Familia Salama (18)
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika mfululizo huu wa makala kuhusu Familia salama. Makala hizi huangazia masuala mbali mbali ya afya ya familia kama vile lishe, mazoezi, madhara ya matumizi ya mihadarati, umuhimu wa mahaba katika familia n.k. Katika makala ya leo tutaangazia suala la kustaafu wafanyakazi. Karibuni kujiunga nasi hadi mwisho.
Zama za kustaafu zina umuhimu mkubwa sawa na zama zingine katika maisha ya mwanadamu na kwa msingi huo, iwapo hakutakuwepo mpango wa kimsingi kwa ajili ya kipindi hicho basi yamkini mwenye kustaafu akakumbwa na matatizo ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Iwapo mwenye kustaafu atakumbwa na matatizo jambo hilo litamuathiri vibaya yeye pamoja na familia, jamii na nchi nzima kwa ujumla.
Katika karne zilizopita uzee aghalabu ulikuwa unaainishwa kwa kutazama mabadiliko ya kidhahiri mwilini na wala si umri kwani wengi hawakuwa na uwezo wa kuhesabu miaka kwa usahihi. Lakini leo uzee ni kipindi ambacho kimeainishwa katika sheria na hivyo serikali ndiyo ambayo hupanga wakati wa kustaafu na baada ya hapo kuanza kulipa kile kinachojulikana kama malipo ya uzeeni.
Kwa kawaida wakati mtu anapostaafu baada ya kufanya kazi kwa miaka mingi, huibuka ufa katika maisha na huwa vigumu kuujaza. Kipindi hiki cha mpito kinapaswa kusimamiwa kwa uangalifu hata na wale wasiokuwa na tatizo lolote la kifedha ambao huutazama kama fursa ya kupumzika kwani wao pia hukumbwa na masaibu wakati huu.
Zama za kustaafu hutajwa kuwa zama za kuanza upweke. Mtu mwenye kustaafu huanza kuwaza na kuwazua na hata kukumbwa na msongo wa mawazo hata kabla ya kustaafu. Baadhi ya watu wenye kuelekea kustaafu huanza kuchanganyikiwa kwa sababu ya kutokuwa na mpango maalumu wa kukabiliana na kipindi hiki kipya katika maisha.
Wataalamu wanasema iwapo mwenye kustaafu atatafakari vizuri na kutambua ukweli na uhalisia wa mambo na kutambua kuwa kipindi hiki ni sehemu ya maisha, basi anaweza kuchukua hatua za kimantiki kukabiliana na hali hii mpya.
Ali Akbar Dekhoda, msomi na mwanafikra Muirani katika kamusi yake maarufu amefasiri neno kustaafu ifuatavyo : "Kustaafu ni kuinuka na kuanza tena." Kwa msingi huo, iwapo mtu atakuwa na mtazamo chanya kuhusu kustaafu, atakuwa ameingia katika kipindi kipya cha maisha ambayo atakipitisha kwa njia nzuri".
Mtu mwenye kustaafu anaweza kutumia kipindi kipya cha maisha kujishughulisha na mambo kadha wa kadha. Aghalabu ya waliostaafu huwa na ujuzi mkubwa ambao waliweza kuupata katika kipindi cha miaka walioyofanya kazi. Kwa msingi huo ujuzi na maarifa waliyonayo wanaweza kuwapa maelfu ya wengine na jambo hili huweza kuwaletea furaha na ridhaa.
Bertrand Russell mwanafalsafa maarufu wa Uingereza, wakati alipokuwa akishereheka mwaka wa 90 wa kuzaliwa kwake aliandika makala kuhusu zama za uzeeni na kusema: "Uzee una shida na raha zake na ni wazi kuwa kwa wengi masaibu ya uzeeni hayavutii. Lakini kuna mazuri mengi katika uzeeni; hii ni kwa sababu kadiri umri unavyozidi kuongezeka uzoefu nao huzindi kuongezeka. Mimi nimewaona watu wengi ambao katika zama za ujana walikuwa na uwezo lakini hawakufanya kazi yenye umuhimu. Lakini wakati umri wao ulipozipidi kupanda walipata uzoefu na kufahamu wanachopaswa kufanya."
Uchunguzi umebaini kuwa, idadi kubwa ya watu hupata mafanikio makubwa maishani wakati wanapostaafu. Kuna wasomi na wanasayansi wengi ambao huvumbua mengi katika zama zao za uzeeni.
Kwa hivyo, ni wazi kuwa tunaweza kutumia kipindi cha uzeeni au kustaafu katika kuvumbua mambo mapya katika nyuga mbali mbali kwa faida ya jamii ya mwanadamu.
Wanasaikolojia wanaamini kuwa, wasanii na waandishi huweza kufanya kazi bora zaidi kadiri umri unavyozidi kuongezeka.
Erik Homburger Erikson mwanasaikolojia maarufu mwenye asili ya Ujerumani anaamini kuwa wakati wa uzeeni, mtu huweza kupata imani thabiti kwani huwa katika mazingira ya kuweza kudiriki vyema masuala mbali mbali na hata kuwa mzalishaji wa fikra au bidhaa. Anasema iwapo mwenye kustaafu hatachukua muelekeo huo, ataanza kupata hisia hasi na kujiona kama asiyefaa. Anaongeza kuwa, wakati wa uzeeni, mtu huweza pia kusimamia vizuri majukumu ya kijamii kutokana na uzoefu alionao.
Uchunguzi wa miaka iliyopita unabaini kuwa, watu mashuhuri duniani kama vile mwanasiasa Winston Churchill, mchoraji Pablo Ruiz y Picasso, na mwanafasafa Betrand Russell waliweza kupata mafanikio makubwa katika zama za uzeeni na walikuwa na uwezo mkubwa pamoja na kumbukumbu nzuri.
Walter Benjamin msomi na mwanafasafa wa Ufaransa katika mwaka wa 1754 akiwa na umri wa miaka 70 aliandika kitabu maarufu kilichokuwa na maudhui ya 'Utamaduni wa Falsafa' naye Thomas Alva Edison , mvumbuzi maarufu wa Marekani akiwa na umri wa miaka 70 alivumbua namna umeme unavyoweza kutumiwa kuendesha injini.
Kama tulivuotangualia kusema, kuna haja ya kuwa na mpango maalumu wa zama za kustaafu ili mwenye kustaafu asikumbwe na matatizo ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, kwani hali hiyo itamuathiri vibaya pamoja na familia, jamii na nchi nzima kwa ujumla.
Kuna wale ambao katika kipindi hiki kipya katika maisha huanza kukumbwa na aina fulani ya msongo wa mawazo, hasira na kutoridhia hali ya mambo. Hivyo wanapaswa kudiriki na kushauriwa kuwa hiki na kipindi kisichoepukika maishani. Njia bora zaidi ya kuandaa kipindi cha kustaafu ni kuwa na mpango maalumu na sahihi wa maisha ya kila siku kama vile kusoma vitabu, ukulima usio mgumu, biashara, kutembelea jamaa na marafiki n.k.
Kwa msingi huo tunamaliza kwa kusema kuwa, kustaafu si miwsho wa njia bali ni mwanzo mpya katika maisha.