Sep 05, 2016 11:57 UTC
  • Maafa ya Mina (1)

Assalaamu Alaykum Wapenzi Wasikilizaji na karibuni katika sehemu ya kwanza ya mfululizo wa vipindi hivi maalumu vitakavyochunguza kwa kina Maafa ya Mina yaliyotokea katika msimu wa ibada ya Hija mwaka jana; ambapo maelfu ya Mahujaji wa nyumba ya Mwenyezi Mungu wakiwemo Mahujaji 464 wa Iran wakipoteza maisha katika Hija wakati wa kutekeleza ibada ya kumpiga mawe shetani katika eneo la Mina.

Tukio hilo la kuhuzunisha limeacha kumbukumbu chungu mno kwa umma wa Kiislamu kuhusiana na ibada ya Hija na wakati huo huo kuifanya serikali ya Saudi Arabia iandamwe na mashinikizo kila upande kutokana na uzembe katika kusimamia ibada hiyo. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

******

Dini Tukufu ya Kiislamu ikiwa ndio ya mwisho na kamili zaidi miongoni mwa dini za mbinguni, imeainisha ibada tofauti tofauti na zenye kutuliza roho kwa ajili ya kumfanya mwanadamu afikie ukamilifu wa kimaanawi na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Ibada hizi kila moja kati ya hizo ina adabu na taratibu zake pamoja na sifa zake maalumu ambazo huongeza mvuto na taathira ya ibada hizo. Miongoni mwa ibada zilizopo katika Uislamu ni faradhi kubwa ya kwenda kuhiji; ibada ambayo kwa hakika ina sifa za kipekee.

Tukirejea katika za 96 na 97 za Surat al-Imran tunaona jinsi Mwenyezi Mungu alivyofaradhisha ibada ya Hija.

Aya hiyo inasema: Hakika Nyumba ya kwanza walio wekewa watu kwa ibada ni ile iliyoko Bakka, iliyobarikiwa na yenye uwongofu kwa walimwengu wote. Ndani yake zipo Ishara zilizo wazi - masimamio ya Ibrahim, na mwenye kuingia humo anakuwa katika Amani. Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya kwendea. Na atakaye kanusha basi Mwenyezi Mungu si mhitaji kwa walimwengu."

Kwa msingi huo kila mtu mwenye uwezo wa kwenda kuhiji, basi faradhi hii kwake ni wajibu mara moja katika kipindi chote cha uhai wake. Kwa maana kwamba, Ni wajibu kwa kila Mwislamu mwenye uwezo kwenda kuhiji Makka mara moja katika umri wake. Kufanya hivyo mja huyu atakuwa amepiga hatua moja muhimu mno kuelekea katika kujijenga na kupata ukamilifu wa kiroho. Tunaona kuna watu wengi ambao baada ya kurejea kutoka katika safari ya kimaanawi ya ibada ya Hija, maisha yao yalibadilika kabisa na hata njia ya maisha yao nayo ilibadilika na ikaonekana kuboreka zaidi kuelekea umaanawi na uchaji Mungu zaidi.

Pamoja na hayo, marasimu ya ibada ya Hija yana sifa zake za kuvutia ambapo sifa yake ya kwanza kubwa ni kufanyika ibada hiyo kwa pamoja na kwa sura ya mkusanyiko. Katika ibada hiyo, mamia ya maelfu kwa maelfu ya Waislamu kutoka pembe mbalimbali duniani hushiriki ibada ya Hija kwa pamoja na kutekeleza matendo na amali zao pia kwa pamoja bila kujali sura, rangi au utaifa wao. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei anasema katika moja ya jumbe zake kwa Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu akitoa taswira na mandhari ya Hija kwamba: "Macho yanayobubujika machozi hupata maliwazo kwenye Haram ya Mtume adhimu wa shani SAW, Mawalii wa Mwenyezi Mungu AS na mujahidina wa Uislamu ; (huwa ni marejeo) ya nyoyo zinazoangaziwa na nuru katika anga ya kimaanawi ya Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu na Haram Tukufu ya Mtume Mtukufu."

Jukumu la mauji yote haya ya watu wasio na hatia abebeshwe nani?

 

Sifa ya pili ya Hija ni kufanyika ibada hiyo sehemu moja na maeneo matakatifu kama Masjidul Haraam, Arafa, Mash'ar al-Haraam na Mina. Aidha sifa ya tatu ni kwamba, ibada ya Hija hufanyika katika kipindi maalumu ndani ya Mfunguo Tatu Dhul Hijja. Kwa msingi huo, Mwenyezi Mungu alitaka watu kutoka nchi, mataifa na kaumu mbalimbali wakusanyike katika mji wa Makka na viunga vyake katika kipindi maalumu na kisha watekeleze kwa sura ya pamoja marasimu ya ibada ya Hija.

Aya ya 27 hadi ya 29 za Surat al-Hajj zinasema:

Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliye konda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali.  Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jina la Mwenyezi Mungu katika siku maalumu juu ya wanyama hawa aliowaruzuku. Basi kuleni katika hao na mlisheni mwenye shida aliye fakiri.

Hata hivyo kama ilivyokuja katika aya ya 97 ya Surat al-Imran na hadithi mbalimbali ni kuwa, ibada ya Hija sio wajibu kwa Waislamu wote bali kwa wale tu ambao wametimiza masharti na wana uwezo. Maulama na mafakihi wa Kiislamu kawaida hudhukuru na kutaja vitu kadhaa kwa anuani ya istitwaa yaani uwezo wa mtu anayetaka kwenda kuhiji. Mosi, anayetaka kwenda kuhiji anapaswa kuwa na uwezo wa kimwili yaani kiafya na kama hana uwezo huo basi anaweza kumtuma mtu akamhijie. Pili, uwezo wa kifedha. Kwa hakika, hili nalo ni sharti la pili kwa mtu anayetaka kwenda kutekeleza faradhi ya Hija. Kwa maana kwamba, mtu anayetaka kwenda kuhiji anapaswa kuwa na uwezo wa kifedha wa kujidhaminia safari yake ambapo katika zama zetu hizi ni kama vile tiketi, visa, hoteli, masurufu na mengineyo na vilevile aiachie familia yake fedha za matumizi kwa ajili ya siku ambazo yeye atakuwa Hija. Hata hivyo moja ya masharti muhimu ya Hija yanayoingia katika mjumuiko wa uwezo ni suala la usalama.

Kwa maana kwamba, hujaji anapaswa kuwa na amani na utulivu unaohitajika anapokuwa katika Nyumba ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Hija.

Kuna watu wanataka maafa haya yasahauliwe, yapitwe vivi hivi bila ya kuuliza chochote, huo ni uadilifu?

 

Hapo zamani, kusudio la usalama zaidi lilikuwa ni kutokuweko hatari katika njia ya kuelekea Makka; kwani katika zama hizo watu walikuwa wakisafiri kwa kutumia vipando vya wanyama kama ngamia, punda, farasi na kadhalika na kutumia siku nyingi wakiwa njiani wakipita mila na mabonde, misitu na hata nyika. Wakati mwingine njiani walikuwa wakikabiliwa na wezi wanaofunga njia na hivyo mali na roho zao kuwa hatarini. Lakini hii leo, takribani hatari hiyo haipo, kwani safari zinafanyika kwa usafiri wa ndege au vyiombo vingine vya usafiri ambavyo ni vya haraka na hivyo kutumia muda mchache mno. Hivyo basi kile kinachozungumziwa hii leo kuhusiana na usalama wa Mahujaji ni Amani, usalama na utulivu wao wakiwa Makka na Madina. Licha ya kuwa katika Uislamu kuna ibada nyingine zinazofanyika kwa sura ya pamoja au ya jamaa kama Swala ya Ijumaa na Swala nyingine za faradhi, lakini ibada ya Hija inahesabiwa kuwa ibada kubwa yenye mkusanyika mkubwa zaidi katika Uislamu. Hapana shaka kuwa, ili kuhakikisha kwamba, mamia ya maelfu ya Mahujaji wakiwa pamoja, katika eneo moja na kwa wakati mmoja wanaweza kutekeleza ibada ya Hija ni lazima wawe na usalama wa roho zao. Kudhamini usalama wao ni jukumu ambalo liko mikononi mwa wasimamizi wa ibada ya Hija yaani serikali ya Saudi Arabia ambayo kimsingi ndio inayosimamia haramu mbili tukufu za Makka na Madina.

Hata hivyo katika miaka ambayo utawala wa Aal Saud umekuwa ukitawala katika ardhi ya Hijaz, viongozi wake hawajaweza kudhamini inavyotakiwa usalama wa Mahujaji. Watawala wa Saudia wakitumia pato linalotokana na mauzo ya mafuta wamezipanua haram mbili za Makka na Madina. Hilo limefanyika kwa kubomoa majengo ya kihistoria ya Kiislamu katika miji hiyo miwili. Watawala hao wameshindwa kabisa kudhamini usalama na roho za Mahujaji katika kipindi cha siku chache wanazokuwa nchini hunmo kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Hija. Hii ni katika hali ambayo, kupatikana maendeleo makubwa katika uga wa elimu na teknolojia hususan katika uwanja wa mawasiliano, vikosi vya usalama na jeshi la polisi na kwa kutumia vifaa na suhula mpya na za kisasa inawezekana kuzuia matukio machungu au kupunguza maafa ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika msimu wa Hija na kuzijeruhi nyoyo za Waislamu kutokana na Mahujaji kupoteza maisha yao. Kutokea matukio ya kuhuzinisha na ya kutia simanzi katika miaka ya hivi karibuni na kusababisha Mahujaji kuaga dunia ni mambo yanayoonesha kwamba, Saudia haina sifa na ustahiki wa kusimamia usalama wa Mahujaji.

Sehemu ijayo ya kipindi hiki itatoa mifano ya matukio hayo ili msikilize aweze kutoa hukumu.

 

Kwa maelezo zaidi kuhusu Maafa ya Mina: http://kiswahili.irib.ir/habari/mina

Kwa maelezo zaidi kuhusu makala za Hija: http://kiswahili.irib.ir/uislamu/hija

 

Tags