Sep 09, 2016 13:55 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (141)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza sehemu nyingine ya kipindi cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kinakujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tunaendelea kuzungumzia swali ambalo tumekuwa tukilijadili katika vipindi kadhaa vilivyopita kuhusiana na siri ya Mtume Mtukufu (saw) kusisitiza na kubana uongofu wa Waislamu na wanadamu wote kwa ujumla pamoja na kuwaepusha na upotovu katika kushikamana kwao kwa wakati mmoja na Qur’ani Tukufu pamoja a Ahlul Beit wake (as) kama ilivyopokelewa katika hadithi mashuhuri ya Thaqalain. Tuliona kwamba hadithi hii kwa hakika ni tafsiri na ufafanuzi wa Mtume Mtukufu (saw) kuhusiana na aya nyingi ambazo zinasema kwamba kushikamana kwa kweli na Qur’ai Tukufu hakutimii ila kwa kushikama na Ahlul Beit watoharifu wa Mtume Mtukufu (saw).

Katika kipindi cha leo tutazungumzia aya nyinginezo ambazo zinazungumzia suala hilo ikiwemo ya 89 ya Surat an-Nahl ambayo inasema wazi kwamba Qur’ani Tukufu ni kitabu ambacho kinabainisha wazi kila jambo. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika aya hiyo: Na siku tutakapomuinua shahidi katika kila umma akiwashuhudia kwa yanayotokana na wao, na tutakuleta wewe uwe shahidi juu ya hao. Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinachobainisha kila kitu, na ni uwongofu, na rehema, na bishara kwa Waislamu.

Je, aya hii inatuongoza vipi kujibu siri ya kubanwa uongofu wa Waislamu na kuwaepusha na upotovu katika kushikamana vilivyo na Vizito Viwili, yaani Qur’ani Tukufu na Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw)? Hili ndilo jambo tutakalolijadili hivi punde, karibuni.

 

Ndugu wasikilizaji, tunaona kwamba aya hii inazungumzia ushuhuda wa Mtume Mtukufu (saw) kwa umma wake au kwa mashahidi wa umma nyinginezo kwa upande mmoja na kuzungumzia kuteremshwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu ambacho kinabainisha kila jambo kwa upande wa pili. Kwa kuzingatia hayo ni kitu gani tunachonufaika nacho kutokana na aya hii?

Ili kupata jibu la swali hili tunakirejea kitabu hikihiki kitakatifu chenyewe ambapo tunapata kwamba kinasema wazi kuwa aliyeteremshiwa kitabi hicho ndiye anayefaa kuwa shahidi juu ya watu. MwenyezI Mungu anasema mwishoni mwa aya ya ar-Ra’d: Na waliokufuru wanasema: Wewe hukutumwa. Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi, na pia yule mwenye ilimu ya Kitabu.

Ushuhuda alioujalia Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake (saw) Mtukufu na walio na elimu juu ya watu, kwa hakika ndio ushuhuda wa haki na halisi na ambao hauhusiani na dhahiri ya watu na matendo yao. Ushuhuda huu ni katika miujiza ya Mwenyezi Mungu ambayo huwathibitishia wanadamu kupitia kwayo kwamba Mitume wametumwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe. Ni wazi kwamba ushuhuda wa aina hii unamlazimu shahidi kuwa na habari kuhusiana na batini ya watu na nia za matendo yao kwa sababu amali na matendo hufungamana na nia. Kwa hivyo shahidi hupata wapi uwezo huu wa kuweza kubaini matendo na nia za watu?

Aya tuliyosoma katika Surat ar-Ra’d inasema wazi kwamba shahidi hupata uwezo huo kutokana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu chenyewe kwa sababu kina ufafanuzi wa kila kitu kama tulivyoona hilo katika aya ya Surat an-Nahl. Na hii ina maana kwamba lafudhi na matashi ya mambo yanayozungumziwa katika kitabu hicho cha mbinguni hayahusiani na masuala ya dhahiri tu bali ndani yake kuna mambo ambayo yalimuwezesha wasii wa Nabii Suleiman (as) kuweza kuleta kiti cha enzi cha Balqis kutoka Yemen hadi Sham kabla ya kupepesa jicho la Nabii huyo. Hii ni kwa sababu wasii huyo alikuwa na elimu ya sehemu ndogo tu ya Kitabu kama inavyobainisha wazi hilo aya ya 40 ya Surat an-Naml. Basi itakuwaje kwa mtu ambaye ana elimu ya kitabu hicho chote na sio sehemu tu ya kitabu hicho kama ilivyokuwa kuhusiana na wasii wa Nabii Suleiman (as)?

*******

Ndugu wasikilizaji, ukweli huu unaashiriwa na aya nyingi za Qur’ani Tukufu ambapo iliyo wazi zaidi kuhusiana na batini ya kitabu hiki kitakatifu ambayo inamuwezesha mtu aliyepewa elimu yake uwezo wa kuweza kubaini yaliyomo kwenye nia na nyoyo za watu, ni aya ya 31 ya Surat ar-Ra’d ambayo inasema: Na kama ingelikuwa Qur'ani ndiyo inayoendeshewa milima, na kupasuliwa ardhi, na kusemeshewa wafu, (wasingeliamini). Bali mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu.

Imam Abul Hassan Musa al-Kadhim (as) ameitolea hoja aya hii maana tuliyoashiria katika hadithi iliyonukuliwa katika vitabu vya al-Kafi, Baswair ad-Darajaat na vitabu vinginevyo. Katika hadithi hii Imam anazungumzia kukusanyika kwa elimu na miujiza ya Manabii wote wa zamani katika Mtume Mtukufu (saw). Alisoma aya hii tuliyoinukuu na kisha kusema: ‘Na sisi tuliirithi Qur’ani hii ambamo kuna mambo yanayoendeshewa milima, kupasuliwa ardhi na kuhuishwa mauti. Na sisi tunajua maji yaliyo chini ya hewa. Hakika kwenye Kitabu hiki cha Mwenyezi Mungu kuna aya ambazo jambo haliombwi kupitia kwazo ila hujibiwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, mbali na kuwa kwenye Mama wa Kitabu, Mwenyezi Mungu ametupa yale yote aliyoruhusu na kuwapa Mitume wote wa zamani. Mwenyezi Mungu anasema: Na hakuna siri katika mbingu na ardhi ila imo katika Kitabu kinachobainisha. Kisha akasema: Kisha tumewarithisha Kitabu wale ambao tumewateuwa miongoni mwa waja Wetu. Na sisi ndio tulioteuliwa na Mwenyezi Mungu na kurithishwa (kitabu) hiki ambacho ndani yake kuna mambo yanayobainisha kila kitu.’

Na katika hadithi nyingine ambayo imenukuliwa na vitabu hivi, Imam Swadiq (as) alizungumzia elimu yao inayogusia masuala ya ghaiba jambo ambalo lilimshangaza sana mpokezi wa hadithi hii ambaye ni Hamaad al-Lahham kuhusiana na ukubwa na upana wa elimu hiyo. Imam (as) alimbainishia chanzo chake kwa kusema: ‘Ewe Hamaad! Hakika yote haya yamo kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu, hakika yote haya yamo kwenye Kiatabu cha Mwenyezi Mungu, hakika yote haya yamo kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu (aliyasema hayo mara tatu). Kisha alisoma aya hii: Na siku tutakapomuinua shahidi katika kila umma akiwashuhudia kwa yanayotokana na wao, na tutakuleta wewe uwe shahidi juu ya hao. Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinachobainisha kila kitu, na ni uwongofu, na rehema, na bishara kwa Waislamu. Kisha akasema: Hakika haya ni katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu ambamo ndani yake kuna ubainishaji wa kila kitu, ndani yake kuna ubainshaji wa kila kitu.’

Image Caption

 

Ndugu wasikilizaji, katika vipindi vilivyopita tulizungumzia hadithi sahihi tukufu ambazo zinabainisha wazi kwamba wale waliopewa elimu ya Kitabu chote ni Ahlul Beit wa Mtume (as) ambao Mtume Mwenyewe (saw) aliwafungamanisha na Qur’ani Tukufu na kusema kuwa hawatatengana na Kitabu hicho wala kitabu hicho cha mbinguni kutengana nao (as).

Kwa msingi huo natija ya somo la leo ni kwamba kunufaika na rehema pamoja na baraka nyingi za Qur’ani Tukufu ambayo inabainisha kila jambo kunafungamana moja kwa moja na kufuatwa pamoja na kushikamana kilamilifu na watukufu walio na elimu ya kitabu hiki chote cha Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambapo miongoni mwa baraka hizo ni kufafanuliwa na kuwekwa wazi njia za uongofu dhidi ya upotovu wa kila aina. Ni kutokana na ukweli huo ndipo Mtume Mtukufu (saw) akabana njia ya uongofu dhidi ya upotovu kwa kushikamana kikamilifu na kwa pamoja na Vizito Viwili, ambavyo ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu ambayo ni Qur’ani Tukufu na Ahlul Beit maasumu wa Mtume (as). Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe taufiki ya kushikamana na vitu viwili hivi kwa pamoja bila ya kufadhilisha kimoja juu ya kingine.

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho mmekisikiliza kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu kutoka hapa mjini Tehran. Basi hadi wakati mwingine, panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.