Sura ya Al-A'nkabut, 24-26 (707)
Sura ya Al-A'nkabut, aya ya 24-26 (Darsa ya 707)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 707, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 29 ya Al-A'nkabut. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 24 ambayo inasema:
فَمَا كَانَ جَوَابَ قَوْمِهِ إِلاَّ أَن قَالُوا اقْتُلُوهُ أَوْ حَرِّقُوهُ فَأَنجَاهُ اللَّهُ مِنَ النَّارِ إِنَّ فِي ذَلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ
Basi haikuwa jawabu ya watu wake ila ni kusema: Muuweni au mchomeni moto! Mwenyezi Mungu akamwokoa na moto. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao amini.
Katika sura hii ya Al-A'nkabut, baada ya kutajwa habari za Nabii Nuh (AS) amezungumziwa Nabii Ibrahim (AS); na aya zilizotangulia zikaeleza hoja alizotoa Mtume huyo katika kuwalingania wito wa tauhidi washirikina wa kaumu yake na kuwataka wauzingatie ulimwengu wa baada ya kifo. Aya hii tuliyosoma inaeleza jibu na hatua waliyochukua watu hao dhidi ya wito wa Nabii Ibrahim na kueleza kwamba: kwa kuwa watu hao hawakuwa na jibu la maana na la kimantiki la kukabiliana na maelezo yenye hoja na mantiki makini ya mtukufu huyo waliamua kutumia nguvu na mabavu; na kama walivyo madhalimu na majabari wote wa dunia walitaka kuchukua hatua kali dhidi ya Nabii Ibrahim (AS). Baadhi ya watu hao walishauri wamchome moto na wengine wakasema: bora mnyongeni hasa tupate kupumua. Kama ilivyoashiriwa katika aya ya 68 hadi 70 za Suratul-Anbiyaa, hatimaye washirikina hao waliamua kuwasha moto mkubwa na kumtupa Nabii Ibrahim ndani yake. Kwa hivyo aya tuliyosoma inaendelea kueleza kwamba watu hao walikula njama dhidi ya maisha ya Mtume wa Allah. Lakini Mwenyezi Mungu alimuokoa Mtume wake na kuunguzwa motoni. Kama ilivyoelezwa katika aya zingine za Qur'ani, kwa amri ya Allah SW moto huo uliowashwa na washirikina ukawa baridi na salama kwa Nabii Ibrahim pasina kumsababishia madhara yoyote. Tukio hili lenyewe linatoa ibra kubwa kabisa kwa waumini, wajue kwamba nguvu za Allah ziko juu ya nguvu zingine zote, kwa hivyo wasitishike na nguvu za kidhahiri na za kimaada. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mantiki ya maadui wa dini ni ya unyanyasaji, utesaji, mauaji na unyongaji. Wao hawataki kuelewa na kufahamu haki na hakika ya mambo bali wanachotaka ni kulinda madaraka, hadhi na utajiri wao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa uchache wa idadi ya waumini si sababu ya kuwafanya wasalimu amri mbele ya majabari na madhalimu. Japokuwa Nabii Ibrahim (AS) alikuwa mtu mmoja tu lakini alisimama kukabiliana na watu wapotofu na makafiri wa kaumu yake na Allah SW akampa auni na msaada wake. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba irada na lile atakalo Allah linashinda nyenzo na visababishi vyote. Yeye ndiye mletaji visababishi na ndiye pia anayeondoa athari za visababishi hivyo. Allah SW anaupa moto nguvu ya kuunguza na kila pale atakapo anaiondoa nguvu hiyo.
Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 25 ambayo inasema:
وَقَالَ إِنَّمَا اتَّخَذْتُم مِّن دُونِ اللَّهِ أَوْثَانًا مَّوَدَّةَ بَيْنِكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ثُمَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُ بَعْضُكُم بِبَعْضٍ وَيَلْعَنُ بَعْضُكُم بَعْضًا وَمَأْوَاكُمُ النَّارُ وَمَا لَكُم مِّن نَّاصِرِينَ
Na alisema: Hakika nyinyi mmeyashika masanamu badala ya Mwenyezi Mungu kwa mapenzi yaliyo baina yenu katika uhai wa duniani. Kisha Siku ya Kiyama mtakataana nyinyi kwa nyinyi, na mtalaaniana nyinyi kwa nyinyi. Na makaazi yenu ni Motoni. Wala hamtapata wa kukunusuruni.
Baada ya Nabii Ibrahim kuokoka na moto hakusita kuendelea kufanya tablighi na kuwalingania watu wake wito wa tauhidi na kuonesha udhaifu wa imani ya kuabudu masanamu. Kwa mtazamo wa kihistoria kila kaumu na kabila ambalo limekuwa likiabudu masanamu limekuwa likijivunia na kujifakharisha kwa mungu wake huyo bandia na kulifanya kuwa alama ya shakhsia na utambulisho wa watu wa kaumu au kabila hilo. Watu hao huwa na umoja na mshikamano kutokana na wote kuabudu sanamu moja. Isitoshe kwa mtazamo wao kufanya hivyo ni kuheshimu imani na itikadi za wazee wao waliotangulia na kuabudu kile kile kilichokuwa kikiabudiwa na wao. Nabii Ibrahim (AS) aliwaeleza watu wa kaumu yake kwamba: haya mafungamano yenu na wazee wenu waliopita pamoja na watu wa kaumu na kabila lenu yaliyounganishwa na ibada ya kuyaabudu masanamu na kukufanyeni muwe na uhusiano imara baina yenu yatasambaratika Siku ya Kiyama. Wakati huo kila mmoja atataka kumbebesha mwenzake mzigo wa madhambi yake na kumwona na hatia katika ibada hiyo ya kuabudu masanamu. Wale waliokuwa wafuataji watawaapiza viongozi wao na wakuu wa jamii yao na kuwaona ndio sababu ya wao kupotea. Hakuna yeyote atakayekubali kubeba dhima na mas-ulia ya upotokaji huo mkubwa. Hao wazee wenu waliotangulia ambao mnasema mnaendeleza ibada ya kuabudu masanamu kwa sababu ya kuheshimu itikadi zao, Siku ya Kiyama watakutwisheni dhima ya kufanya hayo nyinyi wenyewe, kwamba kwa nini mliamua tu kuendelea kufuata njia potofu bila ya kutumia akili zenu na kufikiri. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mhimili wa umoja na utambulisho wa jamii unapasa kuwa kitu sahihi na cha mantiki. Si kama walivyo waabudu masanamu ambao masanamu yao yalikuwa ndio kiunganishi baina yao na wazee wao waliopita. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa fikra na mantiki zinapasa zitawale hisia za upendo na hamasa; na si mafungamano ya kiupendo yawe ndio kipimo cha kuainisha aina ya fikra, imani na itikadi ya mtu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba urafiki wa duniani uliojengeka juu ya msingi usio sahihi, sio tu hautawafaa watu Siku ya Kiyama bali utakuwa sababu ya chuki na uadui baina yao.
Aya ya 26 ya sura yetu hii ya A'nkabut ndiyo inayotuhatimishia darsa yetu ya leo. Aya hiyo inasema:
فَآمَنَ لَهُ لُوطٌ وَقَالَ إِنِّي مُهَاجِرٌ إِلَى رَبِّي إِنَّهُ هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ
Lut'i akamuamini, na akasema: Mimi nahamia kwa Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Kama tulivyoona, Nabii Ibrahim (AS) alitoka salama usalimini kwenye moto mkubwa wenye kurindima na wenye macheche makali, uliokuwa umewashwa na kina Namrudi. Na mtu wa kwanza aliyemwamini na kisha akawa mwenza na msaidizi wake, alikuwa Lut, ambaye baadaye naye pia akafikia daraja ya Utume na akawa mfanya tablighi na mfikishaji risala na ujumbe wa Nabii Ibrahim. Wakati Nabii Ibrahim alipoona kuwa licha ya watu wa kaumu yake kushuhudia muujiza huo mkubwa hakutokea yeyote miongoni mwao aliyesilimu na kumwamini, alitangaza kuwa kwa sababu ya Mwenyezi Mungu anaamua kuhajiri na kuihama ardhi na wat'ani wake na wa wazee wake ili kwenda kuwalingania wito wa Allah wa tauhidi watu wa maeneo mengine. Hijra hiyo ilimnusurisha yeye na maudhi na mateso ya watu wa mji wake, na vilevile ilimpa fursa ya kuendelea kutekeleza jukumu lake na kuweza kueneza wito wa tauhidi katika maeneo mengine. Bwana Mtume SAW, naye pia alipohajiri kwa kuhama Makka na kuhamia Madina, aliweza kupumua kutokana na mbinyo, maudhi na mateso ya washirikina wa Makka, na vilevile akapata wasaa wa kuwalingania Uislamu watu wa Madina. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Mitume, hawako kama walivyo wafalme wanaopigania madaraka zaidi kwa mmoja kutaka kumngo'a na kumwondoa mwenzake. Wao Mitume wanafikiria kupeana msukumo na kusaidiana wao kwa wao na kueneza wito wa dini ya Mwenyezi Mungu. Ni kama alivyofanya Nabii Lut kwa Nabii Ibrahim (AS), ambapo alimwamini, akampa msukumo na kumsaidia katika kutekeleza jukumu hilo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, watu wa njia ya Mwenyezi Mungu hawajifungamanishi na nchi, mahala na zama bali wakati wowote inapolazimu wanahajiri na kuhama kwa ajili ya Allah. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 707 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atuwezeshe kuifuata na atuonyeshe batili atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/