Mar 01, 2016 11:58 UTC
  • Uislamu Chaguo Langu (94)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika kipindi hiki ambacho huangazia watu ambao waliamua kufuata njia iliyojaa nuru katika maisha ya dunia na kesho akhera yaani Uislamu baada ya kufanya utafiti wa kina.

Katika makala yetu ya leo tutamwangazia Mmarekani mwingine aliyesilimu na kuafuata njia ya haki. Endeeleeni kuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
@@@
"Jina langu ni Abu Hadi. Kisa cha namna nilivyokuwa Mwislamu kinaanzia katika mji wa Long Beach, jimbo la California katika pwani ya Bahari ya Pacific nchini Marekani. Wazazi wangu walitalikiana nikiwa na umri wa miaka minne na baada ya hapo baba yangu alihamia katika mji mwingie. Mimi, kaka zangu wawili mapacha pamoja na dada yangu mdogo tulibakia na mama yetu mzazi. Mama yetu alikuwa akifanya kazi kwa bidii ili aweze kukidhi mahitaji yetu na kutokana na kuwa hakuwa na masomo ya juu alilazimika kufanya kazi zenye mishahara duni. Kwa msingi huo hakuweza kututosheleza na hatimaye alishindwa kabisa kuendelea na hali hiyo na hivyo tukaenda kuishi katika nyumba ya babu yetu."
Hayo wapenzi wasikilizaji ni maneno ya Abu Hadi, Mmarekani aliyesilimu. Abu Hadi anasema alikumbwa na masaibu mengi tokea utotoni kutokana na hali ya familia yake. Hivyo alikimbilia katika muziki ili apate hifadhi. Baba yake alikuwa na mjumuiko mkubwa wa miziki ya Jazz na Classic Rock kwa hivyo ilikuwa rahisi kwake kupata anuai ya miziki. Kwa hivyo wakati wote akihisi upweke alikuwa anasikiliza muziki. Hatua kwa hatua alianza kuhifadhi baadhi ya miziki aliyokuwa akisikiliza na hivyo akavutiwa na uimbaji. Anaendelea kusema kuwa: "Nikiwa na umri wa miaka 12 nilinunua gitaa yangu ya kwanza ya kielektroniki. Nilikuwa nafanya mazoezi sana na gitaa hiyo hadi nikavimba vidole. Babu yangu aliona namna nilivyokuwa nimevutiwa kupindukia na muziki na hivyo akaamua kuninusuru. Ilikuwa Jumapili asubuhi nikasikia anabisha mlango wa chumba changu na akaniambia, 'amka umefika wakati wa kwenda kanisani'. Niliruka kutoka kitandani na nikavaa nguo. Tokea wakati huo nikavutiwa sana na masuala ya kwenda kanisani ambako pia nilipata marafiki wengi. Hapo tulikuwa na mijadala mirefu kuhusu Ukristo na falsafa. Kasisi wa kanisa hilo alikuwa mtu mwenye elimu ya juu katika teolojia. Katika mazungumzo yangu naye alinifahamisha nukta mpya kuhusu Ukristo ambazo sikuzijua hapo awali. Niliendelea kwenda kanisani sambamba na kuimarisha kipawa cha muziki na hatimaye mimi na marafiki zangu tuliunda kundi la muziki." Mmarekani huyu aliyesilimu anaendelea kusimulia kwamba: "Baada ya kuunda kundi hilo la muziki nilisahau kabisa masuala ya Ukristo na kwenda kanisani. Nilianza kwenda katika matamasha ya kianasa na kuwatumbuiza washiriki. Baada ya hapo tukawa tunaenda vikao vya mazoezi ya muziki na hapo nikaanza kutumia pombe, dawa za kuelevya na kufanya vitendo vingine vya uhalifu.
Kila wakati niliporudi nyumbani na kukaa peke yangu nilitafakari yaliyojiri pamoja na marafiki niliokuwa nao na kutambua kuwa huo si mkondo sahihi. Hatu kwa hatua nilianza kuhisi upweke tena na singeweza kustahamili hali hiyo. Nilihisi kana kwamba naghiriki."
Hapa tunaona kuwa hata kama Abul Hadi alikuwa amefikia takwa lake la muda mrefu la kuwa mwanachama wa kundi la wanamuziki, lakini pamoja na hayo hakuwa amepata utulivu wa kiroho. Anafafnaua zaidi kuhusu suala hili kwa kusema: "Katika kilele cha ujana, anasa na starehe za muziki, sikuwa na wakati wa kutafakari kwa kina. Sikuwa nafahamu roho yangu inaelekea katika upande gani na hivyo nilikuwa nimechanganyikwa na nikawa nimekosa mwelekeo maalumu maishani. Yale yote nilikuwa nimetamani kuyapata niliyafikia lakini yalishabihiana na sarabi. Ili kusahau masaibu ya kiroho niliyokuwa nayo niliamua kutumbukia zaidi katika ulevi na anasa. Nilianza kubakia muda mrefu zaidi katika studio za kurekodi lakini hakuna chochote kilichobadilika. Hatimaye siku moja niliamua kufanya jambo ambalo nilikuwa sijawahi kulifanya kwa muda wa miezi miwili, yaani kupiga magoti na kuomba dua. Nilimwambia Mwenyezi Mungu kuwa nilikuwa sijui ni kipi kinachonifaa maishani na nikamuomba anionyeshe njia sahihi na iliyonyooka ambayo itaweza kuniondolea mfadhaiko wa nafsi na kuniwezesha kuwa na maisha bora baada ya kuaga dunia."
@@@
Abul Hadi aliamua kufanya bidii kutafuta njia ya hali. Katika kipindi hicho mama yake alibadilisha dini na kuwa Mwislamu. Hapo alikuwa na hamu kubwa sana ya kuujua Uislamu, anafafanua zaidi kwa kusema: "Nilikuwa na umri wa miaka 15 ambapo baada ya mama yangu kusilimu alikuwa akishiriki katika somo la kuujua Uislamu katika chuo kikuu. Alizungumza nami mara kadhaa kuhusu Uislamu. Lakini kile kilichonivutia zaidi kumhusu ni namna tabia zake zilivyobadilika baada ya kuwa Mwislamu. Mama yangu sasa alikuwa ni mwenye tabia nzuri, mwenendo mwema sambamba na kusimama imara kuhusu itikadi yake. Mabadiliko hayo yalipanda mbegu katika moyo wangu lakini katika kipindi hicho sikuweza kudiriki hilo. Mama yangu alianza kuvaa hijabu miaka mitatu baada ya kusilimu. Uamuzi wake huo ulinivutia sana kwani wakati huo kulikuwa na idadi ndogo sana ya wanawake wenye vazi la hijabu katika eneo letu. Alikuwa muuguzi katika hospitali moja kubwa na hivyo alilazimika kuvumilia kejeli za wafanyakazi wenzake. Tangu wakati huo nilianza kufanya utafiti kuhusu Uislamu. Abul Hadi alifanya pia utafiti kuhusu dini zingine lakini anasema Uislamu ndio uliomvutia zaidi. Hivyo aliamua kuomba msaada wa mama yake katika utafiti wake. Anaendelea kusema kuwa: "Nilimuomba mama yangu anisaidie naye alisema: 'Iwapo unataka kujua mengi kesho njoo twende pamoja nikuarifishe kwa marafiki zangu Waislamu.' Niliandamana naye kama alivyo sema na tulipofika niliona wanawake kadhaa waliokuwa na vazi la hijabu na mwanume mmoja. Mama yangu aliniambia, 'huyu bwana jina lake ni Muhammad'. Nilianza kuzungumza naye na akaniambia kuwa ana asili ya Syria. Pamoja na hayo alikuwa anazungumza Kiingereza vizuri sana pasina kuwa na lahaja. Aliniuliza: 'Unamuamini Mwenyezi Mungu? Nilijibu kwa kusema ndio. Hapo akaniuliza, 'Je unafuata dini gani'? Nilimfahamisha kuwa nilizaliwa katika familia ya Kikristo lakini nilikuwa siendi kanisani tena. Hapo aliniuliza, 'kwani nini?' Nilidhani kwa kuwa yeye ni Mwislamu angefurahia kutokana na kuwa nilikuwa siendi kanisani. Papo hapo nilimfahamisha kuwa nilikuwa napinga baadhi ya itikadi za ukristo kama vile utatu, na 'dhambi ya awali' (dhambi inayodaiwa kuwa mwanaadamu amezaliwa nayo". Niliongeza kuwa nilikuwa na maswali mengi ambayo hakuna aliyeweza kuyajibu. Aidha nilimfahamisha kuwa nilikuwa mwimbaji. Katika kujibu alisema: 'Wajua kuwa dini ya mababu sio njia pekee ya kumfikia Mwenyezi Mungu. Aliongeza kuwa kuna njia bora za kumfikia Mwenyezi Mungu. Alizungumza nami kuhusu misingi ya Uislamu na kunifahamisha kuwa iwapo nitafikia natija ya kimantiki na sitaona nukta yoyote dhaifu basi angenifunza zaidi kuhusu Uislamu."
Tauhidi, Unabii, Sala na masuala mengine mengi kuhusu Uislamu. Baada ya mazungumzo hayo na Mohammad, Abul Hadi alipata irada imara zaidi ya kuukubali Uislamu maishani. Anafafanua zaidi kwa kusema: "Nilizungumza na Mohammad na mazungumzo yetu yaliendelea kwa masaa kadhaa hadi saa 10 alfajiri. Pamoja na jitihada zangu zote sikuweza kupata nukta yoyote dhaifu katika yale niliyokuwa nimejifunza kuhusu Uislamu. Mohammad alikuwa anazungumza kwa njia ya wazi na inayoeleweka na kila alichokisema kilikuwa cha mantiki. Mazungumzo yake yalinitatulia matatizo yote niliyokuwa nayo kuhusu Ukristo na hivyo sikuwa na chochote cha kusema.
Baada ya usiku huo nilitafakari sana kuhusu masuala mbalimbali na hatimaye niliutambua Uislamu kama njia ya haki na nikatamka shahada mbili. Nilienda kwa marafiki zangu wanamuziki na kuwafahamisha kuwa mimi si mwanamuziki tena kwani nimepata njia ya haki maishani, yaani Uislamu. Tokea wakati huo hadi sasa imani yangu imekuwa ikiimarika siku hadi siku.

 

Tags