May 11, 2017 02:17 UTC
  • Alkhamisi, Mei 11, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 14 Shaaban mwaka 1438 Hijria mwafaka na tarehe 11 Mei mwaka 2017 Miladia.

Miaka 799 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 14 Shaaban mwaka 639 Hijria, alifariki dunia Ibn Yunus, faqihi, tabibu na mwanahesabati mashuhuri wa Kiislamu. Msomi huyo wa Kiislamu alitumia sehemu kubwa ya umri wake kujifunza elimu kutoka kwa baba yake na wanazuoni wengine wa zama hizo. Baada ya kustafidi na elimu katika zama ambazo wasomi wa Kiislamu walitia fora katika elimu ya sayansi na sanaa, Ibn Yunus alianza kufunza katika vyuo mbali mbali mjini Cairo nchini Misri. Mbali na kutabahari katika nyuga za fiqhi, sayansi na utabibu, msomi huyo wa Kiislamu alikuwa mtaalamu wa muziki. Miongoni mwa athari muhimu za mwanazuoni huyo wa Kiislamu, ni kitabu alichokipa jina la "Al-Asraaru Sultaniya"  kinachozungumzia masuala ya unajimu.

Ibn Yunus

Siku kama ya leo miaka 321 iliyopita, yaani tarehe 11 Mei mwaka 1696 Miladia, alifariki dunia mwandishi na mwanafikra wa Kifaransa, Jean de La Bruyère. De la Bruyère alizaliwa mwaka 1645 Miladia, na kuwa wakili baada ya kutabahari katika elimu ya sheria. Hata hivyo baadaye aliachana na kazi ya uwakili na akaanza kufanya kazi serikalini, huku akijifunza kuhusu masuala ya maadili na tafakuri ya mwanadamu katika zama zake. Mwandishi huyo wa Kifaransa ameandika vitabu vingi vinavyohusu utamaduni, mila na mienendo ya mwanadamu. Kadhalika ametoa mchango mkubwa katika uga wa fasihi ya Kifaransa.

Jean de La Bruyère

 

Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, Salvador Felipe Dali, mchoraji na mchongaji wa sanamu za mawe na mtaalamu wa sanaa ya maandishi au Graphic Arts wa Kihispania alizaliwa. Alianza kuonyesha kipaji chake katika sanaa ya uchoraji akiwa kijana mdogo na kwa muda mfupi tu akawa mashuhuri kimataifa. Salvador Felipe Dali alikuwa na kipaji cha aina yake na ubunifu katika taaluma hizo na ndiye anayehesabiwa nchini Uhispania kuwa muasisi wa uchoraji wa kisasa. Mwanasanaa huyo stadi aliaga dunia mwaka 1989.

Salvador Felipe Dali

Na siku kama ya leo, miaka 150 iliyopita, sawa na tarehe 11 mwezi Mei mwaka 1867 Miladia, iliundwa nchi ya magharibi mwa bara Ulaya ya Luxembourg. Awali Luxembourg ilifahamika kama Lutxenbourg katika karne ya 10 hadi 15, ikiwa sehemu ya Utawala wa Roma. Hadi katikati ya karne ya 19, nchi hiyo ilikuwa ikiendeshwa na serikali na watawala wa madola yaliyokuwa na nguvu na ushawishi wakati huo Ulaya. Luxembourg ambayo inazungukwa na Ubelgiji, Ufaransa na Ujerumani, ilitangazwa kuwa nchi huru katika Kongamano la London lililofanyika Mei 11 mwaka 1867 katika mji huyo mkuu wa Uingereza na kuanza kutambulika kimataifa.

Luxembourg