepee mjini Rio sambamba na kupigwa wimbo wa taifa.
Muirani mwingine Sohrab Moradi aliipa nchi hii medali ya pili ya dhahabu baada ya kunyanyua uzani wa kilo 403 katika kitengo cha wanamichezo wenye kilo 95. Vadzim Straltsou wa Belarus aliibuka wa pili na kujishindia medali ya fedha kwa kunyanyua kilo 395 huku raia wa Luthuania Aurimas Didzbalis akimaliza katika nafasi ya tatu na kutwaa medali ya shaba baada ya kunyanyua kilo 392. Wakati huo huo, mwanamieleka wa Iran Saeid Morad Abdevali alijishindia medali ya shaba katika mieleka mtindo wa Greco-Roman safu ya kilo 75 baada ya kumshinda Peter Bacsi wa Hungary siku ya Jumapili.
Waislamu waeneza Uislamu sahihi Rio

Idadi kadhaa ya Waislamu nchini Brazil wamekuwa wakifanya tablighi ya dini ya Kiislamu pambizoni mwa mashindano ya Olimpiki mjini Rio de Janeiro. Duru za habari zimearifu kuwa, waumini hao wa Kiislamu nchini humo kila siku wamekuwa wakiwasili katika milango ya kuingilia kwenye viwanja kunakofanyika mashindano hayo na kufanya tablighi ya dini ya Kiislamu ambapo wamekuwa wakibainisha na kufafanua sheria za dini hiyo na kujibu maswali mbalimbali yanayoulizwa na watu. Jamila Dalima Yami, mmoja wa wanawake hao wa Kiislamu nchini Brazil amesema kuwa, tangu mashindano hayo yalipoanza amekuwa akijishughulisha na kufundisha mafundisho ya dini ya Kiislamu yeye na rafiki zake ambapo hubainisha misingi ya dini ya Uislamu kuhusiana na masuala tofauti ya ulimwengu wa leo. Yami amesema kuwa maswali juu ya vyakula halali na haramu, ndio ambayo huulizwa sana na waulizaji. Kwa mujibu wa mwanamke huyo wa Kiislamu, hadi sasa Brazil ina Waislamu wanaokaribia milioni mbili.
Kenya na Ethiopia zang'ara katika mbio za masafa marefu Rio

Jemima Jelagat Sumgong amekuwa mwanariadha wa kwanza wa Kenya kutwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya Olimpiki ya Rio. Katika siku ya 10 ya mashindano hayo Jumapili, Sumgong ambaye ni mshindi wa London Marathon aliipa fahari nchi hiyo ya Afrika Mashariki baada ya kuibuka kidedea katika mbio za nyika za kilomita 42 kwa kutumia masaa mawili, dakika 24 na sekunde 4.
Bahrain iliondoka na medali ya fedha baada ya mwanariadha wake mzaliwa wa Kenya Eunice Kirwa kuibuka wa pili huku bingwa mtetezi Mare Dibaba wa Ethiopia akiibuka wa tatu na kutwaa shaba. Huku hayo yakijiri, raia wa Ethiopia Almaz Ayana alifanikiwa kuweka rekodi ya dunia kwa upande wa wanawake katika mbio za mita elfu 10, baada ya kumaliza katika muda wa dakika 29 na sekunde 17, akivunja rekodi ya dunia ya awali iliyokuwa ya muda wa dakika 29 na sekunde 31. Ayana ameweka rekodi mpya ya dunia kwa mtindo wa aina yake haswa kwa kumpiku bingwa wa mbio hizo kwenye michezo ya Olimpiki ya London mwaka 2012, Tirunesh Dibaba aliyemaliza katika nafasi ya tatu. Mkenya Vivian Cheruiyot, alimaliza wa pili kwenye mbio hizo kwa kutumia muda wa dakika 29 na sekunde 33.
Raga: Fiji yashinda, Afrika Kusini na Kenya zaondoka kichwa chini
Timu ya taifa ya mchezo wa raga ya Fiji, yenye wachezaji saba kila upande ndio mabingwa wa raga katika michezo ya Olimpiki ya Rio kwa upande wa wanaume huku wakiwafanya wawakilishi wa bara Afrika katika michezo hiyo Kenya na Afrika Kusini ziondoke Rio kichwa chini mikono nyuma. Kikosi cha Fiji, kilijipatia medali ya dhahabu baada ya kuishinda Uingereza katika mchezo wa fainali Jumatano usiku kwa alama 43 kwa 7.
Fiji imeshinda taji hili kwa mara ya kwanza katika michezo hii ambayo pia imechezwa kwa mara ya kwanza katika historia ya Olimpiki. Wawakilishi wa Afrika, Afrika Kusini, wamemaliza katika nafasi ya tatu na kujishindia medali ya shaba baada ya kuishinda Japan kwa alama 54 kwa 14 kutafuta mshindi wa tatu. Kenya ambayo pia iliiwakilisha bara la Afrika, iliondolewa katika hatua ya makundi baada ya kushindwa katika mechi zake zote.
Judo: Raia wa Misri akataa kumpa mkono Mzayuni
Huenda mwanamichezo wa judo raia wa Misri akaadhibiwa kwa kukataa kumpa mkono mpinzani wake raia wa utawala haramu wa Israel katika mashindano ya Olimpiki yanayoendelea huko Rio de Janeiro nchini Brazil. Msemaji wa Shirikisho la Kimataifa la Judo, Nicolas Messner amesema kuwa, kitendo cha mwanamichezo Islam El Shehaby wa Misri kususia kumpa mkono Or Sasson raia wa Israel aliyekuwa mpinzani wake katika mchezo huo, kitafuatiliwa kwa lengo la kutoa adhabu dhidi yake. El Shehaby ambaye anatajwa kuwa mpinzani mkubwa dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, alisusia kumpa mkono raia huyo wa Kizayuni kutokana kwamba kufanya hivyo ni sawa na kutoa heshima kwa utawala katili wa Israel. Islam El Shehaby alikutana na Or Sasson katika mashindano ya judo ya uzani wa kilogramu 100.
Soka: Yanga yang'ara CAF
Mwakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika klabu ya Yanga, ilipata ushindi wa kwanza kwenye michuano ya CAF hatua ya makundi baada ya kuitandika Mo Beijaia ya Algeria bao 1-0 katika mechi ya marudiano iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam Jumamosi. Matokeo hayo ni kama Yanga imelipa kisasi baada ya timu hiyo kuifunga Yanga bao 1-0 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Algeria. Huo ni ushindi wa kwanza kwa Yanga tangu iingie hatua ya makundi ya michuano hiyo baada ya kupoteza mechi tatu na kutoka sare moja. Bao la Yanga katika mchuano wa Jumamosi lilifungwa katika dakika ya tatu kupitia kwa mchezaji wake Mrundi Amisi Tambwe baada ya kuunganisha mpira wa adhabu wa Juma Abdul kabla ya kutokea piga nikupige langoni mwa Bejaia na mpira kujaa wavuni. Yanga imecheza mechi tano na hivyo inasubiri kucheza mechi ya mwisho dhidi ya TP Mazembe ugenini Lubumbashi Congo DR mwishoni mwa mwezi huu. Ushindi huo umefufua matumaini kwa Yanga ambayo ilionekana kuwakatisha tamaa baadhi ya mashabiki wake kwa matokeo mabaya ya awali. Wawakilishi hao wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa bado wanaendelea kuwa mkiani mwa msimamo wa kundi A wakiwa na pointi nne huku Mazembe ikiongoza kwa kuwa na pointi 10 huku Mo Bejaia na Medeama zikishika nafasi ya pili na ya tatu kwa kuwa na pointi tano kila moja.
..............................TAMATI.....................