Mar 09, 2017 14:17 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 27 ya makala yanayokosoa kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu na suna za Bwana Mtume (sawa) mienendo ya makundi ya ukufurishaji yanayotenda jinai na mauaji ya kutisha dhidi ya Waislamu wengine.

Katika kipindi kilichopita tuliendelea kuzungumzia suala la udhalilishaji wa wanawake kunakofanywa na Mawahabi na makundi ya ukufurishaji. Tukasema kuwa makundi ya ukufurishaji yanamchukulia mwanamke kuwa ni shetani sambamba na kumlinganisha na mbwa au punda, mtazamo ambao uko kinyume kabisa na mafundisho halisi ya Qur'ani na suna za Bwana Mtume Muhammad (saw). Aidha katika fremu hiyo tulisema kuwa mtazamo wa dini ya Kiislamu kumuhusu mwanamke ni chanya na unaomuona kiumbe huyo kuwa ni sawa na ua lenye harufu nzuri.

Vinara wa Daesh na Boko Haram

Hii ni kwa kuwa, kwa kudhihiri nuru ya dini ya Uislamu, yalianza mapambano dhidi ya ada zote za kijahili kumuhusu mwanamke. Katika kipindi ambacho watoto wa kike walikuwa wakizikwa wakiwa hai huku mwanamke akionekana kama kiumbe asiye na thamani yoyote, Uislamu ulimtaja kiumbe huyo kuwa ni hakika ya mwanadamu ambaye ni sawa kabisa na mwanamume. Nukta hiyo ndiyo iliyosaidia kuhitimisha mitazamo ya ujahili na mibaya kumuhusu mwanamke katika jamii. Hata kama katika nchi za Magharibi hii leo kumejaa nara za kutetea usawa na haki kwa ajili ya mwanamke, lakini uhalisia wa mambo ni kwamba, kiumbe huyo amegeuzwa na kuwa chombo cha kibiashara na kujifurahishia katika nyanja za anasa. Kama ambavyo pia kiumbe huyo mefanywa kuwa chombo cha kukidhia mahitaji ya ngono katika jamii hiyo ya Magharibi.

Wanawake wanaojiheshimu baada ya kudhalilishwa na magaidi hao wa Kiwahabi

Katika hali hiyo bado kuna makundi yanayotumia jina la Uislamu na kinyume kabisa na mafundisho ya dini hiyo ya mbinguni, kuamiliana na mwanamke kama mnyama. Mtazamo wa makundi ya ukufurishaji kumuhusu mwanamke ni ishara tosha kwamba makundi hayo yako kinyume kabisa na dini ya Uislamu na ubinaadamu. Moja ya matendo machafu na yaliyo dhidi ya dini ya Uislamu yanayofanywa na makundi ya kigaidi na ukufurishaji hususan Daesh (ISIS) kumuhusu mwanamke, ni suala zima la ndoa ya jihadi (Jihadun-Nikah.) Kama tulivyosema katika kipindi kilichopita, istilahi hiyo kwa mara ya kwanza iliibuka mwaka 2013 kupitia fatwa za mashekhe bandia wa Kiwahabi hasa wakati wa kujiri kwa vita vya kubuniwa na madola yenye kupenda kujitanua dhidi ya Syria hapo mwaka 2011. Baada ya hapo, vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii ya Mawahabi vikajikita katika kuitangaza na kuieneza istilahi hiyo. Mmoja wa mashekhe hao wa Kiwahabi kwa jina la Muhammad Al-Arifi wa nchini Saudia aliandika fatwa yake katika mtandao wa kijamii wa Twitter ambapo aliwataka wanawake na mabinti kwenda nchini Syria kwa ajili ya kuwakidhia mahitaji ya kingono wapiganaji wa kigaidi wanaopigana dhidi ya serikali ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa al-Arifi, wanawake ambao wangefanya hivyo angalau kwa nusu saa tu, basi wangepata ujira wa pepo.

************************************

Baada ya fatwa hiyo wasomi wengi wa Kisuni kote duniani walisimama na kulaani fatwa hiyo na kuitaja kuwa ni aina nyingine ya uzinzi na kueneza ufuska wa wazi katika jamii ya Kiislamu.

Wanawake waliobebeshwa mimba na magaidi hao wa Kiwahabi

Kutokana na mashinikizo mengi kutoka kwa maulama wa Kisuni hatimaye msomi huyo wa Kiwahabi wa nchini Saudia, alilazimika kulegeza msimamo na kuibatilisha fatwa yake hiyo sambamba na kutangaza kwamba siye yeye aliyeihalalisha. Hata hivyo kadhibisho la al-Arifi halikuweza kuzuia makundi ya kigaidi yanayofanya jinai nchini Iraq na Syria kuacha kuendeleza ufuska huo, bali kinyume chake wanachama wengi wa magenge hayo wameendelea kuienzi fatwa hiyo hadi leo. Aidha kwa kisingizio cha fatwa hiyo, wanawake na mabinti kutoka nchi tofauti walihadaika na kujikuta wakisafiri kwenda Iraq na Syria kwa ajili ya kuwakidhia matamanio ya kimwili magaidi hao wakufurishaji na kudhania kwamba kufanya hivyo kunamkurubisha muhusika na radhi za Mwenyezi Mungu.

Baadhi ya wanawake wa Kiwahabi waliosafiri kwenda kufanya ufuska huo wa ndoa ya jihad

Wanawake kutoka Tunisia, Libya, Misri, Chechnya na baadhi ya nchi za Ulaya ni kati ya wanawake walioshiriki ufuska huo kwa kwenda Syria na Iraq na kuwa pamoja na magaidi. Aidha kwa upande mwingine magaidi hao walikuwa wakiwalazimisha wanawake wenye uraia wa Syria na Iraq kushiriki uchafu huo ambapo wale waliokataa waliuawa. Katika fremu hiyo wanachama wa makundi hayo waliwataka wazazi wa mabinti hao kuwakabidhi kwao kwa hiari na kwamba kinyume na hivyo wangehesabika kuwa ni maadui wa Mungu, wanaostahiki kuuawa. Kwa mfano tu baada ya wanachama wa genge la Daesh (ISIS) kuudhibiti mji wa Mosul nchini Iraq, walitoa fursa ya mwezi mmoja tu kwa wanawake wote wa mji huo kujisalimisha wenyewe kwa magaidi hao ili waolewe kwa lazima. Kama hiyo haitoshi wakufurishaji hao wasio na utu mioyoni mwao walianzisha msako wa nyumba kwa nyumba katika kuwatafuta wasichana na wanawake ambao hawakuitikia mwito huo na kudai kwamba, wanawake ni lazima watii amri ya Mungu na Mtume wake ya kuolewa na wanachama hao wa kigaidi. Kutokana na wanawake wengi kupinga amri hiyo waliuawa kwa umati na magaidi hao mjini Mosul. Abu Anas al-Libi, mmoja wa magaidi wa genge la Daesh amekiri kuua wanawake 150 mjini Fallujah Iraq kutokana na kwamba wengi wao walipinga kushiriki ufuska wa Jihadu Nikaah na wanachama wa kundi hilo la Kiwahabi.

****************************************

Kupitia fremu ya ufuska huo wa Jihadu Nikaah, mmoja wa mamufti wa Kiwahabi kwa jina la Sheikh Nasr al Omr alitangaza kwa kusema: "Mujahidina nchini Syria wanaweza kuwaoa maharimu wao hata dada zao wenyewe ikiwa wanawake wasio maharimu hawatopatikana." Mwisho wa kunukuu. Aidha Jihadu Liwatwi na Jihadu Nikahn-Nafsi ni sehemu nyingine ya fatwa za masheikh wa Kiwahabi katika kuwahalalishia ufuska magaidi wakufurishaji wanaopigana vita na kufanya jinai huko Iraq na Syria. Hata hivyo kama tulivyosema, hakuna dini au dhehebu lolote duniani ambalo limewahi kuhalalisha vitendo hivyo vya kishetani katika jamii, kwa ajili ya kuondoa matamanio ya kimwili. Kwa hakika makundi ya kigaidi na Kiwahabi si tu kwamba hayaamini mafundisho ya dini ya Uislamu, bali pia hayafahamu hata kidogo misingi ya ubinaadamu. Hii  ni katika hali ambayo Mtume Muhammad (saw) alitumwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kumuokoa mwanadamu kutokana na vitendo hivyo visivyo vya ubinaadamu na vya kishetani. Aidha dini ya Uislamu imekiwekea kanuni na sheria maalumu kila kitendo ikiwemo ndoa na kwa ajili hiyo haifai mtu yeyote hususan mufti wa Kiwahabi kutoa fatwa ghalati iliyo kinyume na mafundisho ya dini hii ya mbinguni na kubadili misingi ya sheria zilizoainishwa. Ni suala lisilo na shaka yoyote kwamba kwa mujibu wa sheria za dini tukufu ya Uislamu Jihadun-Nikaah, ni ndoa batili. Moja ya sababu muhimu za kutokuwa halali ndoa hiyo ni uwezekano wa wanawake wa ndoa hiyo kuolewa na wanaume tofauti bila kuainishwa kipindi chochote cha eda. Kwa mujibu wa ndoa hiyo kwa siku moja mwanamke mmoja anaweza kufanya ngono na wanaume kadhaa. Hii ni katika hali ambayo Qur'ani na Suna ya Mtume Muhammad (saw) zimemuwekea mwanamke kitenganishi cha eda kati ya wanaume wawili kupitia sheria na masharti maalumu yaliyoainishwa, ambapo kinyume na hivyo haijuzu mwanamke kuolewa na mwanamume zaidi ya mmoja bila kupitia kipindi hicho cha eda. Hii ikiwa na maana kwamba, baada ya mwanamke kutengana na mwanamume, anatakiwa kwanza kukaa eda yenye muda maalumu. Na eda hiyo inatofautiana kulingana na sababu husika. Kwa mfano muda wa mwanamke aliyefiwa na mume wake sio sawa na eda ya mwanamke alitengana na mume wake kutokana na talaka.

****************************************

Kwa ufafanuzi kidogo ni kwamba eda ya mwanamke aliyefiwa na mume wake ni miezi minne na siku 10, huku eda ya talaka tatu za mihula ikiwa ni kusafika kwa tohara ya eda ya mwezi ili aweze kuolewa tena. Hata hivyo isisahulike kuwa suala hilo lina sheria na masharti yake maalumu kama ilivyobainishwa katika elimu ya fiqhi. Hata hivyo wanachama wa makundi ya kigaidi kwa kutumia Jihadun-Nikah, wanamchangia mwanamke mmoja bila kuwepo kitenganishi chochote cha kumtoharisha kabla ya kukutana naye kimwili. Ni kwa kutokuwa na kitenganishi hicho cha tohara, ndio maana ndoa hiyo ikahesabiwa kuwa ni batili kwa mujibu wa sheria za Uislamu. Hata hivyo isisahulike kuwa suala hilo haliihusu tu dini ya Uislamu, bali dini zote za mbinguni zimepinga vikali ndoa ya aina hiyo. Hii ni kwa kuwa ndoa hiyo haina tofauti yoyote na ufuska unaotekelezwa katika nchi za Kimagharibi ambapo kwa siku moja mwanamke anaweza kutembea na wanaume kadhaa tofauti bila kuwepo eda ya kumtoharisha. Aidha sababu nyingine inayoifanya ndoa hiyo kuwa haramu ni kitendo cha mamufti hao wa Kiwahabi kuhalalisha kufanya mapenzi na wanawake maharimu. Kwa mujibu wa Qur'ani na suna za Mtume Muhammad (saw), kufanya mapenzi na maharibu ni kitendo kilichoharamishwa na kupigwa maufuku sambamba na kuwekewa sheria kali kwa mtu mwenye kufanya uovu huo. Aya ya 23 ya Suratun-Nisai zinaelezea uharamu wa kumuoa mwanamke ambaye ni maharimu kwa kusema: "Mmeharimishiwa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu, na shangazi zenu, na khaalati zenu, na binti wa ndugu mume, na binti wa dada, na mama zenu walio kunyonyesheni, na dada zenu kwa kunyonya, na mama wa wake zenu, na watoto wenu wa kambo walio katika ulinzi wenu walio zaliwa na wake zenu mlio waingilia. Ikiwa hamkuwaingilia basi hapana lawama juu yenu. (Pia mmeharimishwa) wake wa watoto wenu walio toka katika migongo yenu. Na kuwaoa pamoja dada wawili isipokuwa yale yaliyokwisha pita. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu." Watu maharimu ni kama vile mama, mtoto wako wa kuzaa, mama mkubwa au mdogo, shangazi, dada, mtoto wa kaka, mtoto wa dada na wengine wengi ambao wameainishwa na sheria za Kiislamu. Ndio maana fatwa hizo za mamufti wa Kiwahabi zikakabiliwa na upinzani mkubwa wa maulama wa ulimwengu wa Kiislamu. Miongoni mwa maulama hao ni Sheikh Ahmad Omar Hashim, mjumbe wa kamati ya maulama wakubwa wa al-Azhar nchini Misri aliyesema: "Fatwa hizo zinakinzana na akili. Hakuna mtu yeyote anayeweza kuzikubali. Ni vigumu kutumia dini kutoa fatwa katika kuhalalisha jambo ambalo Mwenyezi Mungu tayari ameliharamisha na mienendo hiyo humfanya mtu kutoka katika dini. Hii ni kwa kuwa kuhalalisha haramu ya Mungu ni sawa na mtu aliyehalalisha haramu yake na vitendo vyote viwili haviruhusiwi." Mwisho wa kunukuu. Swali la msingi ni hili kwamba, je, pamoja na jinai na mauaji yote hayo ya makundi ya ukufurishaji, ni kwa nini madola ya Magharibi hayatoi kauli yoyote ya kulaani mienendo hiyo na badala yake daima yamekuwa yakiyaunga mkono kwa hali na mali magenge hayo?

Ndugu wasikilizaji sehemu ya 27 ya makala haya inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

 

 

 

Tags