Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (148)
Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni matumaini yetu kwamba hamjambo na mko tayari kabisa kusikiliza sehemu ya 148 ya kipindi hiki kinachojibu maswali tofauti kuhusiana na itikadi ya Kiislamu.
Kama mnavyojua katika vipindi kadhaa vilivyopita tumekuwa tukijadili suala muhimu la wajibu walionao Waislamu kwa Maimamu wa Kizazi cha Mtume Mtukufu (saw). Hilo dilo suala ambalo tumekuwa tukilijadili katika vipindi vinne vilivyopita ambapo kwa kutegemea aya na hadithi tukufu tulipata kujua majukumu manne kati ya majukumu mengine mengi ambayo Umma wa Kiislamu unapasa kuyatekeleza kuhusiana na kizazi hicho kitakatifu cha Mtume (as). Majukumu tuliyoyapitia katika vpindi hivyo ni: Wajibu wa kuwatii na kufuata sira na nyenendo zao katika maisha yetu ya kila siku, ambapo tulipata kujua kwamba kuwatii watukufu hao ni sawa kabisa na kumtii Mweyezi Mungu na Mtume wake (saw). Wajibu wa pili ni kuwarejea ili wapate kutusuluhisha katika kila tofauti na mivutano inayotokea miongoni mwetu kwa sababu wao ndio waliopewa na Mwenyezi Mungu elimu yote ya kitabu kitakatifu cha Qur’ani Tukufu ambayo inabainisha na kufafanua kila jambo. Wajibu wa tatu ni kuwapenda kunakoandamana na kuwanusuru na kuwatanguliza katika kila jambo. Amma wajibu wa nne ni kuwaswalia pamoja na kiongozi wao ambaye ni Mtume Mtukufu (saw). Baada ya kujua wajibu hizo, tunauliza kwamba je, wajibu wa tano ni upi? Karibuni wapenzi wasikilizaji tupate kujua na kunufaika kwa pamoja na jibu la swali hili?

Ndugu wasikilizaji, maandiko matakatifu yanatufahamisha kwamba miongoni mwa wajibu tulionao kuhusu Maimamu watoharifu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (saw) au haki walizonazo kwetu ni wajibu wa kuwaheshimu na kuwatukuza jambo ambalo kwa hakika ni kumuenzi na kumtukuza Mtume mwenyewe (saw) ambaye ni babu na bwana wao anayeongoza kwenye njia ya uongofu na mteule. Hivyo basi dalili ya suala hili ni aya na hadithi tukufu ambazo zinatuamuru kutukuza na kumuenzi Mtume (saw), jambo ambalo tumelizungumzia kwa urefu katika vipindi vingine vinavyojadili wajibu na majukumu yetu kuhusiana na Mtume huyo mwema (saw). Mbali na suala hili kuna hadithi nyingi sana ambazo zimenukuliwa na madhehebu zote mbili za Kiislamu kutoka kwa Mtume (saw) ambazo zinasisitiza kwa ujumla ulazima wa kutukuzwa na kuheshimiwa kizazi cha Mtume na maasumina watoharifu, ambao ni Maimamu wa uongofu (as) kwa namna maalumu.
Mbali na hadithi hizi kuna hadithi nyingine ambazo zinatilia mkazo wajibu huohuo kwa kwa kusisitiza kwamba Mtume mwenyewe (saw) alikuwa akizingatia na kushughulikia sana suala la kulindwa heshima ya kizazi chake. Kisha kuna kundi jingine la hadithi ambazo zinabainisha na kufafanua nafasi muhimu ya Maimamu wa Nyumba ya Mtume (saw) mbele ya Mweyezi Mungu na Mtume wake, nafasi ambayo kwa hakika inatulazimu kuwaheshimu na kuwaenzi kwa sababu tayari wamesifiwa na kuenziwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe pamoja na Mtume wake (saw).
Kundi la nne la hadithi hizo ni zile zinazozungumzia nafasi yao muhimu na ya kipekee ya kutetea dini ya Mweyezi Mungu kwa uwezo wao wote, jambo ambalo linatulazimu kuwaheshimu na kuwatukuza. Tunakunukulieni hapa baadhi ya hadithi hizo za makundi yote manne, hivyo endeleeni kuwa pamoja nasi.

Katika kundi la kwanza, kuna hadithi hii mashuhuri ambayo imenukuliwa na madhehebu zote mbili za Shia na Suni kama ilivyonukuliwa katika vitabu vya Kanz al-Ummal, Uyun al-Akhbar, Firdous ad-Dailami, Dhakhair al-Uqba na vingine kwamba Mtume Mtukufu (saw) alisema: ‘Nitakuwa ni mtu wa kuwafanyia shufaa watu wane Siku ya Kiama: Mtu anayekirimu kizazi changu, anayewakidhia haja zao, anayefanya juhudi za kuwatimizia mambo yao wanapoyahitajia kwa dharura na anayewapenda kwa moyo na ulimi wake.’
Na imepokelewa katika riwaya ya pili: ‘Nitawafanyia shufaa watu wane Siku ya Kiama…Mtu anayewasaidia Ahlu Beit wangu, anayewakidhia haja zao wanapozihitajia kwa dharura, anayewapenda kwa moyo na ulimi wake na anayewalinda (kuwatetea) kwa mkono wake.’
Katika kundi la pili la hadithi hizo, tutatosheka hapa kwa kwa kutaja hadithi hii ambayo imenukuliwa na madhehebu zote mbili za Kiislamu kutoka kwa mmbora wa wanawake wa ulimwengu mzima, Bibi Fatumah az-Zahraa (as) alipowalalamikia watawala wa zama zake waliompokonya urithi wa shamba la Fadak alilopewa na baba yake yaani Mtume Mtukufu (saw). Aliwalalamikia kwa kunukuu maneno ya Mtume yanayosema kwamba heshima ya mtu hulindwa kwa kuheshimiwa kizazi chake, hadithi ambayo ni mashuhuri na imenukuliwa katika vitabu vingi vikiwemo vya Taarikh al-Ya’quubi, Balaghaat an-Nisaa, al-Ih’tijaaj na vinginevyo.

Ndugu wasikilizaji, ama hadithi za kundi la tatu ni nyingi mno na haziwezi kuhesabika. Vitabu vya hadithi vya kuaminika kutoka pande zote mbili zinabainisha wazi kile ambacho kimefafanuliwa na aya za Qur’ani Tukufu kuhusu nafasi muhimu na ya juu waliyonayo Ahlul Beit wa Mtume Mtukufu (saw) mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake Mtukufu (saw), jambo ambalo linatulazimu sisi Waislamu kutukuza na kuwaenzi watukufu hao kutokana na ukuruba walionao mbele ya Mwenyezi Mungu.
Hali ni hiyohiyo kuhusu hadithi za kundi la nne ambazo zinabainisha kujitolea kwao kukubwa katika njia ya kulinda na kutetea dini ya Mwenyezi Mungu na hili ni jambo ambalo limethibitishwa na sira na mienendo yao ya maisha na pia kuthibitishwa na Umma. Nasi hapa tutatosheka kwa kutaja riwaya moja ambayo inaaminika na pande zote mbili za Shia na Suni. Riwaya hiyo ni ile ambayo imenukuliwa na Hakim katika kitabu chake cha Mustadrak, ambayo pia imenukuliwa katika kitabu cha Ibn Majah akimnukuu Ibn Mas’oud. Riwaya hiyo inasema: ‘Tulifika kwa Mtume (saw) naye akatujia akiwa ni mwenye bashasha na furaha tele usoni. Hatukumuuliza swali ila alitujibu kwa njia muwafaka na hatukukaa kimya ila alianza kutuzungumzisha yeye. Hali iliendelea hivyo hadi pale lilipopita mahala pale kundi moja la vijana wa Bani Hashim wakiwemo Hassan na Hussein. Alipowaona machozi yalimtoka na tukasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni kwa nini tunaendelea kuona machoni mwako kile tunachokichukia? Akasema: ‘Hakika sisi ni Ahlu Beit, Mwenyezi Mungu ametuchagulia Akhera juu ya dunia. Hakika Ahlu Beit wangu watafukuzwa na kutawanywa nchini baada yangu hadi zitakapopeperuka bendera nyeusi kutokea Mashariki. Wataomba haki na kunyimwa haki hiyo, kisha wataomba haki na kunyimwa haki hiyo kisha wataomba haki na kunyimwa haki haki hiyo na hatimaye watapigana na kunusuriwa. Mtu atakayediriki kipindi hicho au katika kizazi chenu basi na amwendee Imam wa Ahlu Beit yangu hata kama itakuwa ni kwa kutembea kwa magoti na mikono kwenye theluji. Hii ni kwa sababu bendera hizo ni bendera za uongofu ambazo zitakabidhiwa kwa mtu katika Ahlu Beit wangu, jina lake ni sawa na jina langu na jina la baba yake ni sawa na jina la baba yangu. Atamiliki ardhi na kuijaza kwa usawa na uadilifu kama ambavyo itakuwa imejaa uonevu na dhulma.’
Ndugu wasikilizaji ibara ya ‘jina lake ni sawa na jina langu na jina la baba yake ni sawa na jina la baba yangu’ haijatajwa katika riwaya iliyonukuliwa na Ibn Maja katika Sunan yake. Maulamaa wanasema kuwa ibara hii ni ya ziada iliyoongezwa na watawala wa Bani Abbas kwa sababu za kisiasa.

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Mswali Yatu na Majibu ya Thaqalain kwa juma hili, kipindi ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.