Oct 24, 2016 06:57 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Okt 24

Iran yaibuka ya 2 Kombe la Dunia mchezo wa Kabaddi; Mau U wachezea mkong'oto Stamford Bridge na Sundowns yatwaa Kombe la Klabu Bingwa Afrika.

Kabaddi: Iran yaibuka ya 2 Kombe la Dunia

Timu ya taifa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya mchezo wa kabaddi imeibuka ya pili katika mashindano ya Kombe la Dunia ya mchezo huo, baada ya kushindwa kufurukuta mbele ya mwenyeji India. India ilizoa jumla ya alama 38 dhidi ya 29 zilizokusanywa na vijana wa Iran. Iran ilijikuta inakabiliwa na kibarua kigumu katika fainali hiyo kutokana na ukweli kwamba, India ndiyo nchi yenye timu bora zaidi ya mchezo wa kabaddi duniani na ambayo ipo katika madaftari ya kumbukumbu kwa kutwaa mataji yote ya Kombe la Dunia ya mchezo huo.

Iran ilitinga fainali baada ya kuigaragaza Japan pointi 38-34 katika mchezo uliopigwa katika ukumbi wa TransStadia mjini Ahmadabad nchini India, ikiwa ni muendelezo wa rekodi ya kutoshindwa katika mchezo huo tangu mashindano hayo yaanze Oktoba 7.

Sarah Javanmardi

Mwanadada wa Iran ateuliwa Mwanamichezo Bora Duniani

Sarah Javanmardi kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametawazwa kuwa mwanariadha bora wa kike duniani mwezi Septemba mwaka huu. Mwanamichezo huyo wa kike wa Iran ametunukiwa Tuzo ya Allianz ya Mwanariadha Bora wa Kike ya Kamati ya Kimataifa ya Paralimpiki IPC baada ya kushiriki katika michezo ya walemavu ya Paralimipiki, Rio 2016 kitengo cha ulengaji shabaha kwa bastola. Alipata dhahabu mbili katika kategoria za Bastola ya Mita 10 SH1 na Bastola ya Mita 50 SH1. Tuzo hiyo ya Javanmardi mwenye umri wa miaka 31 inakamilisha ushindi maradufu wa Iran baada ya bingwa wa mchezo wa kunyayua uzani (vyuma vizito) wa Jamhuri ya Kislamu ya Iran, Siamand Rahman kuteuliwa kuwa mwanariadha bora wa kiume duniani katika orodha ya mwezi Septemba mwaka huu na Kamati ya Kimataifa ya Paralimpiki IPC. Rahman wa Iran alivunja rekodi ya dunia na kushinda medali ya dhahabu katika Mashindano ya Olimpiki ya Walemavu ya Rio Septemba 14 mwaka huu. Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 28 alinyanyua uzani wa kilo 270 katika kategoria ya wanariadha walemavu wenye kilo zaidi ya 107 na kuvunja rekodi dunia kwenye mashindano hayo.

Sundowns watwaa Kombe la Klabu Bingwa Afrika

Licha ya kutandikwa bao 1-0, timu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini imetwaa Kombe la Klabu Bingwa barani Afrika kwa mara ya kwanza baada ya kuishinda Zamalek ya jumla ya mabao 3-1. Katika kipute cha fainali kilichopigwa mbele ya mashabiki zaidi ya 80,000 katika uwanja wa Burj al-Arab mjini Alexandria Jumapili, Zamalek walipata ushindi wa bao 1-0, ushindi hafifu ambao usingwewafanya waibuke kidedea, kutoka na ukweli mchungu kuwa, walikuwa wamelazwa mabao 3-0 na Sundowns katika mechi ya kwanza mjini Atteridgeville Jumamosi ya Oktoba 15. Bao tasa la Zamalek lilitiwa kimyani na kiungo Stanley Ohawuchi kunako dakika ya 62.

Droo ya AFCON 2017

Kwengineko Droo ya Kombe la Mataifa ya Afrika ilifanyika Jumatano ya Oktoba 19 katika mji wa Libreville, nchini Gabon. Gabon, ambayo itakua mwenyeji wa michuano hii itakuwa kibarua kigumu kwa kukabiliana na Burkina Faso, Cameroon na Guinea-Bissau katika michuano hii ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2017). Mechi ya ufunguzi itakua kati ya Gabon, mwenyeji na Guinea-Bissau Januari 14, 2017. Kundi A inaundwa na Gabon, Burkina Faso, Cameroon, Guinea-Bissau. Kundi B inazijumuisha Algeria, Tunisia, Senegal na Zimbabwe. Kundi C linaundwa na Kodivaa, DRC, Morocco na Togo. Kundi D linazileta pamoja Ghana, Mali, Misri na Uganda. Duru ya 31 ya Kombe la Mataifa ya Afrika itaanza Januari 14 hadi Februari 5 mwakani nchini Gabon.

Ligi ya EPL

Wachezaji wa timu za EPL

Klabu ya Machester United imepokea kichapo cha mbwa kutoka Chelsea katika mchuano mwingine wa kukata na shoka wa Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza. Ilikuwa ni fedheha kwa Jose Mourinho ambaye alikuwa anarudi ugani Stamford Bridge kama mkufunzi wa Mashetani Wekundu. The Blues ambao walimpiga kalamu Jose Mourinho Disemba mwaka uliopita, walifungua mvua ya mabao sekunde 30 baada ya kupulizwa kipenga cha kuanza mchezo kupitia mchezaji Pedro, hilo likiwa bao la mapema zaidi kuwahi kufungwa tangu msimu uanze. Gary Cahill alifunga bao la pili katika kipindi cha pili huku kiungo Eden Hazard akiongeza la tatu ma kuzima matumaini ya Mashetani Wekundu. N'golo Kante alipiga msumari wa mwisho kwenye jeneza la vijana vijana Mourinho na kuwafanya wasalie katika nafasi ya 7 huku pengo kati yao na viongozi wa ligi likiongezeka na kufikia pointi tano. Hii ni mara ya 51 kwa Man United kufungwa na Chelsea, licha ya kuwa Mashetani Wekundu wanaongoza katika rekodi ya kuwafunga The Blues mara 75.  Kwengineko viongozi wa Ligi Manchester City walitoka sare ya 1-1 na Southampton katika uwanja wa Etihad. Liverpool iliilaza West Brom mabao 2-1 wakati ambapo Arsenal walikuwa wanalazimishwa sare ya 0-0 na Middlesbrough. Mabingwa watetezi Leicester City waliwachachawiza Crystal Palace mabao 3-1 huku vijana wa Hull City wakikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa vijana wa jiji la Stoke. Kwa sasa Man City, Gunners na Liverpool wanabanana kileleni mwa ligi ya Premier wote wakiwa na alama 20 ingawaje wanatofautiana kwa mabao. Chelsea na Tottenham wanashikilia nafasi ya nne na tano kwa utaratibu huo wkaiwa na alama 19.

....................................TAMATI................................