Oct 27, 2016 05:46 UTC
  • Alkhamisi, 27 Oktoba, 2016

Leo ni Alkhamisi tarehe 25 Muharram 1438 Hijria sawa na Oktoba 27, 2016.

Siku kama ya leo miaka 1343 iliyopita, yaani sawa na tarehe 25 Muharram mwaka 95 Hijiria, kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, alikufa shahidi mjini Madina akiwa na umri wa miaka 38, Imam Ali bin Hussein, maarufu kwa lakabu ya Imam Sajjad au Imam Zainul-Abidin, mtoto wa Imam Hussein (as) na mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw). Baada ya mapambano makubwa ya baba yake katika jangwa la Karbala, Iraq Imam Sajjad alikuwa na jukumu zito la kufikisha ujumbe na malengo ya baba yake Imam Hussein (as). Imam Sajjad alifanya juhudi kubwa za kufundisha utamaduni wa Kiislamu na kueneza mafundisho bora ya Qur'ani na suna za Mtukufu Mtume Muhammad (saw) jambo ambalo lilikuwa sababu ya kubakishwa hai Qur'ani na suna hizo za Mtume. Imam Zainul-Abidin alikuwa mashuhuri kwa ucha-Mungu ambapo na alikuwa akisujudu sana kwa ajili ya Mola Muumba na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya 'Sajjad' ikiwa na maana ya mtu mwenye kusujudu sana.

Imam Zainul Abidin (as)

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita Imam Ruhullah Khomeini alipinga vikali mpango wa mfalme wa zamani wa Saudi Arabia, Fahad bin Abdul Aziz kuhusu mapatano ya Palestina na Israel. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na baada ya kutiwa saini mkataba wa Camp David baina ya serikali ya Misri na utawala ghasibu wa Israel chini ya upatanishi wa Marekani, tawala vibara za Kiarabu zilifuata nyayo za utawala wa Misri katika suala hilo. Wakati huo Fahad bin Abdul Aziz aliyekuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, alitoa pendekezo la kutambuliwa rasmi utawala wa vamizi wa Israel, suala ambalo lilikabiliwa na upinzani mkali wa Waislamu kote duniani. Kwa msingi huo katika siku kama hii ya leo Imam Ruhullah Khomeini alitoa hotuba akisema: "Ni wajibu kwetu sisi na kwa kila Mwislamu kupinga mipango kama ule uliopendekezwa na Fahad. Tunawajibika kulaani mipango kama hii isiyokuwa na faida kwa watu wanaodhulumiwa. Jambo hatari sana kwa sasa ni makubaliano ya Camp David na mpango wa Fahad ambayo inaimarisha zaidi Israel na kudumisha jiani zake." Upinzani huo wa wazi wa Imam Khomeini na uungaji mkono wa Waislamu kote dunia kwa misimamo hiyo ya Imam ilikuwa sababu ya kukataliwa na kupingwa pendekezo hilo katika nchi nyingine. 

Imam Ruhullah Khomeini

Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita nchi ya Norway ilivunja muungano wake na Sweden na kujitangazia uhuru. Kabla ya karne ya 14 Norway ilikuwa nchi yenye ushawishi na moja ya madola vamizi. Hata hivyo mnamo mwaka 1380 ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Denmark na kuendelea kuwa chini ya udhibiti wa nchi hiyo kwa muda wa karne 4.

Bendera ya Norway

Miaka 106 iliyopita katika siku kama leo, baada ya Japan kupigana vita na nchi mbili za China na Russia kwa miaka kadhaa na kupata ushindi katika vita hivyo, iliunganisha rasmi ardhi ya Korea na ardhi yake. Korea iliendelea kuwa chini ya udhibiti wa Japan hadi mwaka 1945 wakati Japan iliposhindwa katika Vita vya Pili vya Dunia.

Korea Kaskazni na Korea Kusini

Na tarehe 25 Muharram miaka 185 iliyopita, lilichapishwa gazeti la kwanza la Iran lililojulikana kwa jina la Kaghaze Akhbar. Gazeti hilo lilichapishwa na Mirza Swaleh Shirazi mjini Tehran, likiwa na kurasa mbili kubwa. Gazeti hilo lilikuwa likichapishwa mara moja kwa mwezi na lilizungumzia habari za Tehran na miji mingine ya Iran, nchi za Kiarabu na Uturuki.

Nakala pekee iliyobakia ya gazeti hilo imehifadhiwa kwenye jumba la makumbusho la Uingereza.

Kaghaze Akhbar.

 

Tags