Sura ya Al-A'nkabut, 56-61 (714)
Sura ya Al-A'nkabut, aya ya 56-61 (Darsa ya 714)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 714, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 29 ya Al-A'nkabut. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 56 na 57 ambazo zinasema:
يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ أَرْضِي وَاسِعَةٌ فَإِيَّايَ فَاعْبُدُونِ
Enyi waja wangu mlio amini! Kwa hakika ardhi yangu ina wasaa. Basi niabuduni Mimi peke yangu.
كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ ثُمَّ إِلَيْنَا تُرْجَعُونَ
Kila nafsi itaonja mauti. Kisha mtarudishwa kwetu.
Moja ya miongozo ya kivitendo ya kuvutia ya Qur'ani ni wa kumtaka Muislamu ahajiri kwa ajili ya kulinda imani yake. Katika zama za mwanzoni mwa Uislamu, Waislamu walikuwa katika mbinyo mkali wa washirikina na wakawa hawawezi kutekeleza majukumu na wajibu wao wa kidini kwa uhuru. Kwa sababu hiyo Bwana Mtume Muhammad SAW na waumini wa kweli walihajiri wakahama Makka na kuhamia Madina na kustakimu katika mji huo.
Aya hizi tulizosoma zinataja kaida na kununi moja kuu kwa kusema: "Mfungamano na mapenzi ya mji na wat'ani wenu visikuzuieni kujenga imani zenu na kumwabudu Mola wenu. Msidhani kwamba mtabaki hai milele katika dunia hii; kwa hivyo lengo lenu katika maisha lisiwe ni kutaka kujikusanyia mali tu na utajiri na kutaka kujilindia nafasi, hadhi na vyeo vyenu. Kama mtazingatia kwamba akhera ni maskani na makazi ya milele katu hamtotekwa na kujifunga na mapenzi ya kupindukia kwa mji na wat'ani wenu.
Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika kuchagua mahala pa kuishi tuzingatie kwa uzito mkubwa suala la kuchunga na kulinda dini na imani zetu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuhajiri kwa ajili ya dini ni moja ya majukumu ya waumini. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba watu watakaotumbukia kwenye lindi la upotofu kwa sababu ya mafungamano na mapenzi ya mji na nchi zao hawatokuwa na udhuru wa kukubalika Siku ya Kiyama. Wa aidha tunajifunza kutokana na aya hizi kuwa mauti ni ya watu wote, wala hakuna njia yoyote ya kuyakwepa. Kwa hivyo katika kupanga mahesabu ya maisha yetu kuna ulazima pia wa kupanga na kufikiria juu ya kipindi cha baada ya kifo.
Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 58 na 59 ambazo zinasema:
وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَنُبَوِّئَنَّهُم مِّنَ الْجَنَّةِ غُرَفًا تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا نِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ
Na wale ambao wameamini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawaweka katika maghorofa ya Peponi yapitiwayo na mito chini yake, wadumu humo. Ni neema iliyoje kwa malipo ya watendaji.
الَّذِينَ صَبَرُوا وَعَلَى رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ
Ambao walisubiri, na wakamtegemea Mola wao Mlezi.
Katika aya hizi, Mwenyezi Mungu SW anawaahidi watu ambao wamevumilia shida na tabu kwa ajili ya kulinda imani zao, na pale inapolazimu wanahajiri na kuhama katika miji yao kwamba huko akhera watakuwa na makazi bora ya kuishi katika nyumba za Peponi na watafaidika na neema zisizohesabika. Aya hizi zimetaja sifa tatu muhimu za waumini watakaoifikia Pepo ya rehma za Allah ambazo ni amali, subira na kutawakali. Inapasa kuashiria hapa kwamba imani bila ya amali njema haina thamani yoyote. Amali pia bila ya subira na uvumilivu haiwezi kuwa na tija; na subira nayo haiwezi kudumu pasina kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu.
Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba imani na amali njema ndilo sharti la kuifikia Pepo na neema za peponi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kile ambacho waumini watapoteza hapa duniani kwa sababu ya kulinda imani zao, Allah SW atawafidia Siku ya Kiyama na kuwatunukia vilivyo bora zaidi ya hivyo. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba subira na istiqama ndio siri ya kuyashinda matatizo na kufikia mafanikio katika awamu mbalimbali za maisha. Ni wazi kwamba waumini, ambao huwa siku zote wanaandamwa na maudhi na mateso ya maadui wanapaswa wawe imara na thabiti kuliko watu wengine.
Ifuatayo sasa ni aya ya 60 ambayo inasema:
وَكَأَيِّن مِن دَابَّةٍ لا تَحْمِلُ رِزْقَهَا اللَّهُ يَرْزُقُهَا وَإِيَّاكُمْ وَهُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ
Na wanyama wangapi hawawezi kujimilikia riziki zao! Mwenyezi Mungu anawaruzuku wao na nyinyi pia. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua.
Aya tuliyosoma inaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia kuhusu ulazima wa kuhajiri kwa ajili ya kulinda imani, na kueleza kwamba: "Msiwe na hofu kwa kuona kwamba kutokana na kuhajiri katika ardhi ya kufru mumepoteza kazi na biashara zenu na kufikwa na matatizo katika kukimu mahitaji ya maisha yenu. Ikiwa italazimu kuhajiri hajirini; na mjue kwamba Mwenyezi Mungu ndiye mtoaji riziki yenu. Mola huyo huyo anayeruzuku anuai za viumbe angani na ardhini, hatokusahauni nyinyi. Kwani hata wanyama, ndege na wadudu ambao hawana uwezo wa kubeba chakula chao na kukihifadhi kwenye mapango na viota vyao na kulazimika kila siku kutoka kwenye viota na mapango hayo kwenda kutafuta chakula, huwa hawarudi mapangoni na viotani mwao mikono mitupu. Bali Allah huwadhaminia riziki zao. Naye mwanadamu ni mwenye hadhi zaidi ya mnyama, kwa hivyo anao uwezo wa kufanya bidii na juhudi na kujipatia riziki yake.
Kama mtu atapoteza kazi na njia ya kupatia pato lake kwa sababu ya kuhajiri na kuwa mbali na wat'ani wake, baada ya kuhajiri upo uwezekano wa kuyafidia hayo aliyopoteza; lakini kama mtu atapitisha maisha yake katika njia ya shirki na ukafiri au kusalimu amri mbele ya dhulma, uonevu na utaghuti, hayo hayana njia ya kufidiwa; kwa sababu shirki, kufru na dhulma vinamtoa mtu nje ya mstari wa utu na ubinadamu.
Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba wanaohajiri katika njia ya Allah wasiwe na hofu juu ya riziki yao na juu ya kujikimu maisha yao; na wala wasiache kugura katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa kuchelea kukosa pato na riziki ya kuendeshea maisha yao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mtu muumini huwa kila mara anatawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu na wala harudi nyuma katika kutekeleza wajibu wake kwa Mola wake kwa kuchelea kukosa riziki. Aya hii aidha inatuelimisha kwamba Mwenyezi Mungu ambaye ni Muumba wa ulimwengu amedhamini riziki ya viumbe vyake vyote akiwemo mwanadamu.
Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 61 ambayo inasema:
وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ لَيَقُولُنَّ اللَّهُ فَأَنَّى يُؤْفَكُونَ
Na ukiwauliza; Nani aliye umba mbingu na ardhi na akalitiisha jua na mwezi? Bila ya shaka, watasema: Mwenyezi Mungu. Wapi basi wanako geuzwa?
Washirikina waliokuwa wakiishi Makka na ambao walikuwa wakiabudu masanamu walikuwa wakimkubali Mwenyezi Mungu kuwa ndiye Muumba wa kila kitu. Lakini wakiitakidi kuwa amekabidhi tadbiri na uendeshaji mambo kwa vitu kama jua, mwezi na nyota au aina mbalimbali ya masanamu yaliyoko ardhini. Wao walikuwa wakikiri kuwa Allah ndiye Muumba lakini hawakuwa wakiikubali nafasi ya Uola na ulezi wa Allah kwa waja wake. Kiasi cha kuona, kama kwamba majaaliwa yao na hata riziki yao haiko kwenye mamlaka ya Yeye Mola Mlezi na wala Yeye hana nafasi yoyote katika hilo. Ajabu ni kwamba leo hii pia kuna watu wengi ambao wanakiri kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wao, lakini hawakubali kuwa Yeye pia ndiye mwenye haki ya Uola na upangaji kanuni na sharia na wala hawatii maamrisho yake. Watu hawa wanaitakidi kwamba mwanadamu hamhitajii Mwenyezi Mungu katika maisha yake na ana haki ya kujiamulia na kujifanyia chochote atakacho.
Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba katika majadiliano ya kiitikadi tuanzie kwenye mambo yanayotuunganisha pamoja na wengine kisha tuyaendeleze hayo. Nukta ya pamoja baina ya Waislamu na washirikina wa Makka ilikuwa ni wote kuamini kuwa Muumba wa kila kitu ni Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kupotoka katika kufuata njia ya haki ni moja ya hatari inayowakabili watu wote. Kuukubali Uumba wa Allah pasina kukubali Uola wake katika maisha yote ya mtu ni aina mojawapo ya kupotoka katika kufuata haki. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 714 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuoneshe haki na atupe taufiki ya kuifuata, na atuoneshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/