Jumanne, 14 Februari, 2017
Jumanne 16 Jamadil Awwal 1438 Hijria sawa na 14 Februari 2017.
Miaka 79 iliyopita katika siku kama ya leo, Wazayuni waliokuwa na silaha na wanachama wa kundi la kigaidi la Palmach waliendeleza mauaji ya umati dhidi ya raia wa Palestina kwa kutekeleza shambulizi la kigaidi dhidi ya wakazi wa kijiji cha Sa'sa' huko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Katika operesheni hiyo iliyoendelea hadi kesho yake nyumba 20 za raia wa Palestina ziliharibiwa na watu 60 waliokuwemo, wengi wao wakiwa wanawake na watoto wadogo, wakauawa kwa umati.

Katika siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, wakati wa Vita vya Pili vya Dunia nchi mbili za Marekani na Uingereza zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya Ujerumani. Ndege 1773 za kijeshi zilitumiwa latika mashambulizi hayo ambayo ndiyo yaliyokuwa na hasara kubwa zaidi ya mali na nafsi duniani hadi hii leo. Mashambulizi hayo ya kinyama ya Marekani na Uingereza yaliyoendelea kwa kipindi cha siku tatu mtawalia yalisawazisha na ardhi miji kadhaa ya viwanda ya Ujerumani na kuifanya majivu matupu. Raia kati ya laki moja na nusu hadi laki mbili na nusu waliuawa kinyama katika mashambulizi hayo.

Miaka 53 iliyopita katika siku kama ya leo, Martin Scott tabibu mpasuaji wa Uingereza alifanikiwa kuunganisha figo ya mwanadamu. Siku hiyo Prf. Scott alichukua figo ya mtu aliyekuwa amefariki dunia muda sio mrefu na kuiunganisha na mgonjwa aliyekuwa amelazwa katika hospitali moja ya Leeds huko Uingereza. Operesheni hiyo ya kuunganisha figo ilifanyika kwa mafanikio makubwa.
Katika siku kama ya leo miaka 12 iliyopita, aliuawa Rafiq Hariri Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon kwenye mlipuko wa bomu lililotegwa garini huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon. Alikuwa mmoja wa wafanyabiashara tajiri nchini Lebanon na wakati alipofariki dunia alikuwa na umri wa miaka 61. Hariri alichukua wadhifa wa Uwaziri Mkuu wa Lebanon kutokea mwaka 1992, muda mfupi baada ya kumalizika vita vya ndani vya Lebanon hadi mwaka 1998, na kuchukua tena wadhifa huo mwaka 2000 hadi 2004.
Na Siku kama ya leo miaka 1157 iliyopita, alifariki dunia Abu Hanifah Ahmad bin Daud Dinawari. Dinawari alibobea katika elimu za falsafa, fasihi, hesabu, nujumu, elimu ya mimea na jiografia. Miongoni mwa vitabu vya mwanazuoni huyo ni pamoja na vitabu vya “al-Shi’ri wa al-Shuaraa”, “al-Nabat”, “al-Jabru wal-Muqaabalah” na “al-Buldan.”