Suratul Qas'as 14-17 (685)
Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 14-17 (Darsa ya 685)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 685, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 14 ambayo inasema:
وَلَمَّا بَلَغَ أَشُدَّهُ وَاسْتَوَى آتَيْنَاهُ حُكْمًا وَعِلْمًا وَكَذَلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ
Na Musa alipo fikilia kukomaa kwake na akastawi, tulimpa hekima na ilimu. Na hivi ndivyo tunavyo walipa walio wema.
Aya hii inagusia sehemu nyengine ya kisa cha maisha ya Nabii Musa (AS) na kueleza kwamba: wakati Musa alipofikia rika la ujana, Mwenyezi Mungu aliutia nguvu uwezo wake wa fikra, akili na wa ilhamu za mambo ya kheri na kumpa elimu na uono ili aweze kufahamu hakika za mambo na kupambanua kwa usahihi baina ya haki na batili. Inafaa tueleze kwamba kipindi cha ujana ndio cha kilele cha nguvu na uwezo wa kila mtu katika umri wake wote. Fadhila na uraufu wa Allah kwa Nabii Musa katika kipindi hicho ulitokana na usafi wake wa kiroho na ustahiki aliokuwa nao wa kujaaliwa neema hiyo. Kwa mujibu wa aya hii, kila mtu afanyaye wema na ihsani basi atapata fadhila na rehma za Mola. Tab'an ni kwa kuondoa daraja ya kushushiwa wahyi na kupewa utume ambayo Nabii Musa aliifikia baadaye kwa kupewa cheo na hadhi hiyo ya Utume. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba ujana ndio kipindi bora cha maisha ya mtu. Kwa sababu katika kipindi hicho uwezo wa kimwili na ukuaji wa akili zinajumuika pamoja na kuandaa mazingira ya ukamilifu wa mtu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kuwafanyia wema watu na kuwa mja mwema ni sababu za kumfanya mtu apate rehma na fadhila maalumu za Mwenyezi Mungu.
Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 15 ambayo inasema:
وَدَخَلَ الْمَدِينَةَ عَلَى حِينِ غَفْلَةٍ مِّنْ أَهْلِهَا فَوَجَدَ فِيهَا رَجُلَيْنِ يَقْتَتِلانِ هَذَا مِن شِيعَتِهِ وَهَذَا مِنْ عَدُوِّهِ فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِن شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ فَوَكَزَهُ مُوسَى فَقَضَى عَلَيْهِ قَالَ هَذَا مِنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ إِنَّهُ عَدُوٌّ مُّضِلٌّ مُّبِينٌ
Na akaingia mjini wakati wenyeji wake wako kwenye mghafala. Akakuta humo watu wawili wanapigana - mmoja ni katika wenzake, na mwengine katika maadui zake. Yule mwenzake alimtaka msaada kumpiga adui yake. Musa akampiga ngumi, akamuuwa. Akasema: Hiki ni kitendo cha Shet'ani; hakika yeye ni adui, mpotezaji dhaahiri.
Nabii Musa (AS), mpaka alipokuwa katika rika la ujana alikuwa akiishi kwenye kasri la Firauni; na kama walivyokuwa watu wengine waliokulia na kuishi ndani ya kasri hilo alikuwa katika mazingira mazuri kimaisha pamoja na kupewa mafunzo ya kupigana na kupambana. Siku moja alitoka kasrini na kuelekea mjini, akawa anatembea kupita kichochoro kimoja hadi kingine. Mara akaona ugomvi wa watu wawili waliokuwa wakipigana mpaka kukaribia kuuana. Mmoja wa watu hao alikuwa wa kaumu ya Bani Israil na mwengine alikuwa Mqibti wa Misri. Yule mtu wa Bani Israil alimtambua Nabii Musa kuwa ni mwenzake hivyo akamwomba msaada. Nabii Musa ambaye aliona mtu huyo anadhulumiwa alikimbilia kumsaidia kwa kumpiga ngumi Mqibti iliyomtupa chini na kukata roho papo hapo.
Yeye mwenyewe Nabii Musa hakufikiria asilani kama uzito wa ngumi yake ungekuwa mkubwa kiasi kwamba konde lake moja tu lingemgaragaza na kummaliza adui. Musa hakukusudia kumuua mtu yule bali alichukua hatua aliyochukua kwa ajili ya kumtetea tu mtu aliyekuwa akionewa na kudhulumiwa. Hata hivyo Mqibti huyo hakuhimili kishindo cha ngumi yake hivyo akaaga dunia. Ni hapo ndipo Nabii Musa alipotanabahi na kutambua chanzo cha mzozo na ugomvi ule akasema: chanzo cha mizozo yote na magomvi yote ni shetani, anayechochea ugomvi na mapigano baina ya wanadamu. Kwa hakika yeye ni adui wa wanadamu ambaye huwapotosha kwa kuwagombanisha na kuwapiganisha.
Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba japokuwa Nabii Musa alilelewa na kukulia ndani ya kasri la Firauni lakini alikuwa mtetezi wa madhulumu na wanaoonewa, si madhalimu na waonevu. Kama ambavyo Asia mke wa Firauni alikuwa akiishi ndani ya kasri lakini alimwamini Musa (AS) na akaitoa mhanga roho yake katika njia hiyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa Mitume walikuwa watu waungwana, watetezi wa wanaodhulumiwa na wapiga vita dhulma; hivyo wakisimama kukabiliana na madhalimu kwa ajili ya kuwatetea watu madhulumu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba kuchochea ugomvi na mapigano baina ya watu ni kazi ya shetani. Kwa hivyo tujitahidi kuzidhibiti ghadhabu na hasira zetu na wala tusimruhusu shetani atutawale.
Darsa ya 685 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 16 na 17 ambazo zinasema:
قَالَ رَبِّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي فَاغْفِرْ لِي فَغَفَرَ لَهُ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ
Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nimejidhulumu nafsi yangu; basi nisamehe. Akamsamehe; hakika Yeye ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
قَالَ رَبِّ بِمَا أَنْعَمْتَ عَلَيَّ فَلَنْ أَكُونَ ظَهِيرًا لِّلْمُجْرِمِينَ
Akasema: Mola wangu Mlezi! Kwa ulivyo nineemesha, basi mimi sitakuwa kabisa msaidizi wa waovu.
Kutokana na kuuliwa Mqibti yule, ilikuwa ni wazi kwamba Waqibti wengine wangemsaka mtu aliyewaulia jamaa yao ili wamkamate na kumlipizia kisasi. Nabii Musa, alikuwa ni kama ameidhulumu nafsi yake kutokana na ngumi aliyompiga Mqibti; kwa sababu kitendo hicho kingemtia hatarini; maana Waqibti wangetaka kumkamata tu. Kwa hakika tukio hilo halikumaanisha kwamba Nabii Musa alikuwa amefanya dhambi, lakini lilikuja kumsababishia mashaka na misukosuko baadaye. Kwa hivyo alimwomba maghufira Allah amsamehe kama atakuwa amekosea katika kutekeleza wajibu wake. Amfanyie wepesi katika jambo hilo na kumuokoa na shari ya Mafirauni. Naye Mola Mwenyezi akamtakabalia dua yake na kwa hivyo hakukamatwa na kuingia mikononi mwa Waqibti. Baada ya hapo Nabii Musa akaahidi kwa Mwenyezi Mungu kwamba kwa kushukuru uraufu na rehma hizo za Mola za kumwepusha kuingia mikononi mwa maadui, hadi mwisho wa uhai wake hatowasaidia waovu na madhalimu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika kuwaokoa waumini na shari ya madhalimu, inapasa kuwa waangalifu na wenye hadhari ili kuepusha kutokea hatari kadiri iwezekanavyo pamoja na madhara yasiyotarajiwa yanayoweza kutokea. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa jambo lolote la makosa hata kama mtu atalifanya kwa kuteleza na bila ya kukusudia litakuwa na taathira zake tu za hali na za kimaumbile. Aidha aya hizi zinatufunza kuwa njia sahihi ya mtu kuonyesha ushukurivu kwa nguvu na uwezo alionao ni kuwasaidia wanaodhulumiwa na kujiepusha kushirikiana na madhalimu. Kwa haya machache tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atusamehe madhambi yetu, atutakabalie dua zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/