May 18, 2017 04:30 UTC
  • Alkhamisi, Mei 18, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 21 Shaaban 1438 Hijria mwafaka na tarehe 18 Mei mwaka 2017 Miladia.

Siku ya leo katika kalenda ya Kiirani ni kumbukumbu na maadhimisho ya Omar Khayyam msomi, malenga na Aarif mashuhuri wa Kiirani. Abul-Fat'h Omar bin Ibrahim Khayyam Neishabouri alikuwa mwanafalsafa, mwanahisabati, tabibu, malenga na mwandishi mkubwa wa Kiirani aliyeishi mwishoni mwa karne ya tano na mwanzoni mwa karne ya sita Hijria. Omar Khayyam aliondokea kuwa mashuhuri zaidi kutokana na kubobea katika elimu za tiba, nujumu na hisabati. Hata hivyo mwishoni mwa umri wake alijulikana zaidi kutokana na mashairi yake. ***

Omar Khayyam

Miaka 213 iliyopita katika siku kama ya leo, Baraza la Seneti la Ufaransa lilipasisha Napoleon Bonaparte kuwa mfalme wa Ufaransa na kwa utaratibu huo kwa mara nyingine tena mfumo wa kidikteta ukatawala nchi hiyo ikiwa ni miaka 15 imepita baada ya ushindi wa Mapinduzi makubwa ya nchi hiyo ya bara Ulaya. Hata hivyo, mfumo wa kifalme ulifikia mwisho miaka kumi baadaye, sawa na tarehe 11 Aprili mwaka 1814, baada ya Napoleone kushindwa katika vita vyake na nchi za Ulaya na kubaidishwa.***

Napoleon Bonaparte

Katika siku kama ya leo miaka 187 iliyopita, ilianza operesheni ya jeshi la Ufaransa kwa shabaha ya kuikalia kwa mabavu Algeria. Kisingizio cha Charles wa Kumi mfalme dikteta wa wakati huo wa Ufaransa cha kutoa amri ya kufanywa  mashambulio hayo, ilikuwa ni kufuatia vitisho vilivyokuwa vimetolewa kabla na mtawala wa wakati huo wa Algeria akiitaka Ufaransa ilipe deni la nchi hiyo la Franc milioni saba. Hata hivyo, kinyume na ilivyodhania Paris, wananchi wa Algeria walisimama kidete katika kukabiliana na mashambulio hayo. Ijapokuwa Ufaransa ilifanikiwa kuikalia kwa mabavu Algeria na kupora maliasili na utajiri wa nchi hiyo, lakini hatimaye nchi hiyo ya Kiafrika ilijipatia uhuru wake mwaka 1962.***

Bendera ya Algeria

Siku kama ya leo miaka 145 iliyopita, alizaliwa Bertrand Russell mwanafalsafa na mwanahesabati mashuhuri wa Uingereza. Russell baada ya kumaliza masomo yake ya awali alijiunga na Chuo Kikuu cha Cambridge mjini London. Russell alikuwa mpinzani mkubwa wa Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia, pamoja na vita vya Marekani dhidi ya Vietnam, na hata kufikia hatua ya kufungua mashtaka dhidi ya viongozi wa Marekani, mashtaka yaliyopewa jina lake la Russell. Msomi huyo alifanikiwa kupokea tuzo ya fasihi ya Nobel mwaka 1950 na kufariki dunia mnamo mwaka 1970. ***

Bertrand Russell

Miaka 43 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya India ilifanya jaribio la kwanza la nyuklia katika jangwa la Rajasthan magharibi mwa nchi hiyo na jirani na mpaka wake na Pakistan. Kwa utaratibu huo, India ikawa nchi ya sita baada ya Marekani, Umoja wa Kisovieti, Ufaransa, Uingereza na China katika uwanja huo wa nyuklia. Miaka 24 baadaye yaani mwaka 1998 India ilifanya majaribio mengine matano ya nyuklia na kufanikiwa kutengeneza silaha za atomiki.***

Majaribio ya nyuklia

Na miaka 40 iliyopita kwa mujibu wa azimio la Mkutano wa Kumi na Mbili wa Baraza Kuu la Kamati ya Kimataifa ya Makumbusho, siku hii iliainishwa na kutangazwa kuwa "Siku ya Makumbusho Duniani." Moja ya malengo muhimu ya baraza hilo lilikuwa ni kupanuliwa makumbusho katika kona mbalimbali duniani, kuweko ushirikiano wa kila upande wa majumba ya makumbusho ulimwenguni kwa shabaha ya kufikia malengo ya kiutamaduni na wakati huo huo kuzuia kuangamizwa athari za kale za kiutamaduni. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, lengo  la kuanzishwa sehemu kwa jina la makumbusho ni kuhifadhi athari za kale za vizazi vilivyopita kwa ajili ya vizazi vijavyo. ***

 

Siku ya Kimataifa ya Makumbusho

 

Tags