Jumatatu tarehe 29 Agosti 2016
Leo ni Jumatatu tarehe 26 Dhulqaada 1437 Hijria sawa na tarehe 29 Agosti 2016.
Leo tarehe 8 Shahrivar ambayo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia imepewa jina la Siku ya Kupambana na Ugaidi. Sababu ya kupewa jina hilo ni mauaji yaliyofanywa na wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya Rais wa wakati huo wa Iran, Muhammad Ali Rajai na Waziri Mkuu Hujjatul Islam Muhammad Javad Bahonar.
Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, Muhammad Ali Rajai Rais wa wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Waziri Mkuu Hujjatul Islam Walmuslimiin Muhammad Javad Bahonar waliuawa shahidi baada ya kutokea mlipuko mkubwa wa bomu katika ofisi ya Waziri Mkuu. Jinai hiyo ya kinyama ilifanywa na kundi la kigaidi la Munafiqeen (MKO). Rajai alianza kazi ya ualimu sambamba na kushiriki kwake katika harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Shah na kuendelea katika njia hiyo hadi palipopatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, shahidi Rajai alihudumu nyadhifa za Mbunge, Waziri wa Elimu na Malezi, Waziri Mkuu na hatimaye Rais. Wakati wa kipindi cha Urais wake, Rajai alimteua Dakta Muhammad Javad Bahonar kushika wadhifa wa Waziri Mkuu. Kutokana na juhudi, bidii na ikhlasi waliyokuwa nayo katika kulihudumia taifa la Iran ili kupeleka mbele malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu, maadui wa mfumo wa Kiislamu hawakufurahishwa na utendaji wao huo na ndio maana katika tarehe kama ya leo, wakatega bomu katika ofisi ya Waziri Mkuu na kuwauwa shahidi. Imam Khomeini (MA) Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema baada ya kufa shahidi Rajai na Bahonar kuwa "thamani za mabwana hawa Rajai na Bahonar ni hizi kuwa, viongozi hao walikuwa bega kwa bega na wananchi."
Katika siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, msanii na mchoraji maarufu wa katuni wa Palestina Naji al Ali ambaye alikuwa ameshambuliwa na maajenti wa Shirika la Ujasusi la Israel MOSSAD huko London, Uingereza alifariki dunia baada ya siku 38 za kuwa katika hali ya kupoteza fahamu. Al-Ali alizaliwa mwaka 1937 huko Palestina na alilazimika kukimbia nchi yake akiwa bado mtoto akiwa pamoja na familia yake na kuishi katika kambi ya wakimbizi ya Ain al-Halwa kusini mwa Lebanon kutokana na ukatili na unyama wa Wazayuni. Alishuhudia kwa karibu mashaka na masaibu ya Wapalestina na akaamua kutumia kipawa chake cha usanii kufichua unyama na ukatili wa utawala ghasibu wa Israel kwa kutumia sanaa ya uchoraji vibonzo. Hatimaye magaidi wa Shirika la Ujasusi la Israel MOSSAD walimshambulia na kumuua mwanamapambano huyo akiwa njiani kuelekea ofisini kwake mjini London. Miezi sita baada ya kufariki kwake dunia Jumuiya ya Kimataifa ya Wachapishaji ilimtunuku msanii huyo tuzo ya Kalamu ya Dhahabu ya Uhuru.
Na siku kama ya leo miaka 67 iliyopita Urusi ya zamani ilifanya majaribio ya siri ya bomu lake la kwanza la nyuklia. Kwa utaratibu huo Urusi ikawa nchi ya pili yenye mabomu ya nyuklia baada ya Marekani suala ambalo liliibua mlingano wa nguvu kati ya nchi hizo mbili ambao ulipewa jina la “Mlingano wa Hofu.” Kwani katika hali hiyo kila mmoja wao aliogopa kutumia silaha hizo za nyuklia dhidi ya mwenzake kwa kuogopa kushambuliwa pia na silaha kama hizo. Tangu wakati huo Marekani na Urusi ya zamani ziliingia katika vita vya kipropaganda. Vita hivyo vilipewa jina la "Vita Baridi" au Cold War kwa kimombo. Vita hivyo vya kati ya kambi ya Mashariki na Magharibi viliendelea hadi wakati wa kusambaratika Urusi ya zamani mwaka 1991.