Aug 24, 2016 16:39 UTC
  • Usekulari Katika Mizani ya Uislamu (16)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki, ambacho lengo lake ni kuuchambua Usekulari kwa kutumia mizani ya mafundisho ya Uislamu ili kuweza kuelewa kasoro, dosari na udhaifu wa fikra na nadharia hiyo ambayo chimbuko lake ni Ulimwengu wa Magharibi. Ni mategemeo yangu kuwa mtanufaika na kuelimika na yale mtakayoyasikia katika kipindi hiki. Endeleeni kuwa pamoja nami basi kuitegea sikio sehemu hii ya 16 ya mfululizo huu.

Kwa wale mnaofuatilia kwa karibu kipindi hiki mtakuwa mngali mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tuliendelea kuufanyia uhakiki wa kiukosoaji Uliberali kuhusiana na suala la uhuru wa mtu binafsi, ukiwa ni mmoja wa misingi ya Usekulari na kubainisha kwa muhtasari mtazamo wa Uislamu kuhusu suala hilo. Na tukaahidi kuwa katika kipindi chetu cha leo tutazungumzia kwa upana zaidi uhuru wa mtu binafsi kwa mtazamo wa Uislamu.

Kama tulivyoeleza hapo kabla, moja ya sifa kuu na ya msingi iliyonayo fikra ya Uliberali ni kuufanya “uhuru” wa mtu binafsi kuwa ni tunu na thamani mutlaki, na kuipa nafasi ya mbele zaidi ya thamani nyenginezo za kiutu kama usawa, uadilifu, imani na utukufu wa kiakhlaqi. Kwa mtazamo wa Waliberali “uhuru na kujitawala mtu binafsi” kunapasa kusiwekewe mpaka wala masharti yoyote; na kila mtu, kulingana na tafsiri yake mwenyewe inapasa achague na kujiamulia kile anachokihisi kuwa ni maisha mazuri na ya saada kwake. Kwa upande mwengine, Uliberali unauchukulia uhuru wa mtu binafsi kuwa ndio ‘lengo’, na unaviweka vitu vyote katika nafasi ya kutumikia uhuru mutlaki wa mtu binafsi. Lakini kwa mtazamo wa mafundisho ya Uislamu, uhuru wa binafsi sio ‘lengo’ kwa mwanadamu bali ni ‘wenzo’ na suhula ya kufikia lengo linalolingana na hadhi na utukufu wa kiumbe huyo. Nukta nyengine muhimu ni kwamba japokuwa katika Uislamu uhuru una hadhi na nafasi ya juu, lakini si tunu na thamani ya juu kabisa, bali kuna thamani nyengine kuu za msingi kama uadilifu ambayo ina hadhi na nafasi ya juu zaidi ya uhuru. Tofauti nyengine iliyopo kuhusu uhuru wa mtu binafsi katika Uislamu na uhuru huo unavyotazamwa katika Uliberali ni kwamba katika mtazamo wa Uislamu, pamoja na mwanadamu kuwa huru lakini wakati huohuo ana mas-ulia pia; kwa hivyo ana majukumu na wajibu kwa wanadamu wenzake; na muhimu zaidi ya yote, kwa Mola na Muumba wake. Utekelezaji wa majukumu hayo una athari za moja kwa moja kwa kufuzu au kuharibikiwa kwake. Isitoshe ni kwamba Uislamu haukubaliani na uhuru mutlaki wa mtu binafsi, na kwa mtazamo wa akili yoyote timamu uhuru mutlaki wa mtu binafsi ni jambo lisilowezekana kivitendo, bali huishia kuzusha fujo na mchafukoge. Na ndiyo maana nadharia mbalimbali zina vipimo na vigezo tofauti zinavyotumia kuainisha mipaka ya uhuru wa watu.

Kuna tafsiri nyingi mno zilizotolewa kuhusu maana ya uhuru wa mtu binafsi, ambazo kwa mujibu wa wanafikra, idadi yake inafikia 200. Moja ya sababu za msingi zaidi za kuwepo tofauti za mitazamo kuhusu uhuru wa mtu binafsi, ni tofauti na hitilafu zilizopo kuhusu mtazamo juu ya ulimwengu. Ni wazi kwamba mtazamo wa kimaada kuhusu ulimwengu, ambao unamtambua mwanadamu kuwa ni kiumbe wa kimaada tu anayeanzia kwenye kuzaliwa na kuishia kwenye kifo katika dunia hii hii, hauwezi kutoa tafsiri kuhusu uhuru wa mtu binafsi ya upeo wa juu zaidi ya ulimwengu wa kimaada. Lakini kulingana na mtazamo wa kidini juu ya dunia, ulimwengu huu una kianzio na marejeo yake; na mwanadamu ni msafiri, ambaye anatoka katika ulimwengu mmoja na kuelekea kwenye ulimwengu mwengine; na wala hapotei na kutoweka kwa sababu ya kifo, bali anahama kutoka ulimwengu huu kuelekea ulimwengu mwengine. Kwa maelezo hayo, uhuru wa binafsi wa mtu katika dunia hii ya kimaada ambao ni sehemu ndogo kabisa ya maisha yake yasiyo na mpaka utakuwa na tafsiri tofauti na ya watu wenye mtazamo wa kimaada tu kuhusu mwanadamu.

Kulingana na mtazamo wa kimaada kuhusu ulimwengu, msingi wa uhuru wa mtu binafsi ni hamu na matamanio ya kimaada na matakwa ya binafsi ya mtu. Na ndiyo maana katika upembuzi wa kifalsafa na kisiasa wa Wamagharibi, nchi huonekana ina uhuru zaidi wa mtu binafsi pale watu katika nchi hiyo wanapokuwa huru zaidi kukidhi shahawa na matamanio ya nafsi. Lakini katika mtazamo wa kitauhidi kuhusu ulimwengu, unaobainishwa na Uislamu, mhimili mkuu wa ulimwengu ni Mwenyezi Mungu Mtukufu; na msingi mkuu wa uhuru wa mtu binafsi ni tauhidi. Ni Tauhidi, kwa maana ya kuamini kuwa Mwenyezi Mungu ni Mola pekee wa haki, na kukataa utawala na mamlaka ya mwengine asiyekuwa Yeye. Kwa maelezo haya, uhuru wa mtu binafsi katika Uislamu, maana yake ni mwanadamu kuwa huru na kila aina ya vizuizi isipokuwa afungike katika kuabudu na kudhihirisha uja wake kwa Mwenyezi Mungu tu. Amirul Muuminin Ali bin Abi Talib (AS) amelizungumzia jambo hilo kwa kusema:”Usiwe mtumwa wa mwengine wakati Mwenyezi Mungu amekujaalia kuwa huru”. Katika aya ya 56 ya Suratudh-Dhariyat Mwenyezi Mungu anasema:”Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.” Kwa hivyo kama ambavyo kila mwanadamu ni kiumbe huru mbele ya mwanadamu mwenzake, ni mja na mtumwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Msingi wa uhuru wa mtu binafsi katika Uislamu ni kufikia ukamilifu unaotakiwa na anaostahiki kuwa nao mwanadamu. Ukamilifu anaostahiki kuwa nao mwanadamu katika mtazamo wa Uislamu si kitu kingine isipokuwa ni kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kupata radhi zake Mola ambako humfanya mtu apate saada ya milele. Kwa mujibu wa mtazamo wa Uislamu juu ya mwanadamu, Mwenyezi Mungu ameijaalia nafsi ya mwanadamu kuwa na vipawa mbalimbali, ambapo saada ya milele ya kiumbe huyo haipatikani isipokuwa kwa kuchanua na kuvistawisha vipawa hivyo. Vipawa hivyo haviwezi kuchanua pasina mwanadamu kuwa na uhuru wa binafsi. Ni chini ya kivuli cha uhuru huo ndipo hisi za kutaka kuwa na ukamilifu, kutaka kujua haki na ukweli na kupigania uadilifu huamka na kuhuika. Shahidi Ayatullah Murtadha Mutahhari, mwanafikra mkubwa wa Kiislamu wa Kiirani amesema:” Kinyume wanavyodhani wanafalsafa wengi sana wa Magharibi, kitu ambacho ni chimbuko na msingi wa haki ya uhuru wa mtu binafsi na ambacho kinalazimu kupewa heshima si utashi, matamanio na irada ya mtu, bali ni kipawa ambacho uumbaji umempa mwanadamu kwa ajili ya kukwea daraja za utukukaji na ukamilifu.”

Fikra ya Kimagharibi inajali na kushughulikia vizuizi vya nje tu vya uhuru wa mtu binafsi. Kama vile mathalani serikali, taasisi za kijamii na mashinikizo ya nje na ya watu wengine, ili yasiweze kumbana na kumwekea mpaka mtu ya kuyafikia matakwa yake. Lakini katika Uislamu mbali na vizuizi vya nje, vinazingatiwa na kupewa umuhimu pia vizuizi vya ndani vinavyozuia uhuru wa mtu binafsi.

 Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi cha Usekulari Katika Mizani ya Uislamu, sina budi kuishia hapa kwa leo, nikiwa na matumaini kuwa mtajiunga nami tena wiki ijayo katika siku na saa kama ya leo katika sehemu nyengine ya kipindi hiki. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni heri na fanaka maishani.

Tags