Familia Salama (8)
Makala hizi huangazia masuala mbali mbali ya afya ya familia kama vile lishe, mazoezi, madhara ya matumizi ya mihadarati, umuhimu wa mahaba katika familia n.k. Katika makala ya leo tutaangazia vijana na changamaoto wanazokumbana nazo maishani. Karibuni kujiunga nasi hadi mwisho.
Pengo au mwanya kati ya vizazi ni kati ya changamoto kuu na muhimu za familia. Vijana wa leo wanamiliki suhula zilizostawi za kiteknolojia na hivyo wana uwezo wa kufahamu mambo mengi kwa wakati mfupi ikilinganishwa na vizazi vilivyotangulia.
Kinyume na zama zilizopita, katika zama hizi, familia, mila na desturi za jadi sio chanzo pekee cha mtu kujua maisha, uhusiano wa kijamii n.k.
Hivi sasa, teknolojia ya habari na mawasiliano imepelekea familia kubadilika kiasi cha kuathiri vibaya familia na mila na desturi za kale.
Katika upande mwingine, katika dunia ya sasa, mwanadamu anakumbwa na wimbi kubwa la utumizi bidhaa kupita kiasi au consumerism.
Maslahi ya uchumi wa kibepari hufikiwa kupitia njia mbali mbali kama vile kuhimiza mitindo na matangazo ya kibiashara ya kutumia bidhaa kwa wingi sambamba na maisha ya anasa.
Kizazi kipya kinaibuka na matarajio mapya ambayo yasipodhibitiwa hupelekea vijana kukasirika na jambo hilo huzidisha pengo baina ya vizazi na hivyo kuibuka msuguano wenye madhara kwa pande zote.
Baadhi ya wakati, wazazi ima kwa makusudi au kwa kutojua, hupuuza tafauti za umri baina yao na watoto wao. Wazazi husahau kuwa watoto wanaishi katika zama tafauti na zao.
Wao hujaribu kuwalazimu watoto kuwatazama kama kigezo na kuishi walivyoishi katika zama zilizopita. Hii ni katika hali ambayo kila kizazi kina mtindo wake wa maisha. Pamoja na hayo, watoto au kizazi kipya hakipaswi kusahau kuwa ushauri na muongozo wa wazazi ni muhimu na kamwe haupaswi kupuuzwa.
Iwapo kizazi cha sasa kitakosa au kupuuza ushauri na muongozo wa vizazi vilivyotangulia basi kizazi hiki kitatumbukia katika kinamasi na masaibu.
Katika upande wa pili, wazee na wazazi nao wanapaswa kukubali kuwa vijana ndio wanaopelekea jamii kustawi na kuendelea. Kwa hivyo, iwapo vijana watakuwa na nguvu na uwezo unaofaa, jamii nayo itaweza kupiga hatua za maendeleo. Kwa msingi huo wazee wanapaswa kuzingatia kuhusu namna ya kuwapa vijana uzoefu wao wenye thamani.
Ili wazazi waweze kukabiliana kimantiki na kadhia ya vijana wa kizazi kipya, kunapaswa kuwepo utamaduni wa mazungumzo, ustahamilivu, uwezo wa kupokea na kukubali mabadiliko.
Pengo kati ya vizazi hugeuka na kuwa mgogoro na tishio wakati kunaibuka mvutano baina ya vizazi na hilo huandamana na kuwepo thamani tafauti na mila na desturi zinazokinzana kabisa na jambo hilo kupelekea kutoweka mawasiliano na maingiliano baina ya vizazi.
Wazee na hasa wazazi wanapaswa kutambua hali ya zama tofauti katika jamii ili sambamba na kulinda pamoja na kuhifadhi misingi ya thamani za kibinadamu, waruhusu watoto waendeleze harakati zao maadamu hilo linfanyika kwa msingi wa sheria za kidini na nchi.
Iwapo mafundisho ya kidini yatapuuzwa na watoto kukosa mafundisho ya kidini hatua kwa hatua katika umri wao, basi jambo hilo litapelekea kuibuka tatizo katika maingiliano ya kifamilia na kijamii na hilo litapelekea kuibuka mpasuko na maporomoko ya kimaadili na kiutamaduni.
Kutokana na ustawi wa kasi wa teknolojia ya habari na mawasiliano au technohama, wazazi wanapaswa pia kuenda sambamba na kasi hiyo kwa kujielimisha kuhusu mapya ya ulimwengu wa teknolojia. Kwa njia hii, wataweza kuwaongoza watoto wao na pia kuwasimamia ili wasitumbukie katika maovu yaliyo katika teknolojia mpya ya habari na mawasiliano. Iwapo wazazi ua wazee watafahamu na kudiriki mahitaji ya kizazi cha sasa pamoja na mabadiliko yanayojiri katika uga wa teknolojia ya habari na mawasiliano, basi wataweza kudiriki mahitajio ya watoto na kizazi cha sasa na kuwasaidia katika dunia hii iliyojaa vishawishi vingi.
Moja ya vyanzo vikuu vya kuvurugika na kusambaratika mshikamano katika familia ni utumizi wa kufurutu ada wa vyombo vya habari na mawasiliano hasa mitandao ya kijamii.
Ingawa mabarobaro hupata na kuimarisha maarifa na elimu yao kupitia intaneti sambamba na kuzijua staarabu na tamaduni mbali mbali kutokana na kutokuwepo mipaka ya kijiografia katika intaneti, lakini utumizi usio sahihi wa teknolojia ya habari na mawasiliano au technohama huwa na matokeo mabaya na hatari sana. Ukweli ni kuwa katika dunia yetu ya leo, intaneti imeweza kujipenyeza katika nyumba zetu na katika maisha binafsi na kuwa na taathira isiyoweza kuaminika katika thamani na itikadi za wanaoitumia.
Mitandao hii ya kijamii hatua kwa hatua inachukua nafasi ya mawasiliano ya moja kwa moja baina ya wanadamu. Siku hizi mawasiliano ya uso kwa uso yamekuwa machache yakilinganishwa na mawasiliano ya kimaandishi au kwa sauti kupitia mitandao ya kijamii. Natija ya hili ni kuwa watu katika familia moja badala ya kuwa na mazungumzo yenye mahaba baina yao, hutumia vyombo vya mawasiliano ya kieletroniki kuwasiliana. Aina hii ya mawasiliano hatua kwa hatua huondoa ukuruba na ukarimu baina ya wanadamu.
Familia bora na salama ni ile ambayo, wazazi, watoto, mabarobaro na vijana huwa na uhusiano wa karibu na wa ana kwa ana wenye kuleta ukuraba, mahaba na utulivu wa kiroho.
Mbali na wazazi na wazee, taasisi za elimu, vyuo vikuu na vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika ustawi wa mwanadamu katika sayansi na teknolojia. Vinaweza pia kuwa na mchango mkubwa katika ubunifu katika uga wa fikra, elimu na teknolojia ili kwa njia hiyo kupunguza pengo lililopo kati ya vizazi.
Wapenzi wasikilizaji makala yetu inafikia tamati hapa kwa leo, lakini, panapo majaliwa yake Mola, msikose kujiunga nasi katika kipindi chetu kijacho ambapo tutajadili umuhimu wa kusoma vitabu katika familia. Shukran kwa kuwa nasi.