Apr 25, 2017 02:27 UTC
  • Jumanne, tarehe 25 Aprili, 2017

Leo ni Jumanne 27 Rajab 1438 Hijria sawa na 25 Aprili, 2017.

Siku kama ya leo miaka 1451 iliyopita, Mtume Mtukufu wa Uislamu Muhammad Mustafa (s.a.w) alibaathiwa yaani kupewa Utume na Mwenyezi Mungu. Kipindi hicho Mtume Muhammad (s.a.w) alikuwa na umri wa miaka 40. Mtume Muhammad (saw) alianza kutafakari na kudurusu maumbile ya dunia akiwa bado mdogo na daima alikuwa akifirikia njia za kunyanyua juu utukufu wa mwanadamu. Alikuwa maarufu kwa ukweli, uaminifu na kutenda mema. Jumla ya sifa hizo njema zilimfanya Muhammad (s.a.w) kuwa shakhsia mwenye hadhi na heshima kubwa katika jamii. Alipitisha muda wake mwingi katika ibada na kutafakari katika Pango la Hiraa. Malaika Jibrail alimteremkia Muhammad akiwa katika pango hilo na kumpa bishara ya kwamba ameteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mtume wake kwa walimwengu wote. Tangu siku hiyo Mtukufu huyo alipewa jukumu kubwa la kuongoza wanadamu na kupambana na ujahili, ukafiri, dhulma na uonevu. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa siku hii adhimu.

Siku kama ya leo miaka 971 iliyopita alizaliwa faqihi, mfasiri wa Qur'ani na msomi wa Kiislamu na Kiirani, Jarullah Zamakhshari. Mwanazuoni huyu pia alikuwa gwiji katika elimu za hadithi na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Msomi huyo wa Kiirani ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Muqaddimatul Adab na Asasul Balagha. Kitabu muhimu zaidi cha Jarullah Zamakhshari ni tafsiri ya Qur'ani ya al "Kash'shaf".

Kaburi la Zamakhshari

Siku kama ya leo miaka 525 serikali ya mwisho ya Kiislamu barani Ulaya ilisambaratika huko Granada. Baada ya kudhihiri dini ya Uislamu na kupanua mamlaka yake katika maeneo ya Asia na kaskazini mwa Afrika, jeshi la Waislamu liliingia kusini magharibi mwa Ulaya kupitia lango bahari la Jabal Tariq (Gibraltar) na kulitawala eneo hilo kwa kipindi cha karne 8. Eneo hilo ambao kwa sasa linaitwa Uhispania, wakati huo lilijulikana kwa jina la Andalusia. Katika kipindi cha ustawi wa ustaarabu wa Kiislamu eneo la Granada lilikuwa kituo kikuu cha ustaarabu huo na makao makuu ya kueneza Uislamu hususan barani Ulaya. Dola la Kiislamu la Andalusia liliangushwa kupitia njia ya kueneza ufuska na maovu baina ya watawala na makhalifa wa wakati huo.

Mabaki ya ustaarabu wa Kiislamu katika mji wa Granada

Katika siku kama ya leo miaka 210 iliyopita, aliaga dunia Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa msomi na fakihi mtajika wa Kishia. Alizaliwa mjini Najaf huko Iraq na kuanza kujihusisha na masomo ya dini tangu katika kipindi cha utoto wake. Awali alisoma masomo ya utangulizi kwa baba yake na kisha baadaye akahudhuria masomo kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama sayyid Mahdi Bahr al-Uluum. Baadaye Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa alianza kufundisha na kuandika vitabu na kufanikiwa kuwalea wanafunzi wengi na vile vile kuandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali.

Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Ordibehesht mwaka 1359 Hijiria Shamsia, Marekani ilishambulia kijeshi ardhi ya Iran kwa kutumia helikopta na ndege kadhaa za kivita. Serikali ya Marekani ilifanya mashambulizi hayo baada ya kushindwa njama zake mbalimbali za kutaka kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu wa Iran. Lengo la mashambulio hayo lilikuwa ni kutaka kuwakomboa majasusi wake waliotiwa mbaroni wakati wa kutekwa ubalozi wa Marekani hapa nchini uliokuwa pango la kijasusi. Licha ya kuweko mipango makini, kutumiwa vyombo vya kisasa kabisa na mazoezi mengi yaliyofanywa katika eneo linalofanana na hilo ili kuhakikisha operesheni hiyo inafanikiwa, lakini mashambulizi hayo yalikatishwa na tufani kubwa ya mchanga iliyotokea Tabas na kupelekea kuanguka baadhi ya ndege, kushika moto helikopta za Marekani na kufa baadhi ya askari wa nchi hiyo huku waliobakia wakiikimbia ardhi ya Iran.

Mabaki ya helikopta za Marekani, Tabas

Miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo, Wamarekani laki mbili walifanya maandamano mjini Washington wakiendeleza upinzani wao dhidi ya mashambulizi ya nchi hiyo huko Vietnam. Maandamano hayo yalikuwa miongoni mwa vielelezo vikubwa vya upinzani wa wananchi wa Marekani dhidi ya siasa za kichokozi za serikali ya nchi hiyo huko Vietnam. Katika vita vya Vietnam vilivyoanza mwaka 1964 Marekani ilituma askari laki tano nchini humo ambako maelfu miongoni mwao waliuawa na kujeruhiwa. Kwa sababu hiyo wananchi wa Marekani walizidisha upinzani dhidi ya vita hivyo na mwaka 1975 Marekani ililazimika kufunga virago na kuondoka Vietnam kutokana na mashinikizo ya ndani na ya kimataifa na kushindwa mara kwa mara jeshi la nchi hiyo katika medani za vita. 

Vita vya Vietnam